Yeremia 40: Maswali na Majibu

December 5, 2020 in Mwongozo wa Biblia by TGVS

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Yeremia 40, (24-BSG-40J)/ Maswali na Majibu


 

[1] Jadili kifupi matukio makuu yanayotokea baadaya ya Anguko la Yerusalemu? (Yer. 40-42). Nebuzaradani, kamanada wa jeshi la Babeli, alimkuta Yeremia amefungwa minyororo miongoni mwa mateka wengine kwenye kambi ya wafungwa huko Rama, akamwachilia. Gedalia anateuliwa kuwa liwali wa Yuda. Gedalia anauliwa na Ishmaeli. Yohanani anamuuliza Yeremia endapo watu wangepaswa kubaki Yuda ama kwenda Misri.

[2] Elezea jinsi Yeremia alivyotendewa akiwa mikononi mwa Wakaldayo? — (40:1–5). “Yeremia alikuwa huru kwenda kila mahali alikotaka. Kama angeenda Babeli pamoja na mateka wengine, Nebuzaradani aliahidi kumlinda (cf. 39:12). Endapo angechagua kubaki Yuda, angeweza kustakimu popote ambapo angependa. Hata hivyo, kama angekaa Yuda, Nebuzaradani alipendekeza kwamba aende … kwa Gedalia na kuishi pamoja naye. Bila shaka liwali Gedalia angempatia ulinzi na mahitaji ya kimwili ambayo Yeremia angehitaji kama angebaki. Yeremia alipoondoka Rama ili kusafiri umbali wa maili tatu hadi Mizpa – kituo cha utawala wa Yuda baada ya Yerusalemu kuangamizwa—Nebuzaradani alionesha ukarimu wake kwa kumpatia Yeremia vyakula na zawadi.” [Charles H. Dyer, The Bible Knowledge Commentary: An Exposition of the Scriptures, 1985, 1, 1186].

[3] Zingatia utambuzi wa kushangaza wa kamanda wa kipagani kuhusu mahubiri ya Yeremia. Alisema nini? “Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, Bwana, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa; Naye Bwana ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi Bwana, wala hamkuitii sauti Yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi.” (Yeremia 40:2–3)

[4] Nani ambaye mfalme wa Babeli alimteua kuwa liwali wa miji ya Yuda? (40:5) — Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani.

[5] Ni mambo gani matatu bayana yaliyoandaliwa kwa ajili ya Yeremia baada ya kuachiliwa kwake? — (40:4-5)

  • Nebuzaradani alimpatia uchaguzi wa kwenda Babeli pamoja naye au mahali popote ambapo angependa.
  • Alipendekeza kwamba Yeremia aende kwa Gedalia, liwali mpya (kama angechagua kubaki Yerusalemu); au aende popote katika Yuda
  • Pia alimpatia nabii chakula na zawadi (pengine pesa).

Zingatia: Kwa sababu Yeremia hakuwa na hatia ya kuiasi Babeli, alipewa chaguzi/uhuru huu kama udhihirisho wa kutambua utiifu wake kwa serikali ya Babeli.

[6] Ni uchaguzi gani ambao Yeremia hatimaye alichagua? — (40:6) Alibaki Yuda, katika nchi ya ahadi. Utume wake: kuwahudumia watu. “Basi, Yeremia akaenda kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa, akakaa pamoja naye kati ya watu wale waliosalia katika nchi.” (Yeremia 40:6)

[7] Nini tukijuacho kuhusu Mizpa? — (40:6) Ilikuwa makao makuu mapaya ya serikali alipopachagua Nebukadneza. Mizpa ulikuwa mji katika eneo la kabila ya Benjamini, ambapo Samweli alikuwa mwamuzi, na ambapo Sauli alichaguliwa kuwa mfalme (angalia 1 Sam. 7:15-16; 10:17-25).

[8] Jadili mwitikio wa wapiganaji wapinzaji wa Yuda kufuatia uteuzi wa Gedalia kama liwali— (40:7). Waliomba ufanyike mkutano: “ndipo wakamwendea Gedalia huko Mizpa; nao ni hawa, Ishmaeli, mwana wa Nethania, na Yohana na Yonathani, wana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanhumethi, na wana wa Efai, Mnetofa, na Yezania, mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.” (Yer. 40:8)

Zingatia: “Kuanzia 40:7 hadi 42:2 Yeremia hatajwi kwenye kisa hiki. Wengi miongoni mwa maafisa ya jeshi pamoja na watu wao walikuwa wamekimbia oparesheni kali ya Babeli baada ya Yerusalemu kuanguka, na walikuwa wakijificha kwenye “eneo la wazi,” pengine katika vilima vya Uyahudi. Inawezekana wengine walikuwa wakiendelea kupigana kama askari wa msituni, bila kuridhia kujisalimisha kwa adui. Hata hivyo, waliposikia kwamba Nebukadneza amemteua Gedalia, mmoja wa watu wao, kama liwali, waliungana pamoja naye huko Mizpa. Gedalia alikuwa amewekwa kuwasimamia maskini kabisa katika nchi hiyo na wale ambao hawakupelekwa uhamishoni.” [F. B. Huey, Jeremiah, Lamentations, The New American Commentary, (Nashville: Broadman & Holman Publishers, 1993), 16:350].

[9] Pale ambapo Gedalia, liwali mpya alikutana na wapiganaji hawa, wito wake ulikuwa nini kwao? — (40:9) Wekeni chini silaha zenu, rudini nyumbani, tulieni; jisalimisheni chini ya utawala wa Babeli.

[10] Je ahadi ya Gedalia kwao ilikuwa ipi? — (40:10a) Nitawawakilisheni vyema mbele ya mfalme wa Babeli.

[11] Ipi ilikuwa changamoto ya Gedalia kwa maafisa hao? — (40:10b) Kusaidia kutengeneza mashamba na kujenga upya miji ya Yuda

[12] Nani aliyerejea Yuda? Ni maeneo gani mengine walikotoka Wayahudi na kukusanyikia Mizpa? — (40:11) Walirejea kutoka Moabu, Amoni, Edomu, na nchi zingine zote walikokuwa wamekimbilia. Walistakamani na kuanza kilimo pamoja na mchakato wa kujenga upya taifa lao na uchumi wao.

[13] Ni ujumbe gani muhimu ambao Yohanani alimletea Gedalia? — (40:13-14) Alimtaarifu kwamba Ishmaeli alikuwa anapanga kumuua. Zingatia: Ishmaeli alikuwa amekodiwa na Mfalme Baalisi wa Amoni ili amuue liwali. Ila, kinachosikitisha, Gedalia hakuamini taarifa hizi, achilia mbali kuhoji/kuchunguza madhumuni ya Ishmaeli.

[14] Jinsi gani Yohanani alipendekeza namna ya kushinda njama za Ishmaeli? — (40:15)

“Yohanani alikutana kwa faragha pamoja na Gedalia na kujitolea amuue Ishmaeli. Alipanga kufanya hivyo kwa siri ili asijue mtu yeyote nani aliyehusika. Yohanani alidhani Ishmaeli angepaswa kuondolewa kwa ajili ya ustawi wa Yuda. Kama Ishmaeli angeruhusiwa kuangamiza maisha ya Gedalia, hiyo ingesababisha Wayahudi wote katika nchi ya watawanyike na kuangamia. Gedalia alimwamuru Yohanani asifanye jambo hilo kwa sababu alikuwa na hakika kwamba ulikuwa uvumi tu wa Ishmaeli usio na ukweli. Gedalia alikuwa mtu mwenye heshima aliyefanya kosa la kufisha pale aliposhindwa kutambua vyema kusudi la Ishmaeli.” [Charles H. Dyer, The Bible Knowledge Commentary: An Exposition of the Scriptures, 1985, 1, 1187].


 

MWISHO.

Comments
Print Friendly, PDF & Email