Isaya 27: Usomaji; Mjadala

September 17, 2020 in Usomaji/ Vidokezo by TGVS

Usomaji wa Biblia kwa Mpango
Kitabu cha Isaya sura ya 27.

Isaya 27


1 Katika siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.
Katika siku hiyo; Shamba la mizabibu la mvinyo, liimbieni.
Mimi, Bwana, nalilinda, Nitalitia maji kila dakika, Asije mtu akaliharibu; Usiku na mchana nitalilinda.
Hasira sinayo ndani yangu; Kama mibigili na miiba ingekuwa mbele zangu, Ningepanga vita juu yake, Ningeiteketeza yote pamoja.
Au azishike nguvu zangu, Afanye amani nami; Naam, afanye amani nami.
Siku zijazo Yakobo atatia mizizi; Israeli atatoa maua na kuchipuka; Nao watajaza uso wa ulimwengu matunda.
Je! Amempiga kama hilo pigo la hao waliompiga, au ameuawa kama walivyouawa wao waliouawa na yeye?
Umemwadhibu kwa kiasi, ulipomfukuza; ukampepeta kwa upepo mkali katika siku ya upepo wa mashariki.
Basi, uovu wa Yakobo utatakaswa hivyo, na hayo ndiyo matunda yote ya kumwondolea dhambi yake; afanyapo mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa, hata maashera na sanamu za jua havitasimama tena.
10 Kwa maana mji ulio na boma umekuwa peke yake, makao yaliyoachwa na ukiwa kama jangwa; huko ndiko atakakolisha ndama, na huko ndiko atakakolala, na kuyala matawi yake.
11 Matawi yake yatakapokauka yatavunjwa; wanawake watakuja na kuyachoma moto; kwa maana hawa si watu wenye akili; kwa sababu hiyo yeye aliyewaumba hatawahurumia, yeye aliyewafanya hatawasamehe.
12 Tena itakuwa katika siku hiyo, Bwana atayapiga-piga matunda yake toka gharika ya Mto hata kijito cha Misri, nanyi mtakusanywa mmoja mmoja, enyi wana wa Israeli.
13 Tena itakuwa katika siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa, nao waliokuwa karibu na kuangamia katika nchi ya Ashuru watakuja; na hao waliotupwa katika nchi ya Misri; nao watamsujudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu.


 

Mwongozo wa Biblia
23-BSG-27J (Isaya 27).
MASWALI YA KUJADILI.

[1] Nini maudhui makuu katika sura hii?  Je sura hii inakufundisha nini kuhusu Mungu?

[2] Aya ya kwanza (Isaya 27:1) ni mwendelezo wa sura ya 26. Katika sura hii, nabii anaanza kwa maneno haya: “Katika siku hiyo Bwana, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu Lewiathani, nyoka yule mwepesi, na Lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.” Lewiathani ni nini?

[3] Umeshawahi kutafakari jinsi Mungu akulindavyo usiku na mchana bila kukudai chochote? Unadhani kwa nini anafanya hivyo kwako? Ungetakiwa kumshukuru kwa mema akutendeayo ungempa nini au ungemfanyia nini?

[4] Nini maana ya “shamba la mizabibu?” Kuna tofauti kubwa sana katika mfano wa “Shamba la mizabibu” lilivyotumika katika Isaya 5:1-7 ukilinganisha na Isaya 27:2-6. Kwanini mtazamo wa Bwana ni rafiki katika sura hii? Bwana, ansema atalinda shamba lake la Mzabibu: “atalitia maji kila dakika, Asije mtu akaliharibu; Usiku na mchana atalilinda.” (Isa. 27:3). Linganisha mtazamo wa Bwana kuhusu ‘Shamba Lake la Mizabibu” katika Isaya sura ya 5:

Isaya 5:5-7a — 5 “Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba Langu la mizabibu; Nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; 6 Nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; Nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. 7 Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza.”

[5] “Siku zijazo Yakobo atatia mizizi; Israeli atatoa maua na kuchipuka; Nao watajaza uso wa ulimwengu matunda” (aya ya 6). Je, umewahi kufikiria jinsi siku zako za usoni zitakavyojaa neema na mafanikio? Je, taarifa hizo zimekuongezea ari katika kufanikisha mipango ya maisha uliyojiwekea au zinakukatisha tamaa?

[6] “Basi, uovu wa Yakobo utatakaswa hivyo, na hayo ndiyo matunda yote ya kumwondolea dhambi yake.” (aya ya 9a). Ushindi juu ya dhambi ni jambo linaloonekana kama ndoto kwa wengi. Ikiwa Mungu anajua siku moja utashinda dhambi inakuwaje vigumu kwako kuamini juu ya ahadi hiyo? Siri ya kushinda dhambi ni nini? Je kushinda dhambi kunategemea juhudi za nani?

[7] “Matawi yake yatakapokauka yatavunjwa; wanawake watakuja na kuyachoma moto” (aya ya 11a). Kwa nini shughuli ya kuchoma moto matawi ya miti iliyokuwa kwenye ngome ya adui walipewa wanawake? Wanawake wana jukumu gani muhimu walilopewa kanisani kwako ili kupambana na adui Shetani?

[8] “Tena itakuwa katika siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa” (aya ya 13a). Waisraeli walitumia tarumbeta kuwaita watu kuja katika makusanyiko matakatifu (Hesabu 10). Tarumbeta ilitumika hata katika siku kuu ya upatanisho (Walawi 16) kutangaza hukumu ya Mungu, kupiga mbiu, n.k. ndiyo maana Isaya anatumia ‘tarumbeta’ hapa ili kusisitiza wito na ukusanyaji upya kwa Wayahudi kurudi katika nchi ya Palestina. Ni kwa jinsi gani ‘tarumbeta’ inatumika tena katika zama hizi za mwisho kualikwa walimwengu kukata shauri kwa ajili ya marejeo ya Yesu Kristo? (rejea Ufunuo 14:6-12). Ni kwa namna gani unaweza kushiriki katika mwito huu mtakatifu?

[9] Wongofu katika kurejeshwa:Nao watamsujudu Bwana katika mlima mtakatifu huko Yerusalemu” (aya ya 13c). Hiki ndicho kipengele muhimu sana katika ukusanyaji upywa wa Israeli. Ukusanyaji huu ungekuwa kazi bure kama haukujumuisha uamsho wa kiroho miongoni mwa Wayahudi ambao walimuasi Yehova Mungu—waliyetanga mbali naye, jambo lilipelekea mateso kwao na kupelekwa utumwani Babeli. Siku zote, lengo la Mungu katika kutuadhibu ni kuboresha toba, wongofu, na ibada yetu Kwake. Je umewahi kuadhibiwa na Mungu? Je ulijifunza nini katika uzoefu huo? Je unafanya nini ili kuwahimiza wengine wamrudie Mungu wao?

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email