Ezekieli 29: Usomaji, Vidokezo
January 20, 2021 in Usomaji/ Vidokezo by TGVS
Usomaji wa Biblia kwa Mpango/ Kitabu cha Ezekieli 29/ Dhima: Ukiwa na Urejesho wa Misri (1-16)/ Misri kutolewa kwa Nebukadreza kama Malipo (17-21).
EZEKIELI 29:
1 Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, 2 Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao, mfalme wa Misri, ukatabiri juu yake, na juu ya Misri yote; 3 nena, useme, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ewe Farao, mfalme wa Misri, joka kubwa aoteaye kati ya mito yake, aliyesema, Mto wangu ni wangu mwenyewe, nami nimeufanya kwa ajili ya nafsi yangu. 4 Nami nitatia kulabu katika taya zako, nami nitawashikamanisha samaki wa mito yako na magamba yako; nami nitakutoa katika mito yako, pamoja na samaki wa mito yako walioshikamana na magamba yako. 5 Nami nitakuacha hali umetupwa jangwani, wewe na samaki wote wa mito yako; utaanguka juu ya uso wa uwanda; hutakusanywa, wala kuwekwa pamoja; nimekutoa uwe chakula cha wanyama wa nchi, na cha ndege wa angani. 6 Na watu wote wakaao Misri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, kwa sababu wamekuwa mwanzi wa kutegemewa kwa nyumba ya Israeli. 7 Walipokushika kwa mkono wako, ulivunjika, ukawararua mabega yao yote; nao walipokutegemea, ulivunjika, ukawatetemesha viuno vyao vyote.
8 Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitaleta upanga juu yako, nami nitakatilia mbali nawe wanadamu na wanyama. 9 Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya. 10 Basi, tazama, mimi ni juu yako, na juu ya mito yako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa jangwa tupu, na ukiwa, toka Migdoli hata Sewene, hata mpaka wa Kushi. 11 Hautapita kati yake mguu wa mwanadamu, wala hautapita kati yake mguu wa mnyama, wala haitakaliwa na watu, muda wa miaka arobaini. 12 Nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa ukiwa, kati ya nchi zilizo ukiwa, na miji yake, kati ya miji iliyoharibika, itakuwa maganjo muda wa miaka arobaini; nami nitawatawanya Wamisri kati ya mataifa, nami nitawatapanya kati ya nchi mbalimbali.
13 Maana Bwana MUNGU asema hivi; Mwisho wa miaka arobaini nitawakusanya Wamisri, na kuwatoa katika hizo kabila za watu, ambazo walitawanyika kati yao; 14 nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni. 15 Utakuwa duni kuliko falme zote; wala hautajiinua tena juu ya mataifa; nami nitawapunguza, ili wasitawale tena juu ya mataifa. 16 Wala hautakuwa tena tumaini la nyumba ya Israeli, kufanya maovu yakumbukwe, watakapogeuka kuangalia nyuma yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana MUNGU.
17 Ikawa katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana likanijia, kusema, 18 Mwanadamu, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alilihudumisha jeshi lake huduma kuu juu ya Tiro; kila kichwa kilitiwa upaa, na kila bega liliambuliwa ngozi, lakini alikuwa hana mshahara uliotoka Tiro, wala yeye wala jeshi lake, kwa huduma ile aliyohudumu juu yake. 19 Basi, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitampa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, hiyo nchi ya Misri; naye atawachukua watu wake jamii yote pia, na kutwaa mateka yake, na kutwaa mawindo yake, nayo yatakuwa ndio mshahara wa jeshi lake. 20 Nimempa nchi ya Misri kuwa malipo ya huduma aliyohudumu, kwa sababu walifanya kazi kwa ajili yangu; asema Bwana MUNGU. 21 Siku ile nitawachipushia nyumba ya Israeli pembe, nami nitakujalia kufumbua kinywa kati yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
MUHTASARI WA KUFUNDISHIA.
Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Ezekieli 29: Muhtasari wa Kufundishia/ Ezekieli 29, (26-BSG-29E)/ Dhima: Ukiwa na Urejesho wa Misri (1-16)/ Misri kutolewa kwa Nebukadreza kama Malipo (17-21).
Muhtasari: Sura tatu zilizopita zilihusu Tiro na mfalme wake. Sura nne zinazofuata zinaangazia Misri na mfalme wake. Katika sura hii, Ezekieli anapewa ujumbe wa hukumu kuhusu Farao na nchi ya Misri.
Wahusika: Mungu, Ezekieli, Farao, Nebukadneza.
Andiko Msingi: “Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa Mimi ndimi Bwana; kwa sababu amesema, Mto huu ni Wangu, Nami nimeufanya.” (Ezekieli 29:9)
Neno la Msingi: Ukiwa (Eze. 29:9)
Maandiko Makini: Ezekieli 29:1-2, 3, 4-5, 6, 8-9, 13, 19-20, 21.
Staanani ya Ibada: Kiburi/ (angalia kipengele cha “26-BSG-29Y” kwa maelezo zaidi)
Mgawanyo wa Mawazo Makuu — Dhambi za Farao (1–7)/ Uvamizi wa Nebukadneza (8–12)/ rehema ya Kiungu (13–16).
Matukio ya Biblia – [N/A].
Dhima za Biblia – (angalia Kipengele “H”).
Virai vya Biblia – “Bwana MUNGU asema hivi” (Eze. 29:8, 13, 19, 20); “Neno la Bwana likanijia, kusema” (Eze. 29:1, 17)
Mambo ya Kujifunza Zaidi – Mausia ya Ezekieli dhidi ya Mataifa, Imani, Hukumu, Kiburi, Unabii, Ufunuo, Kudra ya Mungu, Vita, Utajiri.
Taarifa za Kushangaza: 1. Hukumu ya Mungu itamwangamiza dubwana Farao, mataifa yenye uovu, na raia wanaowafuata/ 2. Mungu ataiadhibu Misri kwa kuifanya nchi yake ukiwa na kuwatawanya watu wake kwa miaka arobaini/ 3. Rehema ya Mungu: ataruhusu Wamisri warejee katika nchi yao baada ya miaka 40/ 4. Kusudi la Hukumu ya Mungu: kwamba watu wamjue BWANA, Mungu pekee wa kweli/ 5. Mungu atamlipa Mfalme Nebukadneza kwa ajili ya huduma yake katika kumhukumu Tiro
Wazo Kiini: Rehema ya Mungu juu ya Wapagani: “Nami nitawarejeza Wamisri walio katika hali ya kufungwa, Nami nitawarudisha hata nchi ya Pathrosi, hata nchi ya kuzaliwa kwao; na huko watakuwa ufalme duni.” (Ezekieli 29:14)
“Misri itatawaliwa na Nebukadneza; lakini baada ya muda, nira ya Wakaldayo itavunjwa shingoni mwake na Misri itarejeshwa ili iwepo katika mataifa. Hapa kuna ahadi ambayo kwa namna fulani ni sawa na ile ambayo manabii walirudiarudia kuiwasilisha kwa Wayahudi katika jina la Mungu. Sasa ahadi hii inakarimiwa kwa watu wapagani. Siyo tu kwamba Mungu ni Hakimu wa wapagani; Yeye pia ni Mwokozi. Hashughuliki na watu kwa namna moja tu. Hawekei mipaka mahusiano Yake kwa yeyote katika upande mmoja asili Yake. Lazima daima awe Yeye, nafsi Yake kamili na ya kweli. Lakini ile ya kimahakama, yaani ile tu uhusikayo katika kuhukumu adhabu, vyovyote vile haijumuishi asili yote ya Mungu. Kimsingi Mungu ni upendo. Kwa hiyo, wakati wowote Mungu anaposhughulika na kiumbe Wake yoyote, kwa vile daima yuko sahihi kwa asili Yake na huwatendea katika ukamilifu wa tabia Yake, lazima ajitokeze kwa upendo, japo mwanzoni upendo huu unaweza kufichika nyuma ya mawingu ya ghadhabu na hukumu. Katika Injili, Mungu anaonesha rehema Yake kwa wapagani. Kristo alikuja kwa sababu ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu. Sasa ni shauku ya Kristo kwamba injili Yake iweze kuhubiriwa kwa kila kiumbe.” [H. D. M. Spence-Jones, Ed., Ezekiel, The Pulpit Commentary, (London; New York: Funk & Wagnalls Company, 1909), 2:129].
MASWALI CHANGAMSHI:
- Nini maudhui makuu katika sura hii?
- Je sura hii inazungumza nini kuhusu Mungu?
- Unadhani ni wazo kuu ambalo Mungu anawasilisha kwa kuijumuisha sura hii kwenye Biblia?
- Ni mwitikio gani unaodhani sura hii inapaswa kutuhamasisha kufanya?
MASWALI YA KUJADILI:
- Wakati taifa la Tiro lililotegemea ustawi wake wa kiuchumi likiadhibiwa na Mungu kwa sababu ya kuidhihaki Yuda iliyokuwa imepokea maonyo kwa Bwana, Misri inaendeleza dhana ile ile ya kujiona mbabe anayeweza kuwalinda wale waliokataliwa na Mungu akitumainia mto Nile. Ni nini unachokitegemea zaidi maishani mwako ambacho siku kikiondoka na maisha yako yatakuwa yamefika mwisho?
- Je ni sahihi kumtegemeza aliyekataliwa na Mungu? Misri iliyookoa maisha ya mtoto Yesu alipokuwa anatafutwa na Herode iliwezaje kutofautiana na Mungu kwa kuisaidia Yuda? (Pr. Letta, S.)