Danieli 2: Maswali na Majibu

February 10, 2021 in Mwongozo wa Biblia by TGVS

DANIELI 2: MASWALI NA MAJIBU

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Danieli 2, (27-BSG-2J)/ Maswali na Majibu


 

[1] Je lini Mungu alimpatia Nebukadneza ndoto hii? “Katika mwaka wa pili wa kumiliki kwake Nebukadreza” (2:1).

[2] Hivi unaweza kutambua mstariwakati wa ndoto ya Nebukadneza? (2:1) Zingatia kwamba huu Mwaka wa Pili kwa kweli ni Mwaka wa Tatu wa utawala wa Nebukadneza kwa vile mwaka wake wa kutwaa madaraka hauhesabiwi.

ZINGATIA: Hadi wakati huu, Danieli alikuwa amemaliza miaka yake mitatu ya mafunzo (Angalia Danieli 1:5, 18). Aidha, katika Dan. 2:48, mfalme anamfanya Danieli awe mwenye hekima mkuu, ikionesha kwamba alikuwa amekamilisha mafunzo yake. Kumbuka kwamba mapema katika sura ya Dan 2:5-6, tayari Danieli alikuwa ameainishwa kuwa sehemu ya kundi hili – wenye hekima.

[3] Kwa nini Mungu alimpatia mfalme wa Babeli ndoto hii? Ili kufunua siri; ili kubainisha yale ambayo yangetokea katika “siku za mwisho” (2:28)

[4] Wapo ambapo mfalme aligeukia ili kupata msaada? “waganga, na wachawi, na wasihiri, na Wakaldayo” (2:2)

ZINGATIA:Waganga walitenda maajabu, neno hili likiwa na maana mbaya; yaani, walitumia kaida zote za kishirikina na desturi za wabashiri, na watazamao nyakati za kuzaliwa, na vitu kama hivyo. Mafalaki walikuwa ni watu waliojifanya kutabiri matukio kwa kuchunguza nyota. Sayansi ya ushirikina, ya astrolojia ilikuwa imeshamirishwa sana na mataifa ya Mashariki hapo kale. Wasihiri ni wale waliodai kuwa na uwezo wa kufanya mawasiliano na wafu. Kwa muktadha huu, tunaamini, ndipo neno “msihiri” hutumiwa daima kwenye Maandiko. Wakaldayo waliotajwa hapa walikuwa kikundi cha wanafalsafa sawa na maganga na mafalaki leo, waliojihusisha na uchunguzi wa sayansi asilia na upiga ramli. Makundi au fani hizi zote zilienea Babeli. Matokeo yaliyolengwa na kila moja yalikuwa fanani—kuelezea mafumbo na kutabiri matukio—tofauti kuu kati yao ikiwa ni njia waliyotumia ili kutafuta kutimiza malengo yao. Utata wa mfalme ulikuwa ndani ya uwezo wa kila mmoja kuelezea; hivyo aliwaita wote. Kwa mfalme, hili lilikuwa jambo muhimu. Alikuwa amefadhaika sana, na hivyo alijikita katika kutafuta ufumbuzi wa mtanziko wake kutoka kwenye hekima ya himaya yake.” [Uriah Smith, The Prophecies of Daniel and the Revelation, (Nashville, Tennessee: Southern Publishing Association, 2009), 29–30].

[5] Kwa nini nini chanzo ambacho Nebukadneza alikiendea ili kupata msaada hakikuweza kumpatia awini aliyoitaka? (Dan. 2:2, 27-28). Huku akiwa amedhamiria kutafuta ufumbuzi wa ndoto hiyo, mfalme aliendea chanzo pekee cha taarifa alichodhani kilikuwa kinapatikana—ahari wa kiroho na viongozi wa siku zake. Lakini lilikuwepo tatizo moja: mfalme alikuwa ameisahau ndoto yake!

Sababu ya pili: Kiasili, ndoto yake ilikuwa imetokea kwa“Mungu wa Mbinguni.” Hakuna namna yoyote ambapo wapagani hawa wenye hekima wangeweza kutanzua mafumbo haya ya Yehova Mungu—maana “mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu” (Kumb. 29:29). Na muhimu zaidi, “mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni” (1 Kor. 2:14).

[6] Wakati ule wenye hekima wa mfalme waliposhindwa kudhihirisha na kufafanua ndoto, amri ya Nebukadneza ilikuwa ipi? “Basi kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, akaona hasira nyingi, akatoa amri kuwaangamiza wenye hekima wote wa Babeli.” (Danieli 2:12)

ZINGATIA: Mafalaki na waganga wa Babeli walidai kuwa na nguvu turufushani, lakini pale waliposhindwa kuibainisha ndoto ya mfalme, walioneshwa kuwa walaghai dhaifu. Kama mfalme angekuwa ameikumbuka ndoto yake, wangeweza tu kufinyanga ufafanuzi bandia. Katika ghadhabu yake, Nebukadneza aliamuru wenyewe hekima wote wauawe—hata wale ambao hawakuwepo. Miongoni mwa wale ambao hawakuwepo kwenye mkutano wa kwanza pamoja na mfalme ni mateka mcha-Mungu aitwaye Danieli, ambaye punde tu alikuwa amefunzwa kwa ajili ya utumishi wa mfalme.

[7] Danieli alipogundua kuhusu amri ya kifo, alimwomba nini mfalme? “Basi Danieli akaingia, akamwomba mfalme ampe muda, kisha yeye atamwonyesha mfalme tafsiri ile.” (Danieli 2:16)

[8] Je Danieli aliwaomba marafiki zake wafanye nini? “Ndipo Danieli akaenda nyumbani kwake, akawapasha habari kina Hanania, na Mishaeli, na Azaria wenzake; ili waombe rehema kwa Mungu wa mbinguni kwa habari ya siri hiyo, ili kwamba Danieli na wenzake wasiangamizwe pamoja na wenye hekima wa Babeli.” (Danieli 2:17–18)

ZINGATIA: “Katika wakati huu wa kujaribiwa, Danieli alikuwa mtulivu. Alirejea kwenye nyumba yake, akawatafuta marafiki zake, na kwa pamoja wakaomba rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni. (“Mungu mbinguni” ni cheo kinachotumika kwa ajili ya Mungu mara sita katika Dan.: 2:18–19, 28, 37, 44; 5:23, mara tisa katika Ezra, na mara nne katika Neh. Kwingineko katika AK hujitokeza tu katika Mwa. 24:3, 7; Zab. 136:26; Yona 1:9.) Rehema ni mwitikio wa Mungu kwa mahitaji ya mtu. Danieli alitambua hali yake ya kukosa msaada katika mazingira husika naye akamgeuki aMungu katika staamani, akitegemea Bwana akidhi hitaji lake.” [J. Dwight Pentecost, The Bible Knowledge Commentary: An Exposition of the Scriptures, 1985, 1, 1334].

[9] Bwana alipomdhihirishia Danieli ndoto, alimpatia nani sifa na ustahiki? “Nakushukuru, nakuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu, uliyenipa hekima na uwezo, ukanijulisha hayo tuliyotaka Kwako; maana umetujulisha neno lile la mfalme.” (Danieli 2:23) “Lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho. Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi” (Danieli 2:28)

ZINGATIA:Danieli aliitikia kwa usahihi kwa kumpatia Mungu sifa. Alikiri kwamba Mungu ndiye Mungu wa wisdom, akijua mwisho tangu mwanzo, na ndiye Mungu wa uweza, maana lolote analoazimu, anaweza kulifanya. Danieli alianza na kuhitimisha ombi Lake ilhali akizungumzia hekima na uweza wa Mungu (cf. v. 23).

Ushahidi wa uweza Wake huonekana katika udhibiti Wake wa matukio (hubadili majira na nyakati) na ya mustakabali wa mataifa (huwahuluku wafalme na kuwahuzulu). Nebukadneza alikuwa kwenye enzi kwa sababu Mungu aliazimu kumtumia hapo ili atimize mapenzi Yake.

Ushahidi wa hekima ya Mungu huonekana katika kuwakirimia hekima wenye hekima (v. 21b) na katika kudhihirisha mambo ya kina na ya giza (v. 22). Nuru hukaa pamoja na Mungu kwa maana kwamba vitu vyote viko dhahiri Kwake, japo wanadamu wamezungukwa giza. Mungu anajua na pia anaweza kufunua mambo yajayo. Mungu, wala siyo urajufu wa Danieli, ndiye aliyempatia ndoto na ufafanuzi wake. Sala ya Danieli ya sifa ilihitimishwa kwa shukrani kwamba Mungu alikuwa amemdhihirisha ndoto ya mfalme kwa hawa wanne waliokuwa wamemdhamani. (J. Dwight Pentecost, The Bible Knowledge Commentary: An Exposition of the Scriptures, 1985, 1, 1334).

[10] Ni vitu gani alivyosema Danieli kwamba mfalme aliviona kwenye ndoto yake? “Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha.” (Danieli 2:31) “Nawe ukatazama hata Jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande.” (Danieli 2:34)

ZINGATIA: Kitu cha kwanza alichoona mfalme ni sanamu kubwa iliyotengenezwa kwa viasili vifuatavyo vya madini – 1. Kichwa kilikuwa cha dhahabu/ 2. Kifua na Mikono vilikuwa vya fedha/ 3. Tumbo na mapaja vilikuwa vya shaba/ 4. Miguu ilikuwa ya chuma/ 5. Nyayo zilikuwa za chuma na udongo.

Baada ya hapo, mfalme akaona jiwe lilichokatwa bila kutumia mikono ya mwanadamu. Katika hatua hii, Mfalme Nebukadneza bila shaka alikuwa amepigwa butwaa akiwa ameketi ukingoni mwa kiti chake cha utawala. Danieli akawa amesimulia ndoto hiyo kwa usahihi kama ambavyo Mungu alikuwa amempatia. Sasa mfalme akangojea kwa shauku, akijiuliza kile ambacho ndoto hii ilimaanisha. Danieli aliendelea kueleza fasiri hiyo kama ambavyo Bwana alikuwa amemdhihirishia, na nasi tungefanya vema kuiamini kama vile alivyokuwa ameiwasilisha. Njia pekee salama ya kufasiri Biblia na unabii ni kuruhusu Biblia ijieleze yenyewe.

[11] Je kichwa cha dhahabu huwakilisha nini? “Na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mkononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.” (Danieli 2:38)

ZINGATIA: Kutoka vv. 36, Danieli anaanza kuwasilisha ufafanuzi. Nebukadneza ni kichwa cha dhahabu. The king was regarded as the head of the state. Hii ndiyo sababu Nebukadneza aliiwakilisha Babeli, himaya iliyoanzisha unabii huu. Zingatia kwamba unabii huu huanzia wakati wa Danieli.

Anaanza kumwambia mfalme kwamba yeye ni mfalme wa wafalme, lakini pia anamkumbusha kwamba kuna Mungu wa mbinguni aliyempatia huu ufalme na mamlaka, nguvu, na utukufu, ili asiruhusu mfalme apate namna yoyote ya kiburi au hali ya kujitukuza nafsi katika suala husika, bali kumkumbusha juu ya Mungu wa kweli.

Fasili ya 38 hutuambia kidogo jinsi ambavyo himaya yake iliyokuwa kubwa na kuhusu mawanda aliyotawala. Babeli ilitawala dunia kuanzia 606 K.K. hadi 538 K.K. Hizi hapa taarifa chache kuhusu ufahari wa Babeli. Ilikuwa mraba kamili wa maili 60/km 98.4 katika mzingo, maili 15/km 24.6 kila upande, pamoja na kuta zifikiazo kimo cha futi 350/m 106.68 na futi 87/m 26.52 kwa unene. Ilikuwa na shimo kubwa kuzunguka ukuta huo, lenye ukubwa sawa na ukuta wenyewe. Kila mtaa ulikuwa na urefu wa maili 15/ km 24.6 km na upana wa futi 150/ mita 45.72. Pia mto wa maili 30/km 49.2 ulipita katikati ya mji huo na kuta za mito zilizoshabihiana na malango 250 ya shaba tupu, bustani zake zining’iniazo zilizopanda kazi baada ya ngazi hadi kufikia kimo cha kuza za nje, na orodha hii inaendelea. Biblia huielezea kama utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo,” (Isaya 13:19). Hakika huu ulikuwa mjii mkuu stahiki wa ufalme wa Babeli. Tutajifunza zaidi kuhusu ufalme huu katika mafunuo yajayo ya unabii.

[12] Je himaya ya Babeli ingedumu milele? Hapana. “Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.” (Danieli 2:39)

ZINGATIA: Uturufu wa Babeli usingedumu milele. Falme zilizofuata, adhali kuliko Babeli, zingeshika hatamu zao. Kama ambavyo fedha ni adhali kuliko dhahabu, hivyo ufalme uliofuatia Babeli ulifurahia utukufu pungufu. Ilhali ikiongozwa na Koreshi katika 539 K.K., himaya ya Umedi-Uajemi iliishambulia Babeli na kuingamiza. Wamedi na Waajemi walikuwa wakiutawala ulimwengu tangu 539-331 K.K. Wakati wa utawala wao, kodi zote zilipaswa kulipwa kwa kutumia fedha.

[13] Ni metali gani ingewakilisha ufalme uliofuatia Umedi-Uajemi? “Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.” (Danieli 2:39)

ZINGATIA: Ufalme wa shaba wa Uyunani ulitwaa mamlaka wakati Aleksanda Mkuu ilipowashambulia Wamedi na Wajemi kwenye vita huko Arbela mnamo mwaka 331 K.K., na Uyunani ikasalia kwenye utawala hadi takriban mwaka 168 K.K. Askari wa Kiyunani waliitwa “nakshi za shaba” kwa sababu silaha zao zote zilikuwa za shaba. Zingatia jinsi ambavyo madini ama metali zilizofuata kama ilivyo kwenye sanamu husika zilivyokuwa na thamani duni, lakini zenye kudumu zaidi kuliko zilizotangulia.

[14] Ni metali ipi huwakilisha ufalme wa nne? “Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta.” (Danieli 2:40)

ZINGATIA: Himaya ya chuma ya Rumi iliwashambulia Wayunani mnamo mwaka 168 K.K. na kufurahia uturufu wa ulimwengu hadi Rumi ilipotekwa na Waostrogothi mnamo mwaka 476 B.K. Rumi ni ufalme ulioshamiri ulimwenguni wakati Yesu Kristo alipozaliwa. Zingatia jinsi ambavyo Danieli alitabiri kwa usahihi kamili miaka elfu kabla kuhusu historia ya ulimwengu. Kuinuka na kuanguka kwa falme hizi za ulimwengu—Babeli, Umedi-Uajemi, Uyunani, na Rumi—kumetabiriwa bayana katika Biblia na kuthibitishwa na vitabu vya historia.

[15] Nini kingetokea baada ya anguko la Himaya ya Rumi? “Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo wa mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; lakini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope. Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.” (Danieli 2:41–42)

ZINGATIA: Wakati ule Himaya ya Rumi ilipoanza kuanguka mnamo mwaka 476 B.K., nafasi yake haikuchukuliwa na utawala mwingine wa ulimwengu. Badala yake, makabila ya kijahili yaliishambulia Himaya ya Rumi na kuigawa—kama tu ambavyo Danieli alikuwa ametabiri. Kumi miongoni mwa makabila haya yaliunda Ulaya ya sasa. Haya yalikuwa Waostrogothi, Wavisigothi, Wafranki, Wavandali, Waalemania, Wasueve, Waanglo-Saksoni, Waheruli, Walombadi, na Wabugundi. Saba miongoni mwao bado yangalipo hata leo huko Ulaya. Mfano, Waanglo-Saksoni wakawa Waingereza, Wafranki wakawa Wafaransa, Waalemania wakawa Wajerumani, na Walombadi wakawa Waitaliano.

[16] Je falme 10 hizi zitakuja kufanikiwa kuungana? Hapana! “Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile chuma kisivyoshikamana na udongo.” (Danieli 2:43)

ZINGATIA: Kupitia ndoa, mashirikisho, na mikataba, wanadamu wamejaribu bila mafanikio kuliunganisha bara la Ulaya. Katika historia yote, viongozi kama vile Charlemagne, Napoleon, Kaiser Wilhelm, Mussolini, na Hitler wametafuta kuijenga himaya mpya ya Ulaya; lakini maneno haya ya Maandiko yamezuia kila mmoja ya watawala watarajiwa. Ufunuo 13 hutuambia kwamba litakuwepo jaribio lingine la kuanzisha ufalme wa dunia nzima, lakini unabii wa Danieli hubainisha wazi kwamba ulimwengu utasalia ukiwa umegawanyika kisiasa hadi mwisho wa historia ya Dunia.

[17] Nani atakayeanzisha ufalme wa mwisho? “Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi Yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” (Danieli 2:44)

ZINGATIA: Ufalme mkuu wa ulimwengu unaofuata utakuwa ufalme wa mbinguni, ambao unabainishwa katika Mathayo 25:31–34 — 31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu Wake, na malaika watakatifu wote pamoja Naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu Wake; 32 na mataifa yote watakusanyika mbele Yake; Naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; 33 atawaweka kondoo mkono Wake wa kuume, na mbuzi mkono Wake wa kushoto. 34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono Wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba Yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.”

[18] Nini ambacho Jiwe huzifanyia falme za dunia? “Nawe ukatazama hata Jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote.” (Danieli 2:34–35)

ZINGATIA: Jiwe ni Bwana Yesu Kristo. Biblia hubainisha wazi kwamba jiwe humwakilisha Yesu Kristo (tazama Isa. 28:16; 1 Kor. 10:4; Luka 20:17, 18), ambaye katika marejeo Yake ya pili ataangamiza falme zingine zote na kuanzia ufalme wa milele. (Tazama Kipengele cha “A” na “X’ kwa maelezo zaidi)

[19] Baada ya kusikia ufafanuzi bayana wa Danieli juu ya ndoto yake, Nebukadneza alisema nini kuhusu Bwana? “Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, Hakika Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme, awezaye kufumbua siri, kwa kuwa wewe uliweza kuifumbua siri hii.” (Danieli 2:47)

ZINGATIA: Mwishoni mwa maelezo ya Danieli, mfalme alishawishika kwamba hakika ndoto yake ilikuwa imetoka katika mamlaka turufushani. Alimkiri Mungu wa Danieli kuwa ndiye Mtawala wa ulimwengu. Aliona nafasi yake katika historia ya ulimwengu, naye akaelewa kwamba mamlaka yake yalikuwa chini ya utawala wa Mungu aliyekuwa amemkasimisha (vss. 46, 47).

Kitendo cha mfalme kusujudu mbele ya Danieli (vs. 46) ulifuata desturi ya Mashariki. Alikuwa tayari kumwabudu Danieli kama aina fulani ya miungu, sawa na Walikaonia na Wamiletia, waliomhesabu Paulo kuwa mungu fulani (Matendo 14:11, 28:6). Paulo alikataa kuabudiwa, nasi tunaweza kuwa na hakika kwamba hata Danieli aliitikia jinsi hiyo (japo hatuna rekodi yoyote ya mwitikio wake). Walakini, mfalme alimfanya Danieli awe liwali juu ya jimbo la Babeli na mkuu wa wenye hekima wote. Daima Mungu huwaheshimisha wale wanaomheshimu (1 Samweli 2:30).

[20] Nini ambacho ombi la Danieli kuhusu marafiki zake hudhihirisha juu ya tabia yake? “Tena, Danieli akamwomba mfalme, naye akawaweka Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wawe juu ya mambo yote ya uliwali wa Babeli; lakini huyo Danieli alikuwa akiketi katika lango la mfalme.” (Danieli 2:49)

ZINGATIA: “Nabii huyu hakutaka kufurahia heshima hizi peke yake. Katika saa yake ya ushindi, aliwakumbuka wale waliokuwa wamejumuika pamoja naye katika maombi. mara tu wadhifa wake ulipokuwa ameamuliwa, alimwomba mfalme awateue marafiki zake watatu ili waongoze masuala ya jimbo ambalo yeye mwenyewe aliwekwa kuwa mtawala husika. Kwa juujuu, ombi lake huonekana kuwa rahisi sana, lakini lazima tukumbuke kwamba huenda Wababeli wazawa walilazimika kuacha nyadhifa zao ili kuwaachia nafasi Wayahudi hawa. Katika kudra ya Mungu, washirika wa sala ya Danieli sasa wamewekwa kuwa washirika wa kupandishwa kwake hadhi. Tofauti na mkuu wa wanyweshaji katika kisa cha Yusufu (Mwa. 40:23), Danieli hakuwasahau marafiki zake.

Mungu alitumia umateka wa Danieli na ndoto ya Nebukadneza ili kumfanya Danieli awe wakala thabiti huko Babeli. Yusufu akiwa huko Misri alipata dhahama ya namna hiyo (Mwa. 50:20). Hiyo miwili ni mifano ni kanuni ya Biblia kwamba “mambo yote Mungu hutendeka kwa ajili ya mema ya wale wampendao Mungu” (Rum. 8:28, NKJV).” –(Adult Sabbath School Bible Study Guide; Pacific Press Publishing Association/ 2004-4; uk. 19)


 

Mwitikio Wangu: Baba mpendwa, sasa natambua kwamba unatawala kikamilifu historia ya ulimwengu na matukio ya dunia! Unadhihirisha siri kuhusu wakati ujao, nami najua kwamba unakuja hivi karibuni! Niko radhi kumruhuso Bwana Yesu Kristo atawale maisha yangu kikamilifu –(sasa, kabla ya kuchelewa kabisa) — kadiri nijiandaavyo kwa ajili ya Ujio wa Pili, Amina.

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email