Toba Ya Kweli

September 17, 2020 in Usiku by TGVS

Wazo la Usiku linaloshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa Leo: Isaya 27/ Dhima: Toba Ya Kweli/ 23-BSG-20Y (Isaya 27:8-9)/ Wimbo: “Tumesikia Mbiu: Yesu Huokoa” (NK # 108).


 

Andiko Kuu: Isaya 27:8-9 — 8 “Umemwadhibu kwa kiasi, ulipomfukuza; ukampepeta kwa upepo mkali katika siku ya upepo wa mashariki. 9 Basi, uovu wa Yakobo utatakaswa hivyo, na hayo ndiyo matunda yote ya kumwondolea dhambi yake; afanyapo mawe yote ya madhabahu kuwa kama mawe ya chokaa yaliyopondwa, hata maashera na sanamu za jua havitasimama tena.”

TAFAKARI: “Aya ya 9 inaelezea kwa nini adhabu kwa Israeli itakuwa tofauti sana na adhabu kwa adui yake. Ingawa watu wa Mungu watateseka, kupitia uzoefu huu dhambi zao zitapatanishwa na hatia ya dhambi yao itaondolewa. Hii haimaanishi kwamba mateso huleta upatanisho wa dhambi, lakini kwamba mchakato wa mateso huleta mtu mahali ambapo dhambi hutambuliwa na kukiriwa ili kwamba Mungu aweze kusamehe. Moja ya dhambi kuu ambayo ilihitaji kupatanishwa ilikuwa ibada ya miungu ya kipagani katika madhabahu ya kipagani. Hatimaye watu wanapotambua ya kwamba miungu hii si kitu, “tunda kamili” au matokeo yatakuwa kwamba  watavunja madhabahu na sanamu hizi. Badiliko hili la nje litaashiria badiliko la ndani ya mioyo na hii ni ishara kwamba msamaha utawezekana.” [Gary V. Smith, Isaiah 1–39, ed. E. Ray Clendenen, The New American Commentary, (Nashville: B & H Publishing Group, 2007), 463].

MAANA YA KIIBADA: Hali ya Israeli ilihusisha hatua tatu. Kwanza,  Mungu ataleta adhabu (Isa. 27:8), kama  aya ya 7 inavyosema na kithibitishwa na Isa. 26:7-19. Pili, watu lazima waondoe sanamu zao za kipagani (Isa. 27:9b); hatimaye, Tatu,  Mungu atatoa upatanisho kwa ajili ya dhambi zao (Isa. 27:9a).

Wapendwa, Toba ya kweli inadhihirishwa katika matendo. Kipengele  cha kwanza kinaweza kutafsiriwa hivi: “katika masharti haya ndipo hatia ya Yakobo itakaposamehewa.” Lazima kuwe na ishara za matengenezo — uharibifu halisi wa sanamu na mahusiano yoyote na sanamu, kama thibitisho na dhihirisho la moyo la kujisalimisha na kujiepusha na ibada ya sanamu!

Toba ni kuacha (nyuma) dhambi tuliyoipenda kabla; na kuonesha kwamba kwa kujuta, na huzuni kuu, hatutarudia dhambi hizo kamwe!

Ndugu yangu mpendwa, unaposoma tafakari hii fupi, Je umefanya toba ya kweli? Je umekata shauri kuachana kabisa na dhambi zako? Ukweli ni kwamba hatuwezi wenyewe, lazima tumuendee Kristo, naye atatusaidia kuwa washindi dhidi ya dhambi. Bwana akubariki sana.


 

Usiku Mwema: “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:8-9)

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email