Nasaba ya Esau
February 18, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Mwanzo 36: Mwongozo wa Ibada/ 1-BSG-36A, (Mwanzo 36:1-43)/ Dhima: Nasaba ya Esau/ Wimbo: Have Thine own way, Lord! (SDAH 567)
Uchunguzi: Esau, Edomu, Seiri, Waedomu— (soma Mwa. 25:23; 27:29, 37–40; Mwa. 32:3; 36:31–39; Kut. 15:15; Hes. 20:14; Kumb. 2:4, 5, 12; 1 Nya. 1:43–50; Eze. 32:29; Amosi 2:1; 1 Nya. 1:51–54).
Tafakari: Kuna migawanyiko kumi ya “nasaba” katika kitabu cha Mwanzo – Uumbaji (2:4), Adamu (5:1), Nuhu (6:9), Wana wa Nuhu (10:1), Shemu (11:10), Tera (11:27), Ishmaeli (25:12), Isaka (25:19), Esau (36:1, 9), na Yakobo (37:2). Sura hii inatumika kama hitimisho la sehemu ya Esau katika kitabu cha Mwanzo. Inafuatilia kuhama kwake hadi nchi ya Edomu, uzao wake wa karibu, na muundo wa ukoo unaotokana na uzao wake. Ni utimizo wa ahadi ya Mungu kwa Rebeka wakati mapacha hao walipozaliwa: “[Waanzilishi wa] mataifa mawili wamo tumboni mwako, na utengano wa makabila mawili umeanza katika tumbo lako; taifa moja litakuwa na nguvu zaidi kuliko lingine, na mkubwa atamtumikia mdogo.” (Mwanzo 25:23, AMP) Katika sura inayofuata, tunaanza sasa kutazama kwa mapana nasaba ya Yakobo pamoja na mgawanyiko wake katika makabila kumi na mbili ya Israeli. Kumbuka kwamba kadiri ambavyo walimtii BWANA, Israeli ikawa taifa lenye nguvu. Fikiria hadhi ya taifa hili wakati wa utawala wa Mfalme Daudi, kwa mfano (lakini hilo ni somo tofauti).
Maana ya Kiibada: Mpendwa, Mungu ni mwaminifu kwa kutimiza ahadi Zake. Sura hii inaonesha jinsi gani ahadi za Mungu kuhusu Esau zilitimizwa. Waedomu walikuja kustakimu huko Seiri— (nchi yenye milima mikali, kusini mwa nchi ya ahadi). Esau aliahidiwa fanaka kubwa ya muda kitambo na kwamba angekuwa mwanzilishi wa taifa kubwa (Mwa. 25:23; 27:39, 40) Na hivyo ndivyo ilivyotokia: Edomu (Seiri) ilijawa wazao wa Esau na Wahori wenyeji, mababu wa mataifa ya Kiarabu (Mwa. 27:39–40; 36:1–20).
“Kusudi la sura hii ya nasaba ni kufuatilia maskani ya Esau katika nchi ya Edomu, urithi wake wa halahali na uzao wake unaokaa katika nchi ya Seiri. Bila shaka, Waedomu wanakuwa maadui wakatili mno kwa Israeli. Kwa kweli, wakati wa kutangatanga jangwani wakati Musa alipoandika nasaba hizi, Edomu ndiye ‘aliyekataa kuwapa Israeli ruhusa wapite katika himaya yake; kwa hiyo Israeli wakamwacha’ (Hes. 20:21). Hivyo, mwandishi anaorodhesha uzao wa Esau kwa ajili ya jambo muhimu: mjue adui yako!
Nasaba hiyo pia inatumika kudhihirisha kwamba uzao wa nyoka, watu wasio wa agano, wako hai na wenye hali njema kwenye sayari ya dunia. Wanazaliana na kuongezeka. Na swali tunalobaki nalo sasa ni: Jinsi gani Mungu atawatunza wateule Wake? Atatimizaje ahadi Zake kwa ule uzao wa mwanamke? – [John D. Currid, A Study Commentary on Genesis: Genesis 25:19–50:26, EP Study Commentary, (Darlington, England; Carlisle, PA: Evangelical Press, 2003), 2:183].
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, hata kabla ya Esau kuzaliwa, nilitabiri kwamba Esau angetokeza taifa kubwa (Mwa. 25:23). Sura hii inatimiza unabii huo: kutoka kwa Esau liliinuka taifa kubwa na lenye nguvu la watu, Waedomu. Lakini Yakobo akageuka kuwa mkuu zaidi kuliko Esau: kutoka kwa ukoo wa Yakobo, ahadi ya Mwanzo 3:15 ilitimia, na Masihi akazaliwa “wakati ulioteuliwa” (Angalia Mat 1:1-2; Gal 4:4). Jambo muhimu ni hili: Kabla hujazaliwa, nilijua yote kukuhusu! (Yer. 1:5; Zab. 139:16; Isa. 44:2, 24; 49:1, 5). Najua una uwezo gani; unachohitaji ili kufanikiwa. Najua yote kuhusu vikwazo unavyokumbana navyo, maadui ulio nao. Natamani unigeukie Mimi kwa ajili ya kupata mwongozo, maelekezo na msaada. Katika siku hii, Je utanitumaini Mimi kwa kunikabidhi maisha yako? Je, utatii amri Zangu ili ubarikiwe?
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka kumtumaini Mungu ili ashughulikie mielekeo yote ya maisha yangu. Nataka kuyasalimisha maisha yangu Kwake na kujikabidhi Kwake kikamilifu.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Maana najua mipango na mawazo niliyonayo kwa ajili yenu, asema BWANA: mawazo na mipango kwa ajili ya ustawi mwema na amani, wala si ya uovu, kuwapatieni tumaini katika mustakabali wenu wa mwisho.” (Yeremia 29:11, AMP)
Ibada Kupitia Uimbaji: Nataka Nimjue Yesu (NK 54)
[1] Nataka nimjue Yesu, na nizidi kumfahamu; Nijue pendo lake tu, wokovu wake kamili.
Kibwagizo: “Zaidi, zaidi, nimfahamu Yesu; Nijue upendo wake, wokovu wake kamili.”
[2] Nataka nione Yesu, na nizidi kusikia; Anenapo kitabuni, kujidhihirisha kwangu.
[3] Nataka tena zaidi, daima kupambanua; Mapenzi yake, nifanye yale yanayompendeza.
[4] Nataka nikae naye, kwa mazungumzo matamu; Nizidi kuwaonyesha wengine wokovu wake.