Ishara za Nyakati

June 7, 2021 in Alfajiri by TGVS

Ibada ya Alfajiri/ Dhima: Ishara za Nyakati/ Neno Muhimu: Kesheni.


 

Aya Kuu: “Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.” (Mk 13:37)

Maswali ya Moyoni: Vitabu vingapi katika Biblia vinahusika na Unabii wa Siku za Mwisho? Ni sura ngapi katika vitabu vya Injili vinazungumzia somo hili muhimu? Marko sura ya 13 inahusu nini hasa? Ni mwitikio gani unadhani sura hii ungepaswa kutuhamasisha kufanya?

Kwa Kifupi: Kuna Unabii mwingi katika Biblia. Vitabu vya Danieli na Ufunuo vinashugulika na Unabii wa siku za Mwisho. Katika vitabu vya Injili, kuna sura tatu zilizotengwa kwa ajili ya Unabii: Mathayo 24, Marko 13, na Luka 21. Yohana, yule mwanafunzi mpendwa, hana sura kama hiyo katika Injili ya Yohana; lakini ametenga kitabu kizima kushugulikia mada hii, kitabu hicho ni Ufunuo wa Yohana.

Marko 13 hujulikana zaidi kama “Mazungumzo ya Mizeituni.” Hapa, Yesu anaongea, wakati wanafunzi, husikiliza. Kwanza, anazungumzia juu ya uharibifu wa hekalu na matokeo yake (1-4); Mtiririko wa historia hadi Ujio wa Pili (5–13); Ishara ya Kuja Kwake na Mwisho wa Nyakati (14-37). Tutajifunza sura hii baadaye, lakini kwa sasa, nataka kusisitiza hoja moja ya msingi: Kila Ishara ambayo Kristo alizungumzia imeshatimia! Ishara pekee ambayo bado haijatimizwa ni hii – “Ishara ya Mwana wa Adamu” katika mawingu (Mt 24:30). Wapendwa, wakati Kristo atakapodhihirishwa mawinguni, kama hatukujianda, tutakuwa “tumechelewa sana!” Kwanini? Kwa sababu atakapokuja, “Ujira Wake u pamoja Naye” (Ufu. 22:12); Kwa lugha rahisi, itakuwa ni siku ya Malipo! Lakini sababu ya pili na ya kutisha zaidi ni hii: hakuna ajuaye “Siku wa Saa” (Mt 24:36). Unauliza— “Nifanye nini basi?” Kesha na Kuomba; Jiandae kukutana na Mungu wako, Ee Israeli (Amosi 4:12); Tubuni basi na kuamini Injili (Mk 1:15)… kwa maana ufalme wa Mbinguni u karibu! Je, utatii mwaliko wa Kristo tunapohitimisha ibada hii? – “Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo Bwana wa nyumba, kwamba ni Jioni, au kwamba ni Usiku wa manane, au Awikapo jimbi, au Asubuhi; asije akawasili ghafula akawakuta mmelala. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.” (Marko 13:35–37)

Ahadi ya Leo: Malaika walisema, “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.” (Matendo 1:11) Mtume Yohana anashuhudia akisema: “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina.” (Ufunuo 1:7)

Jambo la Kumshukuru Mungu Kwalo: 1. Wakati Adamu alipotenda dhambi, tulipoteza Edeni (paradiso); Lakini Adamu wa Pili (Yesu Kristo) aliposhinda dhambi na kifo, kwa Imani, Paradiso imerejeshwa tena, pia sasa tuna Uzima wa milele!/ 2. Yesu anatutayarishia maskani (Yn 14:1-3)/ 3. Yesu anarudi tena ili kutupeleka nyumbani (Isa. 25:9).

Masuala ya Kuombea: 1. Mwongozo wa Kujifunza Biblia katika Injili ya Marko/ 2. Wale ambao bado hawaja kata shauri kumfuta Yesu (Yoshua 24:14-15a)/ 3. Kesheni! Amka kutoka usingizini, “kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini.” (Rumi 13:11)


 

Rafiki zangu wapendwa, karibuni sasa katika ‘Wasaa wa Ibada ya Maombi! Jisikie huru kutushirikisha Wimbo wowote, au Mzigo wowote unaoweza kuwa nao; Pamoja, tutamtafuta Bwana katika Maombi. Bwana atubariki sote, tunapo  “ANZA NA BWANA!” Amina.

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email