Alifanya Nyota Pia

February 5, 2022 in Mwongozo wa Maombi by TGVS

Mwanzo 1: Mwongozo wa Maombi/ 1-BSG-1B (Mwanzo 1:1-31)/ Dhima: Alifanya Nyota Pia/ Wimbo: Vito vya thamani kubwa (NK 196)


Andiko Msingi: “Yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; Yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina Lake.” (Amosi 5:8)

Maelezo ya Ufunguzi: Ukweli wa kushangaza sana kwangu katika Mwanzo sura ya kwanza, ni kirai hiki kidogo kinachopatikana katika fasili ya 16, ‘Alifanya nyota pia’. Kana kwamba huu ni mstari wa kupotezea kwenye Biblia. Inashangaza ikizingatiwa idadi na mtandamano wa galaksi na nyota. Lakini ukweli mmoja madhubuti unasalia: Mungu aliumba, “Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.” (Zaburi 33:9). Mungu anapozungumza, vitu hutokea.

Fikiria hili: kuna nyota takriban bilioni 200 (au pengine zaidi) katika galaksi ya Milky Way pekee idadi ina uwezekano wa kuongezeka kadiri teknolojia ya darubini inavyozidi kuboreshwa. Kwa haya yote Biblia inasema, “(Mungu) alifanya nyota pia!” Na jambo la kushangaza zaidi, Mungu anazijua zote kwa majina. Mungu wa kustaajabisha ilioje!

 Wapendwa, kama Mungu anaweza kuamuru mabilioni ya nyota yawepo ndani ya sehemu ya sekunde (nazo zikasimama kikamilifu kwenye obiti zao, miaka takriban 6,000 baadaye), ni mengine mangapi anayoweza kufanya kwa ajili yako? Je unamwamini Mungu Muumbaji? Je unaamini kwamba anao uwezo wa kukuumba upya (Kol 3:10) na kukupatia “mianzo mipya” licha ya hali unayopitia sasa? Tunapokuja katika Kipindi cha Maombi leo, tunaalikwa kumwamini Mungu, kutubu dhambi zetu (1 Yn. 1:9), na kuwa na staamani kwamba “Yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Phil. 1:6). Amina?

Maadili ya Kukuza: Imani katika Mungu; Shukrani; Kumheshimu Mungu; Kuyaheshimu mazingira; Kuheshimu familia.

Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Kushindwa kumkiri Mwenyezi Mungu kama Muumbaji na Mtegemezaji wa Ulimwengu.

Jambo Fulani la Kumshukuru Mungu: Uumbaji wa Mbingu na Nchi; Kuumbwa katika sura na mfanano wa Mungu; Nchi na tunu ya kiungu; Karama ya Uhai (wanadamu); Tunu ya Uzima (wanyama na mimea); Uwezo wa mwanadamu wa kufikiri na kuiga tabia ya Mungu.

Watu wa Kuombewa: Wanadamu wote –(hususan wale waliomo kwenye duara lako) –waige tabia ya Mungu tangu sasa na kuendelea, maana aliwaumbwa katika sura Yake (Mwa. 1:26, 27).

Masuala ya Kuombea: Ndoa (Waume & Wake); Kudra za Mungu; Utakatifu; Sabato na Pumziko; Uwakili; Umilele pamoja na Mungu; Usuhuba pamoja na Mungu.

Ahadi ya Leo: “Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.” (2 Wakorintho 3:18)


 

OMBI LA KUHITIMISHA.

Ombi la Kuhitimisha/ Mwanzo 1 (1-BSG-1Z)/ Je kuna hitaji lolote ninaloweza kuomba/kuwasilisha katika sura hii? Ndiyo.

Sala: “Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo Yako ni ya ajabu, Na nafsi yangu yajua sana.” (Zaburi 139:14)

Baba, tunakushukuru tena kwa ajili ya neno Lako katika Mwanzo, sura ya kwanza. Tunakushukuru kwa ajili ya tunu ya uhai, kwa ajili ya fursa nyingine ya stahimani ya Uumbaji—kwamba Wewe pekee ndiye uwezaye kuumba. Kwamba hatukuibuka (kama ambavyo baadhi hufundisha kimakosa), lakini tulitoka kwenye mikono Yako, na kwamba ulituumba kulingana na sura Yako, kulingana na mfanano Wako (Mwa. 1:27).

Tusaidie tujue kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu Wake; Tu watu Wake, na kondoo wa malisho Yake.” (Zaburi 100:3). Tusaidie ili tutangaze matendo Yako makuu kwa mataifa, katika njia zozote ziwezekanazo, hadharani na faraghani, kwamba Elohimu ndiye Muumbaji (mwasisi, mwandisi, na msanifu mkuu) wa “mbingu na nchi” (Mwa. 1:1).

Tusaidie ili tuyatangazie mataifa kwamba Yehova ni mwenye upendo, Mungu wa kweli, ambaye anastahili kuabudiwa. Tusaidie kukiri: “Lakini sasa, Ee Bwana, Wewe u Baba yetu; sisi tu udongo, Nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono Yako.” (Isaya 64:8). Tunakushukuru kwa kutuumba katika sura Yako kwa ajili ya utukufu Wako.

Baba, tumetenda dhambi, na kila mmoja wetu amekukosea kwa namna fulani. Tusamehe BWANA. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso Wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.” (Zaburi 51:10–11) Baba, hebu Roho Wako atusaidie “tuuvae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.” (Efe. 4:24)

Tunakushukuru kwa ajili ya baraka za kila siku; kwa ajili ya tunu na ahadi za tunu. Hebu tusaidie tukidhi mahitaji yetu ya kila siku—kimwili na kiroho. Mruhusu Roho Wako atufundishe jinsi ya kutii mapenzi Yako, amri Zako, na maagizo Yako.

Bwana Yesu, “tukumbuke utakapokuja katika ufalme Wako!” (Luka 23:42; Yn. 14:1-3); wakati ule kila kitu kitakaposahihishwa tena (Ufu. 21:4); wakati ule utakapowapeleka watakatifu nyumbani. Ni siku kuu ilioje itakuwa! Kwa hiyo, Bwana mpendwa, tutakase katika kweli Yako kila siku, na kutuandaa kwa ajili ya ufalme Wako wa utukufu. Tunakushukuru, Baba, nasi tunakuja katika jina la Yesu Kristo, Amina.

 

Comments