Yusufu Auzwa na Nduguze
February 19, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Mwanzo 37: Mwongozo wa Ibada/ 1-BSG-37A, (Mwanzo 37:1-43)/ Dhima: Yusufu Auzwa na Nduguze/ Wimbo: Burdens are lifted at Calvary (SDAH 476)
Uchunguzi: Mateso mara nyingi hutokana na Kutahawani (Kukiri) Injili – (Mat 24:9; Jn. 15:21; 2 Tim 3:11-12)
Tafakari: Sura hii inaanza sehemu ya kumi na ya mwisho ya “vizazi” vya kitabu cha Mwanzo. Ni “vizazi vya Yakobo” (Mwa. 37:2), lakini kisa hiki kwa sehemu kubwa kinamhusu Yusufu, mwana wa Yakobo, ambaye Raheli alimzaa. Yakobo alimtuma Yusufu akaone jinsi ndugu zake kumi wanavyoendelea walipokuwa wakichunga kondoo. Yusufu alimletea Yakobo taarifa mbaya kuhusu ndugu zake (v. 2). Yakobo alimpenda Yusufu kuliko watoto wake wengine, akamshonea joho (v. 3). Matokeo yake, ndugu zake “wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani” (v. 4). Chuki yao inaongezeka pale Yusufu anaposimulia ndoto yake ya kwanza (v. 5, 8). Chuki ya ndugu hao sasa inaongezeka na kuwa wivu (v. 11)—ambayo huanzisha hatua ya makabiliano makuu: Yusufu anatupwa shimoni ili afie humo (v. 24), kisha anauzwa kama mtumwa huko Misri kwa shekeli 20 za fedha (v. 28). Lo! Hiki ni kisa cha kusikitisha (kibinadamu). Nani anamtendea hivyo ndugu yake wa damu?
Maana ya Kiibada: Kisa cha Yusufu (Mwanzo 37–50) kinajulikana sana kwa sababu ya asili yake ya ajabu lakini iliyojaa maana madhubuti za kiteolojia. Nyuma ya kisa hiki ni mkono wa Mungu afanyaye maagano, ambaye daima hutimiza ahadi Zake (Mwa. 15:13-14). Mkono wa Mungu unaonekana wazi katika kila tukio—kuanzia unyama waliotenda kaka zake Yusufu, hadi matukio yaliyofanyika nyumbani kwa Potifa, hadi chumba cha gereza, hadi mwishowe kupandishwa cheo kabisa (Yusufu, waziri mkuu wa Misri). Hatimaye, Mungu anaiokoa familia ya Yakobo (dhidi ya njaa), wanahamia Misri (Gosheni), wanaokolewa salama kupitia Bahari ya Shamu, na kuanzia wakati huo na kuendelea, Mungu anaanzisha taifa lenye nguvu litakalokuwa baraka kwa ulimwengu wote! (Angalia Mwa. 12:1-3).
Pili, Yusufu ni mfano wa Kristo. Yusufu ni mojawapo ya mifano maridhawa zaidi inayomwakilisha Yesu Kristo, inayopatikana katika Agano la Kale. Tutachunguza haya tunapoendelea, lakini hebu tuitaje michache hapa – Kuzaliwa Kimuujiza: baada ya Raheli kuwa tasa kwa muda mrefu, Mungu akamfungua tumbo lake, naye akapata mimba ya Yusufu (Mwa. 30:22-23). Vilevile, kuzaa kwa bikra Mariamu kulitokana na uwezo wa Mungu (Mat. 1:18). Familia: Yusufu na Yesu walipendwa sana na baba zao (Mwa. 37:3-4; Mat 3:17). Chuki: Ndugu za Yusufu walimdharau, walimchukia, walijaribu kumuua, na wakamuuza utumwani. Watu wake Yesu walimkataa: “Alidharauliwa na kukataliwa na watu” (Isa 53:3), na Yuda akamuuza kwa vipande 30 vya fedha. Yusufu na Yesu walichukiwa kwa maneno waliyotamka mdomoni mwao (Mwa. 37:5-7, 11; Yn. 15:25). Nyumbani: Yusufu aliondoka nyumbani kwao kwa miaka 13 ili kutumika katika nchi nyingine. Yesu aliacha makao Yake ya utukufu mbinguni kwa miaka 33 ili kutumikia dunia hii inayoangamia: “Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi Yake iwe fidia ya wengi” (Marko 10:45).
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, unaweza kunidhamani kwa sababu Mimi natimiza ahadi Zangu daima (Hes. 23:19; 2 Kor. 1:20). Nilitimiza ahadi zote nilizompa Ibrahimu. Ingawa Yusufu hakuelewa kikamilifu kilichokuwa kikiendelea, aliendelea kuwa mtiifu kwa mapenzi Yangu. Kamwe sikuwahi kusema kwamba kunifuata siku zote itakuwa safari ya raha, kwa sababu “wote wapendao kuishi kwa utauwa katika Kristo Yesu watakabiliwa na mateso” (2 Tim. 3:12). Lakini naahidi kuwa pamoja nawe katika majaribu yako. Kamwe usikate tamaa, maana Mimi niko pamoja nawe!
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka kumtii Mungu kama Yusufu alivyomtii—nikimwachia Yeye matokeo yote.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.” (Yakobo 1:12)
Ibada Kupitia Uimbaji: Burdens are lifted at Calvary (SDAH 476)