Mauaji ya Kumwaga Damu huko Shekemu
February 16, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Mwanzo 34: Mwongozo wa Ibada/ 1-BSG-34A, (Mwanzo 34:1-31)/ Dhima: Mauaji ya Kumwaga Damu huko Shekemu/ Wimbo: Kumtegemea Mwokozi (NK 129)
Uchunguzi: Mausia dhidi ya Mijumuiko Miovu – (1 Kor. 5:9; 15:33; Zab. 1:1-2; Mit. 9:6; 2 Kor. 6:14, 17; Efe. 5:11; 2 Thes. 3:6, 14).
Tafakari: Hii ni mojawapo ya sura za giza kabisa katika historia ya Yakobo. Dina ni binti wa Yakobo na Lea. Yakobo ndipo tu ametoka kuhamia na kuishi Shekemu. Matukio kadhaa yanafanyika hapa: Unajisi (1–5). Dina alitoka kwenda kujumuika na marafiki zake mabinti wapagani. Matokeo yake, alibakwa na Shekemu, mwana wa mfalme. Posa (6–12): Hamori (babaye Shekemu) anakutana na Yakobo, akipendekeza ndoa kati ya Dina na Shekemu. Hila (13–24): Wakijifanya kukubaliana na pendekezo hili (lakini wakichukia moyoni), ndugu za Dina wanasisitiza kwamba Hamori na wanaume wa jamii yake lazima watahiriwe kwanza. Mauaji (25–29): Siku ya tatu, watu wa mji wakiwa hoi kwa sababu ya majeraha yao ya kutahiriwa, Simeoni na Lawi wanaingia kwenye kambi yao, na kuwachinja wote, na kuchukua mali zao—“mali yao yote; watoto wao wote wadogo na wake zao waliwachukua mateka!” (v.29). Karipio (30–31): Yakobo anawakemea wanawe kwa ajili ya matendo yao, akiogopa kwamba wengine wanaweza kulipiza kisasi. Lakini wana wa Yakobo walitetea kitendo chao, wakijibu, “Je, amtende dada yetu kama kahaba?”
Maana ya Kiibada: Matendo ya Shekemu kwa Dina ni ya kulaumiwa. Mara tatu katika kisa hiki, neno “unajisi” linatumiwa kuelezea tendo la uovu la Shekemu (Mwa. 34:5, 13, 27). Ingawa Shekemu kumbaka Dina haikuwa sahihi, Simeoni na Lawi waliitikia kupita kiasi na kutenda dhambi. Lakini Dina analaumiwa vilevile: kwanza alikuwa akifanya nini katika eneo hilo la uhasama? Kwa nini kuhawaana na wasiomcha Mungu? Je, unaona jinsi dhambi moja [kufanya maafikiano] inaweza kukua na kupelekea nyingine kutokea? Kwa sababu ya kutojali, alitambuliwa na mwana huyu mwovu, akamtamani, akamwingilia kwa nguvu kimapenzi. Matokeo yake, hilo lilisababisha kifo cha Shekemu na watu wote wa jamii yake! Tazama kwamba matokeo ya mauaji haya yalisababisha familia nzima ya Yakobo kukusanya vitu vyao vyote, kuondoka eneo hilo, na kuhamia Betheli na Hebroni (35:1) — mbali na hatari ya mapatilizo na kulipiza kisasi.
Pili, sura hii haitaji jina la Mungu au kulidokezea. Wapendwa, tunapokosa kumtii Mungu, tunajiweka sisi wenyewe na wapendwa wetu katika hatari. Fikiria matokeo ya kutotii kwa Adamu (Mwa. 3:17-19), Kaini (Mwa. 4:10-12), ulimwengu kabla ya gharika (Mwa. 6-7), Ibrahimu akiwa Misri (12:10–20) na Gerari (Mwa. 20:1), Lutu katika Sodoma (Mwa. 19:12-13), Isaka huko Gerari (Mwa. 26:6–16), Samsoni katika Ufilisti (Yuda 14; 16), Petro katika baraza la kuhani mkuu (Luka 22:54-62), nk.
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, daima kuna hatari kubwa katika uzembe wa kuchangamana na uovu. Ili kuwalinda watu Wangu, niliwaamuru wasichangamane na wasiomcha Mungu (Kut. 23:2; Kumb. 7:2-4; Law. 18:3; 20:23; Hes. 16:26); kwa njia hiyo, wangeweza kuepuka vishawishi, kufanya mapatano, na dhambi. Ikiwa Dina angetii maonyo haya, ikiwa Yakobo angebaki mwaminifu kwa wito wake (udhibiti na usimamizi wa mzazi), mauaji haya ya umwagaji damu yangeweza kuepukwa. Je, utatii maonyo Yangu ili uweze kubarikiwa? (2 Kor. 6:17)
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka –[1] kuungama na kutubu dhambi zangu; [2] kubaki mwaminifu kwa masadikisho yangu; [3] kujitenga na waabudu sanamu na tabia zao mbaya; [4] kujiepusha na dhambi zilizoorodheshwa katika sura hii: kuhawaana na wasiomcha Mungu, tamaa, uzinzi (ubakaji), udanganyifu, kupanga njama za kumdhuru mwingine, kupanga uovu, vurugu, na kisasi.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria Yake huitafakari mchana na usiku.” (Zaburi 1:1–2)
Ibada Kupitia Uimbaji: “Kumtegemea Mwokozi” (NK 129).
1. Kumtegemea Mwokozi, kwangu tamu kabisa;
Kukubali neno lake nina raha moyoni.
Yesu, Yesu namwamini, nimemwona thabiti;
Yesu, Yesu yu thamani, ahadi zake kweli.
2. Kumtegemea Mwokozi, kwangu tamu kabisa
Kuamini damu yake nimeoshwa kamili.
3. Kumtegemea Mwokozi, kwangu tamu kabisa;
Kwake daima napata, uzima na amani.
4. Nafurahi kwa sababu nimekutegema;
Yesu, M-pendwa, Rafiki, uwe nami dawamu.