Danieli 3: Usomaji, Vidokezo, Mjadala.

February 11, 2021 in Usomaji/ Vidokezo by TGVS

Usomaji wa Biblia kwa Mpango/ Kitabu cha Danieli 3/ Dhima: Kukombolewa kutoka kwenye Tanuru Liwakalo Moto: Somo Kuhusu Imani Thabiti (3:1-30).


 

DANIELI 3:

1 Nebukadreza, mfalme, alifanya sanamu ya dhahabu, ambayo urefu wake ulikuwa ni dhiraa sitini, na upana wake dhiraa sita; akaisimamisha katika uwanda wa Dura, katika wilaya ya Babeli.
Ndipo Nebukadreza akatuma watu kuwakusanya maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, ili wahudhurie wakati wa kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadneza aliyoisimamisha.
Ndipo maamiri, na manaibu, na maliwali, na makadhi, na watunza hazina, na mawaziri, na mawakili, na wakuu wa wilaya zote, wakakusanyika ili kuizindua ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha; wakasimama mbele ya ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
Ndipo mpiga mbiu akapiga kelele akisema, Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi,
wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.
Basi wakati huo, watu wa kabila zote walipoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, watu wote na mataifa na lugha wakaanguka, wakaiabudu ile sanamu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha.
Basi baadhi ya Wakaldayo wakakaribia, wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.
Wakajibu, wakamwambia mfalme Nebukadreza, Ee mfalme, uishi milele.
10 Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu;
11 na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao.
12 Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
13 Basi Nebukadreza akatoa amri kwa hasira na ghadhabu, waletwe hao Shadraka, na Meshaki, na Abednego. Basi wakawaleta watu hao mbele ya mfalme.
14 Nebukadreza akajibu, akawaambia, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?
15 Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?
16 Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.
17 Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
18 Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.
19 Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki, na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto.
20 Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
21 Basi watu hao wakafungwa, hali wamevaa suruali zao, na kanzu zao, na joho zao, na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.
22 Basi kwa sababu amri ya mfalme ilikuwa ni kali, na ile tanuru ilikuwa ina moto sana, mwako wa ule moto ukawaua wale watu waliowashika Shadraka, na Meshaki, na Abednego.
23 Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto.
24 Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme.
25 Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.
26 Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.
27 Na maamiri, na manaibu, na maliwali, na mawaziri, waliokuwa wamekusanyika pamoja, wakawaona watu hao, ya kuwa ule moto ulikuwa hauna nguvu juu ya miili yao, wala nywele za vichwa vyao hazikuteketea, wala suruali zao hazikubadilika, wala harufu ya moto haikuwapata hata kidogo.
28 Nebukadreza akanena, akasema, Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.
29 Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.
30 Kisha mfalme akawakuza Shadraka, na Meshaki, na Abednego, katika wilaya ya Babeli.


 

MUHTASARI WA KUFUNDISHIA

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Danieli 3: Muhtasari wa Kufundishia/ Danieli 3, (27-BSG-3E)/ Dhima: Kukombolewa kutoka kwenye Tanuru Liwakalo Moto: Somo Kuhusu Imani Thabiti (3:1-30).

Muhtasari: Nebukadneza aliisimamisha sanamu ya dhahabu. Shadraka, Meshaki, na Abed-Nego wakakataa kuiabudu sanamu hiyo. Walihukumiwa kufa, japo tanuru la moto lilithibitisha kutokuwa na madhara yoyote kwao. Mfalme alishawishika kwamba hakika hakika vijana hawa wanamwabudu Yehova Mungu Aliye Hai, nao wakapandishwa wadhifa.

Wahusika: Mungu, Nebukadneza, Shadraka, Meshaki, Abednego, Mwana wa Mungu.

Andiko Msingi: “Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu. Kisha Nebukadreza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iliyokuwa inawaka moto. Akanena, akasema, Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu, tokeni, mje huku. Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakatoka katika ule moto.” (Danieli 3:24–26)

Neno la Msingi: Theofania — Mhusika wa Nne, Yule “afananaye na Mwana wa Mungu” (Danieli 3:25)

Maandiko Makini: Danieli 3:1, 2, 4-6, 8-12, 13, 14-15, 16, 17, 18, 19-21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30.

Staanani ya Ibada: Tanuru la moto (angalia kipengele cha “Y”)

Mgawanyo wa Mawazo Makuu – Sanamu Kuu (3:1)/ Uwakifishaji (3:2–3)/ Amri (3:4–6)/ Ibada (3:7)/ Mashtaka: Washtaki (3:8); Mashtaka (3:9–12)/ Uchunguzi (3:13–18)/ Hukumu (3:19–23)/ Ukombozi (3:24–27)/ Kupandishwa Hadhi (3:28–30)

Matukio ya Biblia – [Matukio yanayofanyika]: Utumwa wa Babeli (Dan 1:3–3:30)/Kazi ya awali ya unabii ya Danieli (Dan 1:3–3:30)/ Nebukadneza asimamisha sanamu ya dhahabu (Dan 3:1–7)/ Danieli akataa kuiabudu sanamu (Dan 3:1–30)/ marafiki wa Danieli wakataa kuiabudu sanamu (Dan 3:8–18) /marafiki wa Danieli wanaokolewa katika tanuru la moto (Dan 3:19–30).

Dhima za Biblia – Imani na Majaribu ya Moto Maishani (tazama Kipengele cha “H”).

Virai vya Biblia – Baadhi ya watu mashujaa (3:20); Tanuru iliyokuwa ikiwaka moto (3:21); Mwako wa ule moto (3:22); Watumishi wa Mungu Aliye juu (3:26); Watakatwa vipandevipande (3:29); Hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii (3:29)

Mambo ya Kuchunguza Zaidi – Adhabu ya Kifo; “mwana wa Mungu/miungu” (Dan 3:25) –- Linganisha [Mwanzo 6 na Wana wa Mungu; Kumbukumbu 32:8 na Wana wa Mungu]; ibada ya kipagani; Vikwazo vya Kidini; Theofania; mamlaka za Kiraia & miitikio ya waumini kwa uovu; Utii kwa Mungu hasa pale inapomaanisha uzima na mauti!


 

Taarifa za Kushangaza: Durusu ndoto ya Nebukadneza katika Danieli 2.

Hizi hapa ni Taarifa chache katika sura ya 3:

 1. Nebukadneza anatengeneza sanamu ya dhahabu yenye kimo cha futi 90 na upana futi 9.
 2. Mfalme anawaita pamoja viongozi wake wote ili kuhudhuria sherehe ya uwakifishaji sanamu.
 3. Bendi inapopigwa, watu wote wanapaswa kusududia na kuiabudu sanamu ya dhahabu.
 4. Wale wote wanaokataa kusujudu watatupwa kwenye Tanuru liwakalo moto.
 5. Mfalme anagundua kwamba Shadraka, Meshaki, na Abednego wamekataa kuisujudia.
 6. Mfalme anawapatia Waebrania hawa watatu nafasi ya pili ya “kujirudi!”
 7. Jibu lao: “Tutateketea, kama ikihitajika, ila hatuwezi kusujudia chochote isipokuwa Mungu.”
 8. Hasira ya Mfalme: Anaamuru watupwe kwenye tanuru liwakalo moto.
 9. Sasa Tanuru linawaka mara saba kuliko hapo awali.
 10. Muujiza: Mfalme anastaajabu kuona kwamba Waebrania hawa bado wangali hai motoni.
 11. Mtu wa Nne: Anamwona Mtu mwingine anayefanana na “Mwana wa Mungu.”
 12. Kwa amri ya mfalme, watu hao wanne wanatembea kutoka motoni, bila hata kuwa na harufu ya moshi.
 13. Kisha mfalme anapitisha hukumu ya kifo dhidi ya yeyote atakayezungumza chochote kinyume na Mungu wa Waebrania hawa; na watatu hawa watatu wanapandishwa vyeo vya juu.

Wazo Kiini: “Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; Naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” (Danieli 3:16–18)

“Waebrania 11 inaorodhesha majina na matendo ya wanaume na wanawake mashuhuri wa imani, pamoja na Wayahudi hawa watatu (Ebr. 11:34), lakini kwenye fasili ya 36, mwandishi anasema “Na wengine” kisha anawaorodhesha watu wanaoonekana kana kwamba wameoshindwa licha ya imani yao (aya ya 36–40). Neno la Kiyunani humaanisha “wengine wa namna tofauti,” yaani, wengine waliokuwa na imani lakini hawakumwona Mungu akitenda miujiza aliyowafanyia wale walioorodheshwa katika fasili thelathini za kwanza. Daima Mungu hutunza Imani, lakini siyo kila wakati anaingilia kutenda miujiza maalum. Siyo kila mtu aombaye huponywa, lakini daima Mungu hutukirimia nguvu ya kustahimili maumivu na neema ya kukabili mauti bila hofu. Waebrania hawa watatu waliamini kwamba Mungu angeweza kuwaokoa, lakini wangeendelea kumthamani hata kama asingefanya hivyo. Hivyo ndivyo imani inavyopaswa kutenda kazi maishani mwetu. Angalia Habakuki 3:17–19.” [Warren W. Wiersbe, Be Resolute, “Be” Commentary Series, (Colorado Springs, CO: Victor, 2000), 43].

Mausia:Usiwe na miungu mingine ila Mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa Mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao” (Kutoka 20:3–5)


 

MASWALI CHANGAMSHI:

 1. Kwa nini kitendo cha mfalme cha kutengeneza Sanamu ni ukaidi dhidi ya kile ambacho Danieli, katika sura ya 2, alisema kwamba kingetokea? (Durusu Dan. 2:34-35).
 2. Nani aliyetoa taarifa kwa mfalme kwamba marafiki wa Danieli walikataa kuisujudia sanamu yake? (Dan. 3:8)
 3. Nini ambacho pengine kiliwahamasisha washtaki wamwambie mfalme? Zungumzia hali kama hiyo katika Danieli 6.
 4. Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; Naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo…” Je Shadraka, Meshaki na Abednego walikosa imani kwamba Mungu angewaokoa? (Dan. 3:18)
 5. Kirai cha Kiarami hapa kwa ajili ya “mwana wa miungu” (Dan 3:25) ni shabihi na kirai cha Kiebrania “mwana wa Mungu/miungu,” ambacho kijumla ni rejea ya “mjumbe wa kiroho” aliyetumwa kutoka kwa Mungu. Je mhusika huyu wa Nne alikuwa nani ndani ya tanuru la moto?
 6. Kuna uhusiano gani kati ya sanamu katika Danieli 3 na Ufunuo 13:11-18?
 7. Je unadhani ni wazo gani kuu ambalo Mungu anawasilisha kwetu kwa kuijumuisha sura hii katika Biblia Takatifu?
 8. Ni mwitikio gani unaodhani sura hii (Danieli 3) ingepaswa kutuhimiza kufanya?

 

MWISHO: Karibu kwa maswali ya ziada, majibu, ufafanuzi, mjadala, n.k. / Bwana Akubariki.

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email