Uovu wa Mwanadamu & Hukumu ya Mungu
February 5, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Mwanzo 6: Mwongozo wa Ibada/1-BSG-6A (Mwanzo 6:1-8)/Dhima: Uovu wa Mwanadamu & Hukumu ya Mungu/ Wimbo: Umechoka Je Umesumbuka (NK 124)
Uchunguzi: Safina ya Nuhu & Umuhimu Wake– (Mwa. 6:8, 14-22; Mwa. 7:1, 7, 23; 8:1, 18; Mat 24:37-39; Luka 17:26-30; Ebr. 11:7; 2 Pet 2:4-5).
Tafakari: Hebu tupitie yale ambayo tumejifunza hadi sasa. Mwanzo 1, Uumbaji; Mwanzo 2, maisha makamilifu katika Edeni; Mwanzo 3, dhambi na athari za dhambi—mauti; Mwanzo 4, Kaini na Habili. Mwanzo 5 ulistamakani kighahilifu kwa wana waliozaliwa kabla ya gharika, nasaba ya kiungu kutoka kwa Adamu hadi Nuhu. Katika Mwanzo 6, tunatambulishwa kwa mabinti waliozaliwa na watu hawa —(uharibifu wa uzao wa kiungu—wakichangamana na uzao usiomcha Mungu). Dhima kuu tatu zinajitokeza katika sura hii: dhambi, hukumu, na habari njema ya wokovu kupitia Safina.
Kadiri wakati ulivyopita, uzao wa kiungu ulimpuuza Mungu, wakawa watu wakilimwengu na wapotovu. Maandiko yanasema kwamba “wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua!” (Mwa. 6:2). Wacha-Mungu walilisha akili zao ngono. Walimpuuza kabisa na kumwasi Mungu. Hivyo, Mungu alifadhaika. Kwa hakika, alimhuzunikia mwanadamu; alijuta kumuumba mwanadamu. Kwa hiyo, alitoa onyo—kwamba neema Yake ilikuwa na mipaka, Hukumu Yake ilikuwa inakuja, na kwamba angemwondoa Roho Wake. Lakini katika aya ya 8, tunaona rehema ya Mungu: Alimkumbuka Nuhu, mtumishi Wake, Naye akazindua mfumo ambao kwao watu wa Ulimwengu wangeokolewa, yaani Safina.
Maana ya Kiibada: Safina ya Nuhu inawapa Wakristo mdokezo wa Ujio wa Pili– yaani, kutokea kwa Yesu Kristo, mara ya pili (Ebr. 9:28) ili kuwahukumu watu wa Ulimwengu huu. Tafadhali kumbuka kwamba atakapokuja, ujira Wake utakuwa pamoja Naye (Ufu. 1:7; 22:12-14). “Daima Mungu amewapa wanadamu onyo la hukumu zinazokuja. Wale waliokuwa na imani katika ujumbe Wake kwa wakati wao, na kutimiza imani yao, kwa kutii amri Zake, waliepuka hukumu zilizowapiga wasiotii na wasioamini.” (The Desire of Ages, uk. 634). Vilevile, Mungu ametoa onyo kwamba Ulimwengu huu unakaribia mwisho (2 Pet 3:3-7, 10; Tit 1:13; Ufu. 21:1-4), kwamba lazima watu watubu, wapatane na Mungu, na kuokolewa. Lakini ni wangapi wanaotii maonyo haya? “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.” (Luka 17:26–27)
Dondoo ya Mwisho: Ni nini kilichohifadhi uhai wa Nuhu kupitia tufani hiyo? Ilikuwa ni Safina? Hapana. Safina ingeweza kuharibiwa kirahisi (kumbuka, hii ilikuwa kabla ya uhandisi wa karne ya 21). Nuhu aliokolewa “kwa neema kupitia imani” (Mwa. 6:8; Efe. 2:8-9). Kristo ndiye aliyeilinda salama safina hiyo katikati ya mawimbi yenye kunguruma na kufurukuta; kwa sababu Nuhu alikuwa na imani katika uwezo wa Mungu wa kumhifadhi yeye na familia yake katika dhoruba hiyo. Si kwamba Nuhu hakuwa mdhambi, la Hasha. Alikuwa mdhambi, lakini alitubu, akasamehewa, akawa mwaminifu, na Mungu akamwokoa. Mpendwa, Mungu anashauku ya kukuokoa siku hii ya leo lakini, hivi umeweka imani yako Kwake? Je unaamini kuwa anao uwezo wa kukuokoa?
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, niliuangamiza Ulimwengu kabla ya gharika kwa sababu ya dhambi kuenea. Yesu anakuja hivi karibuni, na Ulimwengu huu utaangamizwa. Lakini nataka kukuokoa. Sitaki kukuona ukiangamia katika mafuriko ya ghadhabu Yangu (Rum. 1:18; Ufu. 14:10). Ndiyo maana nakualika asubuhi ya leo utubu dhambi zako; kabidhi maisha yako kwa Yesu: mruhusu awe Bwana na Mwokozi, kisha jiandae kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Je ungependa kufanya hivyo?
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka – 1. kuhacha dhambi na kila aina ya uovu (Mwa. 6:1-2); 2. Kuepuka kumhuzunisha BWANA kwa kuendelea katika njia ya uovu (Mwa. 6:5-6); 3. Kumuomba BWANA aniokoe dhidi ya maangamizi yanayokuja (Mwa. 6:7); 4. Kuweka bidii ya kuwa mtu mwadilifu, mkamilifu kama alivyokuwa Nuhu; (Mwa. 6:8); 5. Kumtii Mungu na kufanya “sawasawa na yote ambayo ameniamuru” katika neno lake (Mwa. 6:22); 6. Kujitayarishe kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu… Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.” (Mathayo 24:42, 44)
Ibada Katika Uimbaji: Umechoka Je Umesumbuka (NK 124)
(Are You Weary?)
1. Umechoka, Je, Umesumbuka?
Mwambie Yesu Sumbuko Lako;
Unayalilia Yapitayo? Mwambie Yesu Pekee.
Mwambie Yesu Sumbuko Lako, Yu Rafiki Amini,
Hakuna Rafiki Kama Yeye, Mwambie Yesu Pekee.
2. Je, Machozi Yakulengalenga?
Mwambie Yesu Sumbuko Lako;
Walemewa Na Dhambi Rohoni? Mwambie Yesu Pekee.
3. Waogopa Shida Na Majonzi?
Mwambie Yesu Sumbuko Lako;
Wasumbukia Mambo Yajayo? Mwambie Yesu Pekee.
4. Kuanzia Kifo Kukutisha?
Mwambie Yesu Sumbuko Lako;
Watamania Ufalme Wake? Mwambie Yesu Pekee.