Isaya 51: Mwongozo wa Ibada

October 10, 2020 in Mwongozo wa Ibada by TGVS

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Isaya 51/ Dhima: Wokovu wa zamani wa Mungu unahimiza Imani kwa siku zijazo/ 23-BSG-51A, (Isaya 51: 1-8)/ Wimbo: Mwamba wenye Imara, Kwako nitajificha! (NK 192)


 

UCHUNGUZI: Fikiria kile ambacho Mungu amefanya katika siku za nyuma – (Kumb. 5:15; 8:2; 9:7–8; 11:2–7; 15:5; 24:9; 24:18; Zab. 77:7–13–20; 105:5, 8–45; 143:5; Isa 46:8–10; 51:1–3; Isa 64:5). Kumbuka jinsi Mungu alivyokuokoa/ alivyokukomboa (Kum. 7:18-19, 20–24; 32:7–14, 5–6, 15–35; Efeso 2:11–13).

TAFAKARI: Isaya 51: 1-52:12 inaweza kuitwa “wito wa Mungu na faraja kwa watafuta Haki.” Maagizo yanayotolewa katika sehemu hii ya Maandiko yanaweza kufupishwa kama ifuatavyo: “Nisikilizeni” (Isa. 51:1, 4, 7); “Amka, Amka” (Isa. 51:9, 17; 52:1); “Simama, Ee Yerusalemu” (Isa. 51:17); “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja” (Isa. 52:9); ” Nendeni zenu, tokeni huko — (nchi za uhamishoni), (Isa. 52:11).

“Isaya sasa anazungumza na wacha Mungu katika Israeli, wale ambao kwa dhati na kwa bidii walitazamia utimilifu wa ahadi zilizotolewa kwa mababa lakini ambao walikuwa wamekata tamaa kwa sababu ya kuchelewa na kushindwa kwa ahadi hizo (Is. 49:4, 14; 50:1). Walikuwa wamesahau jinsi Bwana alivyowaongoza baba zao katika zama ziliopita. Sasa Mungu anawaalika kumgeukia, na kuhachana na  wasiwasi/ mashaka. Kwa wale wanaotafuta haki na ukombozi kuna njia moja tu ya kufikia malengo haya, na hiyo ni kwa utiifu wa uaminifu kwa sauti ya Bwana.” (SDA BC 4:284).

MAANA YA KIIBADA: Mungu anamwita kila mmoja wetu kuifuata haki! — Kujitahidi kuishi maisha ya haki na utakatifu; kumsikiliza Yeye; kutembea pamoja Naye, kuzingatia sheria/ maagizo Yake katika mioyo yetu (aya ya 7). Tunapaswa kumtafuta Bwana; tunapaswa kujiepusha na majaribu ya “kutafuta miungu mingine” kama vile wengi katika uhamishoni walivyofanya (Is. 40:19; 41:7; 44:9–20; 46:5–8). Tunapaswa kuangalia mwamba – ‘ule ambao tulitolewa kwa kuchongwa’ (aya ya 1). Yaani, kuzingatia historia yetu ya nyuma, enzi za mababu zetu. Tunapaswa kuzingatia historia ya ukombozi/ wokovu wetu: gharama kubwa iliyolipwa pale Kalvari. Tunapaswa kuwa na faraja kwa ajili ya siku zijazo kutokana na udhihirisho wa uaminifu wa Mungu katika zama zilizopita. Tunapaswa kusonga mbele, kwa shauku kuu, tukichuchumilia ushindi unaopatikana  katika Kristo Yesu! Tunapaswa kutoka huko (Babeli), kutogusa kitu chochote kichafu. Tunapaswa kuitikia mwito wa Bwana –”tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya Bwana.” (Isa. 52:11)

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza moja kwa moja nawe—kwa sababu hufanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, sitahacha ujaribiwe kuliko uwezavyo kustahimili (1 Kor. 10:13). Ninafahamu taabu, majaribu, na mateso unayopitia. Ninafahamu kuugua/ kutaabika kwako (Kutoka 2:23), Ninafahamu kilio/ huzuni zako (Kutoka 3:7). Nimekukomboa katika siku za nyuma, na Ninaweza kufanya hivyo tena! Ninao uwezo wa ‘kukuokoa kabisa’ (Ebr 7:25) na kukupeleka juu mbinguni (Yohana 14: 1-3). Je leo hii utanigeukia Mimi ili uokolewe?

Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, ninataka kukiri, kutubu dhambi zangu zote, na kumgeukia Mungu— kujikabidhi chini ya uongozi Wake, na kutii amri Zake.

Iweni na Alfajiri Njema: “Nisikilizeni, ninyi mnaoifuatia haki; ninyi mnaomtafuta Bwana; uangalieni mwamba ule ambao mlitolewa kwa kuchongwa, na tundu la shimo ambalo mlitolewa kwa kuchimbuliwa.” (Isaya 51:1)


 

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email