Yeremia 20: Mwongozo wa Ibada.

November 15, 2020 in Mwongozo wa Ibada by TGVS

Mwongozo wa Ibada Unaoshabihiana na “Mpango wa Usomaji Biblia” wa leo: Yeremia 20/ Dhima: Kukamatwa kwa Yeremia na Kufedheheshwa Hadharani/ 24-BSG-20A, (Yeremia 20:1-7)/ Wimbo: Lo, the storms of life are breaking! [Mwandishi: Henry Alford, (1810–1871)]


 

UCHUNGUZI: Wito wa Mungu kuhusu kustahimili katikati ya mateso — (Zab. 119:87; Mat 10:22,28; 1 Kor. 4:12; 2 Thes 1:4; Yak. 5:8).

TAFAKARI: Katika sura hii tuna ahima (mdokezo) wa mateso ya kwanza ya Yeremia. Sura hii inaweza kuanishwa kama ifuatavyo — [A] Kifungo cha Yeremia (1–2): Pashuri, kuhani mkuu mwovu wa Yuda, anamshikilia Yeremia na anashurutisha achapwe na kuwekwa katika mkatale usiku kucha. [B] Uhatinishwaji wa Yeremia (3–6): Baada ya kuachiliwa, nabii huyu anatabiri kiyama cha kuhani huyo — rafiki zake wote watauawa au kuchukuliwa kwenda Babeli (3–5); yeye pamoja na familia yake watatwaliwa kwenda utumwani, na kamwe hawatarejea (20:6). [C] Malalamiko ya Yeremia kwa BWANA– “Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika” (7); “Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa” (8); “Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite” (10); “Na ilaaniwe siku niliyozaliwa!” (14). [D] Kikwazo cha Yeremia: Yeremia anataka kuondoka, lakini hawezi, maana neno la Mungu huchoma moyoni mwake kama moto (9). [E] Faraja: “Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda.” (11).

MAANA YA KIIBADA: Kwa nini Pashuri alimchukia Yeremia kiasi hicho? Makuhani walikuwa katika kiini cha upinzani dhidi ya Yeremia (Yer. 11:21) sababu mojawapo ni kwamba walikuwa miongoni mwa walengwa wa ukosoaji wake mkali (Yer. 1:18). Walikuwa sehemu ya mifumo ya mamlaka kuu Yerusalemu ambayo Yeremia alitangaza kwamba ilikuwa inakaribia mwisho wake (Yer. 18:18). Zingatia Utoshelevu wa Ulinzi wa Yeremia: “Hapa kuna mtu wa imani thabiti, na mwenye hotuba iliyojaa ujasiri na utulivu. Pengine kweli akawa na fadhaa; ilhali akiwa amesetwa kama alivyo na chuki nyingi kiasi hicho, akiwa ameletwa karibu sana na uovu mbaya kabisa wa moyo wa mwanadamu. Lakini, kwa upande mwingine, analo hili kama faraja yake, kwamba kadiri watu waovu wanavyomkaribia, ndivyo anavyojikuta kuwa karibu na Mungu. Hii ndiyo huduma ambayo waovu huwapatia mashahidi wa Mungu, kwamba, kadiri wanavyowatesa, ndivyo wanavyowasukuma wasogee kwenye Msaada wao mkuu.” [H. D. M. Spence-Jones, Ed., Jeremiah, The Pulpit Commentary, (London; New York: Funk & Wagnalls Company, 1909), 1:478].

SAUTI YA INJILI: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, hupaswi kushangaa pale watu wanapokutukana na kukunenea uongo kila aina ya mambo maovu kwa sababu Yangu. Yesu Kristo alikabili dhuluma kama hizo. Kwa kweli, hupaswi kutegemea lolote tofauti (Mat. 10:18; 24:9; Yohana 15:20). Nakualika umwige Yesu Kristo kwa kuishi kwa haki hata kama uko katikati ya mateso. Watu wanapokuchukia, wakakukashfu, wakakutukana, na kukutesa– furahia! Maana nina “thawabu kuu” kwa ajili yako mbinguni (Mat 5:11-12; Efe. 1:3).

Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka kumwiga Yesu Kristo kwa kustahimili mateso.


 

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina Langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.” “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu.” (Mathayo 10:22, 28)

Comments
Print Friendly, PDF & Email