Isaya 53: Mwongozo wa Maombi

October 13, 2020 in Mwongozo wa Maombi by TGVS

Mwongozo wa Maombi Unaoshabihiana na “Mpango wa Usomaji Biblia” wa leo: Isaya 53/ Dhima: Yesu Anaita! /23-BSG-53B, (Isaya 53:5)/ Wimbo: Jesus is tenderly calling thee home, [Mwandishi: Fanny Crosby]


 

Andiko Msingi: ““Bali alijeruhiwa sababu ya makosa yetu, alichubuliwa sababu ya hatia na udhalimu wetu; adhabu ya [iliyohitajika ili kupata] amani na ustawi wetu ilikuwa juu Yake, na kwa mapigo [yaliyomjeruhi] sisi tumeponywa na kupata uzima.” (Isaya 53:5, AMP)

Maelezo ya Ufunguzi: Isaya 53 hutupatia mtazamo dhahiri wa Msalaba wa Kalvari kuliko andiko linginelo katika Agano la Kale. Hebu tuanze kwa nukuu hii—“Yule ambaye amepata mtazamo dhahiri wa msalba, ataichukia dhambi, na kupenda haki. Mashaka yake yatatoweka katika nuru inayoakisiwa kutoka kwenye msalaba wa Kalvari.” Wapendwa, leo tunapokuja katika Kipindi hiki cha Maombi, tunaalikwa kuitikia kwa namna chanya ujumbe wa msalaba wa Yesu. Tunafanya hili kwa kushughulika na dhambi zetu: tunapoichukia dhambi, na kuipenda haki!

Hebu sikiliza maneno haya yaliyovuviwa — “Usipoteza muda, hebu usiruhusu siku nyingine ipotelee umilele, lakini kama ulivyo, licha ya udhaifu wako, kutofaa kwako, upuuziaji wako, usichelewe kuja sasa.… Wito wa Yesu kuja Kwake, kupewa taji ya utukufu isiyoharibika, uzima, uzima wa milele unaolingana na uzima wa Mungu havijawa vishawishi wa kutosha kukuongoza kumtumikia Yeye kwa upendo usiogawanyika.…

Usiendelee tena kuwa upande wa Shetani. Fanya mabadiliko makini ya dhati kupitia neema uliyopewa na Mungu. Usiendelee tena kutukana neema Yake. Anasema kwa machozi, “Wala hamtaki kuja Kwangu mpate kuwa na uzima.” (Yohana 5:40). Sasa Yesu anakualika, akibisha hodi kwenye moyo wako ili aingie. Je utamruhusu aingie ndani? [That I May Know Him, uk. 56].

Maadili ya Kukuza: Kuchukia dhambi; Toba ya kweli; kujitahidi kupata Haki.

Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Dhambi za Kuepuka / Kukiri: Dhambi zote — Dhambi ambazo zimetendwa moja kwa moja dhidi ya Mungu; zile ambazo zimetendwa moja kwa moja dhidi ya watu wengine; na zile ambazo zimetendwa moja kwa moja dhidi yako mwenyewe. Ni kweli kwamba dhambi zote zimetendwa dhidi ya Mungu (Zaburi 51:4). Mahali pazuri pa kuanza kujichunguza itakuwa Amri Kumi (Kut. 20).

Jambo la Kumshukuru Mungu Kwalo: Unabii kuhusu Yesu Kristo; Huruma ya Yesu Kristo; Kifo cha hiari cha Yesu Kristo; Kusudi la Kifo Chake Kalvari; Utakatifu wa Yesu Kristo; Mbadala wa Yesu Kristo; Utii wa hiari wa Yesu Kristo; Upendo wa Yesu Kristo; Upole wa Yesu Kristo; Ukamilifu wa Yesu Kristo; Wokovu kutoka kwa Yesu Kristo; Kuja Kwa Yesu Kristo Mara Ya Pili.

Watu wa Kuombewa: Maadui wa Msalaba wa Yesu Kristo—waongolewe (waokolewe) na “waje kuifahamu ile kweli” (1 Tim 2:4).

Masuala ya Kuombea: Masomo juu ya Msalaba & hatari kubwa ya kumpuuza Kristo (Ebr. 2:3; 6: 4-6); Vipengele vya kihisia vya mateso; Hitaji la mwongozo wa Mungu katikati ya majaribu; Unyenyekevu; Haki ya Kristo.

Ahadi ya Leo: “Hakika ameyachukua masikitiko yetu (magonjwa, udhaifu, na fadhaa), Amejitwika huzuni na maumivu yetu [ya adhabu]’ (Isaya 53:4a, AMP) “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)

Hatua ya Maamuzi: Tumia Muda fulani kujichunguza Binafsi: Je unaona maishani mwako yoyote miongoni mwa Dhambi Mahususi zilizoorodheshwa hapo juu? Ikiwa ndivyo, ungama na kutubu mara moja– “Dhambi ambazo hazijafanyiwa toba na kuachwa hazitasamehewa, na kufutwa kwenye vitabu vya kumbukumbu, bali zitasimama ili kushuhudia dhidi ya mdhambi husika katika siku ya Mungu.” (The Faith I Live By, uk. 211). Tumia muda fulani kuombea mambo yaliyoorodheshwa hapo juu; mwombee mtu fulani anayekabiliana na dhambi hizi. Endapo una Mahitaji ya Maombi, tafadhali yaandike hapa chini, na mtu fulani atayaombea. Mungu akubariki!


 

Sala: Baba, tunakushukuru sana kwa neno Lako katika Isaya 53. Tunakushukuru kwa Msalaba wa Yesu Kristo. Tunakushukuru kwa ahadi za thamani katika neno Lako, kwamba “Tukikiri dhambi zetu,” Wewe ni “mwaminifu na wa haki kutusamehe dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote.”

Tunakushukuru kwa unyenyekevu wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo: ingawa Yeye ni / alikuwa Mungu (mmoja na Wewe), hakufikiria ‘kuwa sawa huu na Mungu’ ni jambo la kushikamana nalo au kuling’ang’ania; badala yake akawa kama mwanadamu, na akazaliwa mwanadamu! Alijivua mwenyewe (fursa zote za kiungu, ukuu, na hadhi), ili kuchukua nafasi ya mtumishi (mtumwa), ili kutufikia na kutuokoa! Kwa hivyo alikuja na kutuosha miguu, na kutuokoa! Na kisha, alijishusha na kujinyenyekeza (hata kwenda chini zaidi) na akaelekeza utii Wake kwa kiwango kingine – kifo, hata kifo cha msalaba! Upendo wa ajabu sana ulioje!

Tusaidie kuzingatia Msalaba kwa jinsi ulivyo: uthibitisho wa tabia Yako. Kwamba Wewe ni mtakatifu na Sheria Yako ni takatifu! Kwamba kwa sababu unatupenda sana hukumkatalia Mwanao, lakini umemtuma afe kwa ajili yetu! Kwamba unachukia dhambi, na mshahara wa dhambi ni mauti (Rum 6:23). Nakiri leo kuwa mimi ni mdhambi, namhitaji Yesu! Nisaidie kujifunza maisha na mfano ambao Yesu ameweka mbele yangu. Nisaidie kuchukia dhambi na kupenda haki.

Naomba ujumbe wa msalaba unifundishe kukupenda zaidi; kuwa na nia ya Kristo – mtazamo na kusudi lilelile na roho ya unyenyekevu iliyokuwa katika Kristo Yesu. Nisaidie kutangaza ujumbe huu mbali na kwingi, na kuwaalika watu waukaribie Msalaba wa Yesu.

Njoo BWANA Yesu maishani mwangu na uongoze mawazo yangu, maneno, matendo. Nisafishe na niandae kwa ajili ya Ufalme Wako, Amina.

Comments
Print Friendly, PDF & Email