Kijana Tajiri

June 4, 2021 in Alfajiri by TGVS

Ibada ya Alfajiri/ Somo: Kijana Tajiri/ Andiko Makini: Marko 10:17-25.


 

Aya Kuu: “Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. ‘Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.’ Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. (Marko 10:21-22)

Maswali ya Moyoni: Kwanini kijana Tajiri alimfuata Yesu? Kwanini hakukubaliana na ushauri wa Yesu, balada yake akaondoka kwa huzuni? Je kwanini ni rahisi Ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko Tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu? (Mk 10:25). Je kuna fundisho gani hapa kwetu sisi leo?

Ufupisho: Kijana Tajiri alikariri Amri za Mungu, lakini hakuishi kulingana na Neno la Mungu. Yesu anamualika kuja Kwake jinsi alivyo, lakini kwa kuzingatia mali alizo nazo, anaona ugumu. Yesu alijua kuwa mali hizo zingemzonga na kufifisha ukristo wake. Wapendwa, hakuna utajiri mkuu hapa duniani kama karama ya Roho Mtakatifu (ndani yetu). Hakuna tuzo kuu kuliko kuurithi Uzima wa Milele! Je, Bwana inapokuita, alfajiri ya leo, upo tayari kuacha vyote na kuja Kwake, au kama kijana huyu Tajiri, utaondoka kwa huzuni? BWANA akusaidie kufanya uchaguzi uliyo sahihi. Tafakari ya kina ya somo hili (pamoja na Mada zingine katika Marko 10) zitaletwa katika vipindi vijavyo, hapo baadaye.

Ahadi za Bwana: “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili Yangu, ataiona.” (Mathayo 16:24b-25)

Leo Katika Maombi: Ombea Mambo yafuatayo – 1. Maandalizi ya Masomo haya katika Injili ya Marko/ 2. Wongofu na Toba ya Kweli/ 3. Kutoa fedha, mali zetu kwa ajili ya masikini/ 4. Mwamko wa Kiroho katika siku hizi za Mwisho.

Sifa na Shukrani: 1. Mtoto tuliyemuombea juzi anaendelea vizuri/ 2. Zawadi ya uhai leo/ 3. Ahadi ya Uzima wa Milele.

Endelea kuomba kimoyo-moyo sasa tunapo “ANZA NA BWANA!” Kama una Wimbo fulani wa Injili, unaalikwa kuushirikisha hapa (kundini), ili tumsifu Yesu Kristo pamoja. Bwana Akubariki Sana.


Nawatakia Sabato Njema: “Kama ukigeuza mguu wako usihalifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu Wangu; ukiita Sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya BWANA yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika BWANA; Nami Nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha BWANA kimenena hayo.” (Isaya 58:13-14)

Comments
Print Friendly, PDF & Email