Danieli 5: Usomaji, Vidokezo, Mjadala.

February 13, 2021 in Usomaji/ Vidokezo by TGVS

Usomaji wa Biblia kwa Mpango/ Kitabu cha Danieli 5/ Dhima: Karamu ya Belshaza na Anguko la Babeli (5:1–31)


 

DANIELI 5:

1 Belshaza, mfalme, aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa akanywa divai mbele ya elfu hao.
Belshaza, alipokuwa akionja ile divai, akaamuru wavilete vile vyombo vya dhahabu na fedha, ambavyo baba yake, Nebukadreza, alivitoa katika hekalu lililokuwako Yerusalemu; ili kwamba mfalme, na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wapate kuvinywea.
Basi wakavileta vile vyombo vya dhahabu, vilivyotolewa katika hekalu la nyumba ya Mungu lililokuwako Yerusalemu; na mfalme na wakuu wake, na wake zake, na masuria wake, wakavinywea.
Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.
Saa iyo hiyo vikatokea vidole vya mkono wa mwanadamu, vikaandika katika chokaa ya ukuta wa nyumba ya enzi ya mfalme, mahali palipokikabili kinara; naye mfalme akakiona kitanga cha ule mkono ulioandika.
Ndipo uso wa mfalme ukambadilika; fikira zake zikamfadhaisha; viungo vya viuno vyake vikalegea; magoti yake yakagongana.
Mfalme akalia kwa sauti kubwa, akaamuru waletwe wachawi, na Wakaldayo na wanajimu. Mfalme akanena, akawaambia wenye hekima wa Babeli, mtu awaye yote atakayesoma maandiko haya, na kunionyesha tafsiri yake, atavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
Basi wakaingia wenye hekima wote wa mfalme; lakini hawakuweza kuyasoma yale maandiko, wala kumjulisha mfalme tafsiri yake.
Ndipo mfalme Belshaza akahangaika sana, uso wake ukambadilika, na wakuu wake wakaona fadhaa.
10 Basi malkia, kwa sababu ya maneno ya mfalme na ya wakuu wake, akaingia katika nyumba ya karamu; malkia akanena, akasema, Ee mfalme, uishi milele; fikira zako zisikufadhaishe; wala uso wako usibadilike.
11 Yuko mtu katika ufalme wako, ambaye roho ya miungu watakatifu inakaa ndani yake; na katika siku za baba yako nuru na ufahamu na hekima zilionekana ndani yake; na mfalme Nebukadreza, baba yako, naam, mfalme, baba yako, akamfanya kuwa mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu;
12 kwa kuwa roho njema kupita kiasi, na maarifa, na ufahamu, na uwezo wa kufasiri ndoto, na kufunua maneno ya fumbo, na kufungua mafundo, zilionekana katika Danielii huyo, ambaye mfalme alimwita Belteshaza. Basi na aitwe Danielii, naye ataionyesha tafsiri.
13 Ndipo Danielii akaletwa mbele ya mfalme. Na Mfalme akanena, akamwambia Danielii, Je! Wewe ndiwe Danielii yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu?
14 Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako.
15 Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.
16 Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
17 Ndipo Danielii akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.
18 Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu;
19 na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha.
20 Lakini moyo wake ulipoinuliwa, na roho yake ilipokuwa ngumu akatenda kwa kiburi, aliuzuliwa katika kiti chake cha enzi, nao wakamwondolea utukufu wake.
21 Akafukuzwa mbali na wanadamu, moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng’ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu, na ya kuwa humweka juu yake yeye amtakaye, awaye yote.
22 Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote.
23 Bali umejiinua juu ya Bwana wa mbingu; nao wamevileta vyombo vya nyumba yake mbele yako; na wewe, na wakuu wako, na wake zako, na masuria wako, mmevinywea; nawe umeisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe; wasioona, wala kusikia, wala kujua neno lo lote; na Mungu yule, ambaye pumzi yako i mkononi mwake, na njia zako zote ni zake, hukumtukuza.
24 Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele zake, na maandiko haya yameandikwa.
25 Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI.
26 Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.
27 TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.
28 PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.
29 Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danielii mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme.
30 Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.
31 Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.


 

MUHTASARI WA KUFUNDISHIA

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Danieli 5: Muhtasari wa Kufundishia/ Danieli 5, (27-BSG-5E)/ Dhima: Karamu ya Belshaza na Anguko la Babeli (5:1–31)

Muhtasari: Hii ni sura ihuzunishayo sana katika Biblia. Siku za Belshaza zimehesabika! Wakati akifanya karamu, anaona “Maandishi Ukutani” na anamwita Danieli – (mtu ambaye Roho wa Mungu anakaa ndani yake) –kwa ajili ya ufafanuzi wa ndoto husika. Anakufa usiku huo wakati Dario Mmede anapouteka mji huo.

Wahusika: Mungu, Belshaza, Wageni (wakuu 1,000); Malkia, Danieli, Dario, Nebukadneza, Mafalaki.

Andiko Msingi: “Ndipo kile kitanga cha ule mkono kikaletwa kutoka mbele yake, na maandiko haya yameandikwa. Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI. Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.” (Danieli 5:24–28)

Neno la Msingi: Kukutwa Amepungua (Dan 5:27).

Maandiko Makini: Danieli 5:1, 2-4, 5-6, 7-9, 10-12, 13-16, 17, 18-21, 22-23, 24-28, 29, 30-31

Staanani ya Ibada: Kuhesabiwa, Kupimwa, Kukatawaliwa (tazama kipengele “Y”)

Mgawanyo wa Mawazo Makuu[a] Upujufu: karamu za ulafi, ulevi na uasherati (5:1); [b] Kutomstahi Mungu wa Israeli (5:2–4); [c] Ibada ya sanamu/Kufuru: kunywa pombe kwa kutumia vyombo vitakatifu wakati wakiisifu miungu ya Babeli (5:4); [d] Maandishi ukutani (5:5–6); [e] Wenye hekima wa Babeli waliitwa lakini hawawezi kuleta ufumbuzi! (5:7–9); [f] Danieli Aitwa/Mhadhara wa Danieli (karipio kali kwa mfalme (5:10–23); [g] Maandishi yafafanuliwa (5:24–28); [i] Kutukuzwa kwa Danieli na Anguko la Babeli (5:29–31)

Matukio ya Biblia – [Matukio yanayofanyika]: Mungu anaandika ukutani (Dan. 5:1–12); Danieli anafafanua maandishi ukutani (Dan. 5:13–29); Nebukadneza anahukumiwa (Dan. 5:20–21); Nebukadneza anafukuziwa mbali (Dan. 5:20–21);  utimamu wa Nebukadneza warejeshwa (Dan. 5:21); Uajemi waiteka Babeli (Dan. 5:30–31); Dario awa mtawala (Dan. 5:30–31); Uajemi yawatawala Wayahudi (Dan. 5:30–6:27); Kurejea Kutoka Uhamishoni (Dan. 5:30–6:27).

[Matukio Yaliyotajwa]: Hekalu laangamizwa na Watu watwaliwa uhamishoni — 2 Wafalme 25:8–21; 2 Nya. 36:18–21; Yer. 39:8–10; 52:12–27 (Dan. 5:2)

Dhima za Biblia – (Kwa ajili ya Dhima na Dondoo ndogo, tazama Kipengele “H”).

Virai vya Biblia –mfalme, wakuu, wake zake, masuria wake (5:2, 23); hekalu la nyumba ya Mungu (5:3); katika saa hiyohiyo (5:5); mfalme alifadhaishwa (5:6); Roho wa Mungu mtakatifu (5:11, 14); hekima ya miungu (5:11); roho njema, maarifa, ufahamu, kufasiri ndoto, kutegua vitendawili, na kuelezea mafumbo (5:12, 14); Mwenyezi Mungu (5:18, 21, 23); ufalme, na ukuu, utukufu na heshima (5:18); watu wote, mataifa, na lugha (5:19); moyo: kuinuliwa/roho: kufanywa mgumu katika kiburi (5:20, 22); Mungu ashikiliaye pumzi yako mkononi Mwake (5:23); MENE, MENE, TEKELI, PERESI (5:25); Usiku huohuo (5:30).

Mambo ya Kujifunza Zaidi: Hasira ya Mungu; Miitikio ya waumini kwa uovu; Mauti ya wasioamini; Mifano ya Biblia kuhusu kiburi; Matokeo ya kiburi; Chanda cha Mungu; Kujazwa Roho Mtakatifu; Mizani na Vipimo – tazama “kukutwa umepungua” (Dan 5:27); Upuuzi wa Ibada ya sanamu.

Taarifa za Kushangaza: Karamu haramu ya Belshaza na Anguko la Babeli (5:1–31). Zingatia taarifa zifuatazo zinazoshangaza: —

 1. Belshaza anaandaa “karamu kubwa” pamoja na viongozi wake.
 2. Anakunywa kutoka kwenye vyombo vitakatifu –kutoka hekaluni.
 3. Wanashikana mikono katika kuzisifu sanamu zao
 4. Ghafla, kitanga kinaonekana kikiandika ukutani.
 5. Mafalaki hawawezi kusoma kile kilichoandikwa: mfalme amepata hofu kuu mno
 6. Danieli, kupitia kwa malkia, analetwa ili asome na kufasiri maandishi haya
 7. Anakataa tunu ya mfalme; kisha…
 8. Anakemea vikali kiburi cha mfalme, ibada ya sanamu, na kukosa kicho
 9. Anasoma fumbo la maandishi husika: “MENE, MENE, TEKELI, PERESI.”
 10. Anamwelezea mfalme maana ya kila neno: MENE –(umehesabiwa): siku za utawala wa Belshaza zimehesabiwa; TEKELI –-(umepimwa): mfalme amepimwa na kubainika amepungua katika hukumu ya Mungu; PERESI — (umegawanyika): ufalme wa Babeli utaganywa kwa Wamedi na Wajemi.
 11. Usiku huohuo Belshaza anaangamizwa, na Dario Mmedi anautwaa ufalme huo.

Wazo Kiini: “Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.” (Danieli 5:26–28, NKJV) “Maneno haya ya hukumu yenye kuogofya, yaliyowasilishwa kwa mfalme huyu mpotovu, huwashutumu wote ambao, kama alivyokuwa Belshaza, wanapuuza fursa zao walizopewa na Mungu. Katika hukumu ya upelelezi ambayo sasa inaendelea (angalia katika Dan. 7:10) watu wanapimwa kwenye mizani ya patakatifu ili kuona endapo tabia yao ya kimaadili na hali ya kiroho inashabihiana na manufaa na baraka ambazo Mungu amewakirimia. Hakuna rufaa dhidi ya maamuzi ya mahakama hiyo. Kwa kuzingatia taadhima ya wasaa husika, wote hawana budi kuwa makini vinginevyo wakati huo wa maamuzi ya mwisho unaohitimisha milele mustakabali wa mwanadamu usije kuwakuta hawajajiandaa na wakiwa “wamepungua.” – (The SDA Bible Commentary, 4:805).

Mausia: “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaye.” (2 Wakorintho 5:10)


 

MASWALI CHANGAMSHI:

 1. Jinsi gani na wakati gani Belshaza alikuwa mfalme? (5:1)
 2. Mfalme anaandaa karamu kuu kwa wakuu wake 1000, wakewe, masuria wake (5:2, 23). Je ilikuwa umuhimu?
 3. Je kuna kosa gani kutumia vyombo vya “hekalu la nyumba ya Mungu?” (5:3).
 4. Belshaza alifadhaika? Hivi hakuwa mfalme mwenye uwezo wa kijeshi mikononi mwake? Je dhambi—dhambi yoyote—ina matokeo gani—kwa mdhambi?
 5. Wakanywa divai, wakaisifu miungu ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya mti, na ya mawe.” Kwa nini miungu hii? (5:4)
 6. Nebukadneza alimfanya Danieli awe “mkuu wa waganga, na wachawi, na Wakaldayo, na wanajimu.” Je ilikuwa kosa kwa Danieli kusimamia mambo aliyoyachukia Mungu? (5:11)
 7. Danieli alikuwa “hekima ya miungu” (5:11). Nini chanzo cha hekima ya kweli? Tunawezaje kuipata?
 8. Je Danieli alikuwa na umri gani wakati wa matukio yaliyobainishwa katika sura hii? (5:12)
 9. Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine.” (5:17) Danieli alizungumza kwa hamaki. Kwa nini alizungumza jinsi hii? Hivi hatupaswi kuwa wapole na wasahibu wakati wote? Unafikiriaje?
 10. Jinsi gani Belshaza mwovu alijua kuhusu “Mwenyezi Mungu?” (5:18, 21, 23).
 11. Jadili maana ya maneno haya – “MENE, MENE, TEKELI, PERESI” (5:25). Je maandishi ukutani yalikuwa katika lugha gani?
 12. Mungu angeweza kuandika katika lugha ya Belshaza. Kwa nini unadhani ujumbe Wake ulimhitaji mfafanuzi?
 13. Usiku huohuo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa” (5:30). Hukumu ya Mungu ilikuwa haraka na halani. Je alipewa muda wa kutubu? Linganisha fasili hii na kiama cha Anania na Safira katika Matendo 5:1-11.
 14. Unadhani ni wazo kuu ambalo Mungu anawasilisha kwa kuijumuisha sura hii kwenye Biblia? Ni mwitikio gani unaodhani ibada hii ingepaswa kutuhimiza kufanya?

 

MWISHO: Karibu kwa majibu, mijadala, ufafanuzi zaidi/ Mungu Akubariki!

Comments
Print Friendly, PDF & Email