Mwanzo 50: Usomaji wa Biblia

March 4, 2022 in Usomaji/ Vidokezo by TGVS

Mwanzo 50:

 


1 Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu.
Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli.
Siku zake arobaini zikaisha, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini.
Siku za kumlilia zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema,
Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi.
Farao akasema, Uende, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha.
Basi Yusufu akaenda amzike babaye, na watumwa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri.
Na nyumba yote ya Yusufu, na nduguze, na nyumba ya babaye; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo zao, na ng’ombe zao, katika nchi ya Gosheni.
Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana.
10 Wakaja mpaka sakafu ya Atadi, iliyo ng’ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya babaye siku saba.
11 Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng’ambo ya Yordani.
12 Wanawe wakamfanyia kama alivyo waagiza;
13 kwa kuwa wanawe wakamchukuwa mpaka nchi ya Kanaani, nao wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia.
14 Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliyokwenda pamoja naye kumzika babaye, baada ya kumzika babaye.
15 Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.
16 Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema,
17 Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.
18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako.
19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?
20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.
21 Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.
22 Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi.
23 Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu.
24 Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.
25 Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.
26 Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

 

 

MASWALI YA KUJADILI:


1. Je, ni sahihi kuiangukia maiti na kuibusu kutokana na kushikwa na uchungu wa kufiwa na upendo kwa marehemu? Je kubusu maiti na kuiaga ni kukubaliana na dhana potofu kuwa aliyekufa bado yu hai?

2. Je kuihifadhi maiti kwenye jeneza la thamani ni dalili ya upagani na matumizi mabaya ya raslimali? Je kuihifadhi maiti isioze inaendana na mafundisho ya dini.

3. Kwa nini watu humaliza msiba baada ya siku arobaini? Je kuliliwa sana msibani ni dalili kuwa ulipendwa na watu au ulipendwa na Mungu? Kitu gani kiliwafanya Wamisri wamlilie Israeli kwa siku sabini?

4. Je, kujiandalia maziko kwa kutayarisha kaburi lako na sanda ukiwa hai ni njia ya kuwapunguzia waliobaki mzigo wa gharama au ni uchuro na kujitabiria kufa?

5. Yakobo au Israeli alizikwa kwa heshima ya kitaifa mazishi yake yakihudhuriwa na wazee wote wa ikulu na wazee wote kutoka nchi ya Misri tofauti na pacha mwenzake Esau. Je hiyo inatokana na yeye Yakobo kumpa Mungu kipaumbele maishani mwake au ni upendeleo kutoka kwa mwanae Yusufu?

6. Je unauona uwezekano wa kuzuka mgogoro mkubwa Katika familia ya Yakobo kama Yusufu asingetumia hekima na busara kuumaliza? Je unauona umuhimu wa wazazi kumaliza migogoro ya watoto wao kabla hawajafa? Je unakubaliana na mbinu waliyotumia kaka zake Yusufu kuumaliza mgogorro huo?

7. Katika kila jambo baya analotendewa mcha Mungu kwa nia ovu Mungu huligeuza jambo hilo hilo kuleta matokeo mema kwa watu wengi. Unaiona hali hiyo katika kisa cha Yusufu? Je kisa cha Yusufu kimekuongezea ari ya kutokata tamaa unapotendewa mabaya na kutolipiza kisasi?

8. Yusufu bado anajitambua kuwa ni muumini wa tumaini lililowekwa na Mungu kwa wazazi tofauti na watu wengine ambao wakipata madaraka makubwa husahau mambo ya dini. Nini kilimsaidia Yusufu kubaki mwaminifu kwa Mungu wake licha ya kuwa na madaraka makubwa?

9. Yusufu aliagiza mifupa yake ibebwe wakati wana wa Israeli watakapokuwa wanaondoka Misri kuelekea Kaanani. Unadhani agizo hili lilikuwa na umuhimu wowote? Unadhani wana wa Israeli kwa kutii agizo hili (Kutoka 13:19; Yoshua 24:32) walionesha kumkubali Yusufu kama kiongozi wao wa kiroho?

10. Kubeba mifupa ya marehemu ili kwenda kuizika nyumbani kama walivyofanya Waisraeli inatofautianaje na inalinganaje na desturi ya kuhamisha msiba inayofanywa na baadhi ya makabila hapa nchini?

Comments
Print Friendly, PDF & Email