Mjane na Senti Mbili

June 6, 2021 in Alfajiri by TGVS

Ibada ya Afajiri/ Dhima: Mjane, Maskini na Senti Mbili/ Andiko Makini: Marko 12:41–44; Luka 21:1–4.


 

Fungu Kuu: “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” (Marko 12:41–44)

Maswali ya Moyoni: Yesu alijuaje kwamba mwanamke huyu alikuwa Mjane? Je, ukweli huu (maarifa ya kiungu) unathibitishaje kwamba Yesu ni Mungu? Kama mtu maskini, Mjane huyu alitakiwa kutoa senti moja tu. Kwa nini kutoa mbili? Yesu huona utoaji wa Mjane (41–42) kisha hupima sadaka ya Mjane (43–44). Je, Mungu anachunguza kile au jinsi tunavyomtolea leo? Je, utoaji wetu una maana yoyote kwa Mungu?

Kwa Kifupi: Katika sehemu hii ya Maandiko, tunaona mapendekezo ya Yesu kwa Mjane kujitolea kwa Mungu. Anawatazama baadhi ya matajiri wakiweka kiasi kikubwa cha fedha katika hazina ya Hekalu. Pia anaona sadaka ya Mjane. Analinganisha aina mbili za ujoaji: Sadaka ya Matajiri (waliyotoa kingi), huhesabika kama kitu kidogo. Sadaka ndo ya Mjane huhesabika kama kiasi kikubwa (aya ya 43). Yesu anasema Mjane maskini ametoa zaidi, kwa nini? –“Maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia” (aya ya 44).

Yesu alitumia Utoaji wa Mjane kama mfano kufundisha wanafunzi Wake thamani ambayo Mungu anaiweka kuhusu kujitolea kwa moyo wote. Kujitolea kwao kwa Yesu hivi karibuni kungejaribiwa vikali (Mk. 14:27–31). Tukio hili pia linaonesha kujitoa kabisa kwa Yesu katika kifo Chake. Mpendwa, Mungu alitoa kila kitu ili kukukomboa (Yn 3:16, Rum 8:32). Je utampatia nini? Je utatoa nini? Kumbuka, Mungu anatazama kila tendo la huduma linayotoka kwa dhati ndani ya moyo–  “Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.” (Waebrania 13:16) Moyo wako uko wapi?

Ahadi ya Leo: “Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema.” (2 Cor. 9:6–8)

Jambo la Kumshukuru Mungu: 1. Dunia ni ya Bwana, na mali yake yote (Zab. 24:1)/ 2. Fadhili Zake zadumu milele: ingawa tumekuwa si waaminifu katika miendendo na utoaji wetu, Bado anatupenda na kutubariki (Mal 3:10).

Masuala ya Kuombea: 1. Mwongozo wa Kujifunza Biblia katika Injili ya Marko/ 2. Uaminifu tunapompatia Mungu fedha zetu, wakati, rasilimali, talanta, n.k. / 3. Kujitolea kumtumikia Bwana kwa moyo mkunjufu (Rum 12: 1-2)/ 4. Uamsho na Matengenezo kwa waumini wote hapa.


 

Marafiki zangu wapendwa, karibu sasa katika ‘Wasaa wa Ibada ya Maombi!’ Jisikie huru kutushirikisha Wimbo wowote, au Mzigo wowote unaoweza kuwa nao, na Pamoja, tutamtafuta Bwana katika Maombi. Bwana atubariki sote, tunapo “ANZA NA BWANA!” Amina.

Comments
Print Friendly, PDF & Email