Ibada (Torati 24)
April 6, 2019 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
MWONGOZO WA IBADA.
(“Mwongozo wa Ibada” unaoshabihiana na programu ya “Usomaji wa Biblia” kila siku)
April 7, 2019
Mwongozo wa Biblia
5-BSG-24A.1 (Torati 24)
NJONI, TUABUDU, TUSUJUDU, TUPIGE MAGOTI MBELE ZA BWANA.
Aya ya Mwitikio: Torati 24:5-18
Wimbo wa Ufunguzi: “Nataka nimjue Yesu.”
AHADI ZA MUNGU KWA AJILI YAKO.
Dhima: [Mungu, mtetezi wa Yatima]
“Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani; bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.” (Torati 24:17-18)
JAMBO LA KUMSHUKURU MUNGU.
Mungu ni mwenye Haki: Atatetea maslahi ya wanyonge, maskini, yatima, wajane, wageni, na watumwa.
(a) Wanyonge: “Kwa ajili ya kuonewa kwao wanyonge, Kwa ajili ya kuugua kwao wahitaji, Sasa nitasimama, asema Bwana, Nitamweka salama yeye wanayemfyonya.” (Zaburi 12:5)
(b) Maskini: “Usimnyang’anye maskini, kwa kuwa ni maskini; Wala usimdhulumu mtu mnyonge langoni; Kwa sababu Bwana atawatetea; Naye atawateka uhai wao waliowateka.” (Mithali 22:22-23)
(c) Yatima, na Wajane: “Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima.” (Kutoka 22:22)
(d) Wageni: “Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.” (Kutoka 22:21)
(e) Watumwa: “Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi.” (Walawi 19:13) Linganisha (Torati 24:14-15)
WAJIBU/ UNGAMO/ USHUHUDA WOWOTE?
(a) Tubu dhambi ya kuonea wanyonge, maskini, yatima, wajane, wageni, na watumwa.
(b) Ikumbukwe kwamba nasi tulikuwa “watumwa katika nchi ya Misri;” utumwa wa dhambi; Lakini Bwana akatukomboa. (aya ya 18, 22)
(c) Talaka si mpango wa Mungu. Mungu anachukia Talaka: “Maana Mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli.” (Malaki 2:16a). Anasihi sana wanandoa wasuluhishe tofauti zao, na wasameheane. “Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” (Marko 10:9)
DHAMBI ZA KUEPUKA/KUUNGAMA.
Dhambi (Dhambi Mahususi) → (Torati 24)
(a) Talaka (aya ya 1-4)
(b) Kumgeuza nduguyo “mtumwa, au kumwuza” (7)
(c) Ukoma: Kutofuata mafundisho ya “makuhani Walawi” (8-9)
(d) Mkopo: Usitwae rehani kwake uliyemkopa (10-13)
(e) Dhuluma: “Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji.” (14)
(f) Mshahara: “Mpe ujira wake kwa siku yake, wala jua lisichwe juu yake.” (15)
(g) Haki katika adhabu ya kifo: “Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.” (16)
Je unayo mambo yoyote ya kuombea? Yaandike hapa chini ~ (Angalia “Fomu ya Maombi”), au kwenye Blogu ya “Sauti ya Injili,” na mtu fulani atayaombea. Mlilie Bwana akusamehe dhambi hizi, kisha mwombee mtu fulani awe mshindi katika maeneo haya yaliyotajwa.
KUJIWEKA WAKFU:
Kwa neema ya Bwana, Leo ninaahidi kufanya yafuatayo:
(a) Kumpenda mke wangu; na kuachana kabisa na mawajo ya “kumtaliki.”
(b) Kuungama na kuachana na dhambi zilizotajwa hapo juu.
(c) Kutetea maslahi ya wanyonge, maskini, yatima, wajane, wageni, na watumwa.
SALA: Ee Bwana, nisaidie kuakisi tabia Yako, ili niweze kutetea maslahi ya wanyonge, maskini, yatima, wajane, wageni, na watumwa. Nikumbushe kuwa na mimi nilikuwa “mtumwa;” Lakini ukanihurumia, , ukanirehemu, ukaniponya, ukaniweka huru. Nisaidie siku hii ya leo nisije nikakutenda dhambi. Nimeomba haya katika jina la Yesu Kristo, Bwana wetu, Amina.
UWE NA SIKU YENYE BARAKA! “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu.” (Maombolezo 3:22–23)
Sauti Ya Injili SDA © 2019