Mathayo 2: Ibada

April 25, 2021 in Mwongozo wa Ibada by TGVS

Mathayo 2: Mwongozo wa Ibada/ 40-BSG-2A, (Mathayo 2:1-12)/ Dhima: Mtanitafuta na Kunipata/Wimbo: “Jesus paid it all, All to Him I owe” – [Mwandishi: Elvina M. Hall (1865)].


 

Uchunguzi: Mamajusi kutoka Mashariki (Mat. 2:1-12)/ Kumtafuta Mungu – (Isa 45:19; 1 Nyak. 28:9; Zab. 14:2; 27:8; 32:6; 95:7; Mit. 8:17; Yer. 29:12-14; Mat 7:7- 8; 2 Kor. 6:2; Ebr. 2:3; 3:13; Yak. 4:8).

Tafakari: Soma Mat 2:1-2. “Mamajusi walikuwa wameona nuru shanifu mbinguni katika usiku ule ambapo utukufu wa Mungu ulivigharikisha vilima vya Bethlehemu. Kadiri nuru hiyo ilivyofifia, nyota angavu ikajitokeza, na kudumu angani. Haikuwa nyota stakamani wala sayari, na tukio hilo lilisisimua shauku ya kina zaidi. Nyota hiyo lilikuwa kundi malaika wang’aao kwa mbali, lakini kuhusu hili wenye hekima hawa hawakujua. Hata hivyo walivutiwa kwamba nyota hiyo ilikuwa yenye umuhimu maalum kwao. Waliwaendea makuhani na wanafalsafa, na kuchunguza magombo ya rekodi za zamani. Unabii wa Balaamu ulikuwa umetamka, “Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli.” Hesabu 24:17. Ingewezekana nyota hii ya ajabu imetumwa kama ishara ya Yule Aliyeahidiwa? Mamajusi walikuwa wamekaribisha ukweli uliotumwa kutoka mbinguni; sasa iliangazwa juu yao katika miali angavu zaidi. Kupitia ndoto walielekezwa kwenda kumtafuta Mfalme aliyezaliwa.” (The Desire of Ages, uk. 60).

Maana ya Kiibada: Kumtafuta Kristo: Somo kutoka kwa Wenye Hekima. Wenye hekima hawa wanawasilishwa kwetu hapa kama watafutaji – walikuwa watafutaji wa dhati; walimtafuta Kristo kwa uaminifu, bidii na ustahivu. Mungu aliwasaidia katika kutafuta kwao. Baada ya kumpata Mtoto, utafutaji wao ukafikia mwisho, “wakaanguka wakamsujudia” (Mat 2:11). Wapendwa, yeyote amtafutaye BWANA kwa bidii atampata: “Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.” (Kumbukumbu 4:29) Yeyote amtafutaye kwa bidii Mwana wa Mungu atampata, na kutegemea kuongozwa na Mungu. BWANA aliingilia kati na kuwaonya wenye hekima kuhusu hatari iliyokuwa imekaribia kuja kutoka kwa Herode. Kwa namna hiyohiyo, Mungu ataongoza njia ya nafsi yoyote iaminiyo, ambaye humtafuta kwa bidii: “Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” (Yeremia 29:13).

Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, “Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.” (Mithali 8:17). Pili, nilifanya yote kadiri nilivyoweza ili kukufikia, kupitia Mwanangu Yesu Kristo: alizaliwa ili afe kwa ajili yako; ili kukupatanisha upya Kwangu; ili kukuonesha njia ya Mbinguni. Yesu alitoa maisha Yake hasa kwa ajili yako: “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13) Wenye hekima waliwasilisha zawadi zao zao – dhahabu, uvumba, na manemane kwa Yesu. Je utampatia nini Yesu Kristo? Je umempatia vilivyo bora kutoka kwako? Je umemkubali Yesu kama BWANA na Mwokozi wako? Je utakuwa radhi kufanya hivyo leo?

Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka – 1. Kumtafuta BWANA kwa bidii/ 2. Kumwabudu BWANA/ 3. Kumpatia vitu vyangu vilivyo bora kabisa: muda wangu, hazina zangu, talanta, maneno, silika/ 4. “Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu.” (Isaya 55:6)/ 5. Kufuatilia hali ya kujitoa kwangu: “Yesu alilipa yote, nawiwa Naye; Dhambi ilikuwa imeacha doa jekundu, lakini Yeye akanisafisha nikawa mweupe kama theluji.” (soma Isa 1:18; 1 Yn. 1:9; Ufu. 3:20)

Iweni na Siku Yenye Baraka: “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” (Warumi 12:1)


 

Ibada Kupitia Uimbaji: “Jesus paid it all, All to Him I owe” – [Mwandishi: Elvina M. Hall (1865)]. “Alilipa Bei!” (NK # 119)

  1. Yesu anasema, “Wewe huna nguvu, Kesha ukaombe, Na uje, Mwangu.”

[Pambio] — Alilipa bei, Nawiwa naye; Dhambi ilitia waa, Aliiondoa.

  1. Bwana, nimeona Uwezo wako tu; Waweza ‘takasa, Mioyo michafu.
  2. Sina kitu chema Kudai neema, Hivi nitafua, Mavazi kwa damu.
  3. Ninaposimama Juu ya mawingu, Taji nitaweka, Miguuni pa Yesu!

 

Mwisho: Kutakuwa na Mwongozo wa Maombi katika kipengele kinachofuata (40-BSG-2B). Bwana Akubariki!

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email