Ibada ya Sanamu
February 17, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Mwanzo 35: Mwongozo wa Ibada/ 1-BSG-35A, (Mwanzo 35:1-4)/ Dhima: Ibada ya Sanamu/ Wimbo: Near to the heart of God (SDAH 495).
Uchunguzi: Ondoeni Sanamu Zenu – (2 Falm 3:2; 2 Nya. 15:8; 1 Sam 7:3; Mwa. 35:2; Yos. 24:14; 1 Falm 15:12; 2 Falm 23:24)
Tafakari: Sura hii ina dhima nyingi, lakini tutazingatia masuala ya ibada (“sanamu”). Kwenye msingi wa hofu ya Yakobo ya kulipiza kisasi kwa Wahivi (rejea somo la jana, Mwa. 34:25-29, 30), Mungu anamwagiza aondoke Shekemu ahamie Betheli. Madhumuni ya kuhama yalikuwa mawili: makao (Yakobo alipaswa kusimika hema lake “na kuishi humo”); ibada (alipaswa “kumfanyia Mungu madhabahu huko” (v. 1). Neno “Betheli” linamaanisha “nyumba ya Mungu.” Lakini kabla Yakobo hajahamia Betheli, alihitaji kujitayarisha kwa ajili ya safari hiyo. Katika fasili ya 2 & 4, tunajulishwa aina ya matayarisho aliyopaswa kufanya: “Kwa hiyo Yakobo akawaambia watu wote wa nyumba yake, “Ondoeni sanamu zenu za kipagani, jitakaseni, na kuvaa mavazi safi.” (Mwanzo 35:2) Labda unauliza: “Jinsi gani sanamu hizi za kipagani zilipata nafasi ya kupenya katika hii familia ya Kikristo, katika nyumba ya Yakobo? Kumbuka Raheli alikuwa ameiba baadhi ya sanamu kutoka kwenye nyumba ya baba yake (Mwa. 31:19), na inaonekana bado alikuwa nazo. Pia, mateka, waliochukuliwa kutoka mji wa Shekemu, pengine walileta sanamu zao.
Maana ya Kiibada: Ibada ya sanamu haipatani na huduma ya Mungu. Yakobo na familia yake waliishi miongoni mwa wapagani walioabudu miungu, na sanamu zilikuwa zimeingia katika familia yake. Lakini sasa, lazima aitakase familia yake kwanza kabla ya Mungu aliye hai kuikubali ibada yake. Hivyo, Yakobo aliwahimiza wanafamilia yake watupilie mbali sanamu zote, nao wakafanya hivyo. Mpendwa, ni aina gani za sanamu iliyomo maishani mwako leo? Unajua, sanamu ni zaidi ya kuabudu vielelezo na miungu ya uwongo (Kut. 20:3-5). Ni suala la moyoni linalofungamana na kiburi, ubinafsi, uchoyo, ulafi (Php 3:19), na kupenda mali (Mat 6:24). Ibada ya sanamu huanzia moyoni: shauku, matamanio, kufurahia, kuridhika na chochote unachokithamini zaidi kuliko Mungu. Mtume Paulo anaita hii tamaa!
Sanamu ndizo zinakuteketeza badala ya wewe kuteketezwa na Mungu. Sanamu inaweza kuwa chochote kinachochukua nafasi ya Mungu. Mpendwa, Mungu asipokuwa katikati, lengo, na kipaumbele maishani mwako, hilo ni tatizo kubwa. Sanamu za leo zinaweza kuwa mali, ufahari, na mamlaka; elimu, kazi, kutafuta pesa kwa gharama yoyote ile, michezo/video, uzinzi— (tamaa, mapenzi, ujuhuba, kulisha akili yako vianzi vya ponografia, huku ukimwacha mke wa ujana wako, Mit. 5:18), mahusiano (maisha ya faragha), shughuli zisizo halali, nk. Na orodha hii inaendelea na kuendelea!
Mpendwa, hivi kuna sanamu za kutowesha maishani mwako? Roho Mtakatifu anapokusadikisha juu ya dhambi hizi (Yn. 16:6) anapozungumza nawe kuhusu kuondoa sanamu hizi, hivi, unasikiliza? Je, unakumbuka siku hizo ulipokuwa “karibu na moyo wa Mungu”? – (sala, ibada, Kuichunguza Biblia, kushuhudia). Kwa nini uliacha? Nini kilitokea? Nini kilijaza ombwe hilo? Neno moja: Ibada ya sanamu. Mwombe BWANA akusaidie ili umkabidhi maisha yako kabisa (Mat 5:6). Tubuni na kuongoka (Matendo 3:19). Amina.
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, nataka kukubariki, lakini kuna Dhambi maishani mwako—kuabudu sanamu (Isa. 59:1-2). Nachukia chochote kinachochukua usabihi wako kutoka Kwangu. Nachukia ibada ya sanamu kwa sababu nimekuumba: wewe ni Wangu. Unapoviabudu vitu vingine badala Yangu, unasema kwamba Mimi si muhimu kabisa. Mimi ni “Mungu mwenye wivu” na “Sitampa mwingine utukufu Wangu, wala sitazipa sanamu sifa Zangu.” (Isa. 42:8) Katika siku hii, nakualika unitambue Mimi kama mlengwa halisi wa ibada (Ufu. 14:6-7). Kumbuka kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wako. Tubu, na kuniabudu kwa moyo wako wote (Mt 4:10; Lk 10:27) Je utafanya hivyo?
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka – [1] Kuondoa sanamu zote maishani mwangu, kujitakasa nafsi yangu, na kuvaa mavazi safi (Mwa. 35:2); [2] Nimwombe Kristo anivike vazi la haki Yake na kunitumia kama chombo kitakatifu katika ufalme Wake; [3] Niwasaidie wengine watambue sanamu katika maisha yao, watubu na kuokolewa.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu.” (Wakolosai 3:5–6)
Ibada Kupitia Uimbaji:
KARIBU NA MOYO WA MUNGU! (SDAH 495).
1
Kuna mahali pa pumziko tulivu,
Karibu na moyo wa Mungu;
Mahali ambapo dhambi haiwezi kudhuru,
Karibu na moyo wa Mungu.
Kiitikio
Ee Yesu, Mkombozi Mbarikiwa,
Aliyetumwa kutoka moyoni mwa Mungu,
Tushikilie sisi tungojao mbele Yako
Karibu na moyo wa Mungu.
2
Kuna mahali pa faraja tamu,
Karibu na moyo wa Mungu;
Mahali tunapokutana sisi na Mwokozi wetu,
Karibu na moyo wa Mungu.
3
Kuna mahali pa uhuru kamili,
Karibu na moyo wa Mungu;
Mahali ambapo yote ni furaha na amani,
Karibu na moyo wa Mungu.