Kutimiza Nadhiri kwa Mungu
July 8, 2022 in Mwongozo wa Ibada by TGVS
Kumbukumbu 23: Mwongozo wa Ibada/ 5-BSG-23A, (Kumbukumbu 23:21-23)/ Dhamira: Kutimiza Nadhiri za Kidini/ Wimbo: Take my life and let it be!
Uchunguzi: Mwa. 28:20; Hes. 21:2; 30:2–16; Waamuzi 11:30; 1 Sam. 1:11; 2 Sam. 15:7
Tafakari: Angalau sheria nane Musa amezichanganua na kuzihimiza katika sura hii na kwa ajili ya mwenendo wa Israeli katika nchi ya ahadi. Kumbukumbu la Torati 23 inaweza kugawanywa katika sehemu kuu nane kama ifuatavyo: Masharti ya utakatifu wa kutaniko la BWANA (23:1–8); Mwenendo wa Askari (23:9); Maagizo kuhusu usafi (23:10–14); Watumishi walioponyoka (23:15, 16); Utakatifu wa maadili (23:17, 18); Riziki kutokana na mikopo (23:19, 20); Taadhima wa nadhiri (23:21–23); Ulaji shambani (23:24, 25)
Kuna dhima nyingi hapa, lakini hebu tuzungumzie nadhiri. Mada ya nadhiri pia imezungumziwa katika Walawi 27 na Hesabu 30. Kijumla, nadhiri ni ahadi anayopewa Mungu ambayo hushabihi sharti Lake la kutujalia matokeo au manufaa mema. Mungu aliamuru waziwazi kwamba Israeli iwe makini kutunza nadhiri zao na kutimiza kila kiapo kilichowekwa (Kumb 23:21-23). Mwabudu alikuwa akija kwenye hema la kukutania (au baadaye, hekalu) na kutangaza hadharani, “Endapo Mungu akiridhia (manufaa yanayohitajika), basi nitatoa (shekeli kiasi fulani) kwa maskini (au kusudi fulani lingine).” Mtu angeweza kuweka nadhiri kwa BWANA kwa namna ya utumishi aliomfanyia (Hes. 6:2, 5, 21) au dhabihu ambayo ingetolewa kama tendo la ibada (Hes. 15:8; Kumb 12:6; Zab. 66:13-14). Mtu angeweza kuweka nadhiri ya kutoa, au kufanya kitu fulani kwa ajili ya Mungu, ili ajaliwe baraka maalum. Pia ingehusisha kujiepusha na kitu fulani ili kumpendeza Mungu. Nadhiri zilikuwa hiari kabisa (Kumb. 23:22), na zilipaswa kutangazwa waziwazi na kutimizwa kwa utiifu (Kumb. 23:23). Chochote kilichoahidiwa kilipaswa kuletwa patakatifu na kukabidhiwa kwa BWANA (Mhu. 5:4–6). Kuahidi na kutoitimiza ilihesabika kama kulitaja bure jina la BWANA (Kut. 20:7; Mit. 20:25).
Maana ya Kiibada: Ingawa nadhiri iliwekwa kwa hiari, kukataa kuitimiza, mara ilipowekwa, ilikuwa (na bado ni) kumwibia BWANA kile kilichokuwa Chake kwa haki. Unajua Mungu anawapenda watu Wake sana na anatamani kujibu matakwa yao (au maombi). Wakati fulani Yesu alitupatia changamoto, “Ikiwa Baba Yangu huwalisha ndege wa angani, hivi ni mara ngapi zaidi atawajali ninyi?” (Mat 6:26). Hakuna kosa lolote katika kueleza shauku/ na kuweka nadhiri kwa Mungu, ila ni lazima “ifikiriwe vilivyo” kwanza kwa sababu madhara ni makubwa kwa kushindwa kutimiza kile kilichowekwa nadhiri! Nadhiri taadhimu zinazowekwa kwa Yehova ni sharti ambalo halipaswi kupuuzwa. Nadhiri lazima zitimizwe kwa sababu Mungu hutimiza ahadi Zake na anatamani kwamba watu Wake waige tabia Yake ya maadili. Kwa hiyo ni lazima tuwe waangalifu kabla ya kuweka nadhiri. Nadhiri mbele ya Mungu si jambo dogo. Katika jamii nyingi leo, kuvunja nadhari ni desturi ya kawaida tu—lakini mbele ya Mungu, ni kutenda dhambi.
Sauti ya Injili: Sehemu hiyo imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu Yeye anafanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, “unapoweka nadhiri kwa BWANA, Mungu wako, timiza upesi chochote ulichomwahidi. Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, anataka utimize nadhiri zako zote upesi, la sivyo utakuwa na hatia ya dhambi. Hata hivyo, si dhambi kuacha kuweka nadhiri. Lakini ukishaweka nadhiri kwa hiari, zingatia kuitimiza ahadi yako kwa BWANA, Mungu wako.” (Kumbukumbu 23:21–23, NLT)
Shauku Yangu: Kwa neema ya Mungu, nataka kukumbuka aina zote za nadhiri ambazo nimewahi kuziweka kwa BWANA, na kuzitimiza.
Uwe na Siku Yenye Baraka: “Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho. Bali “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo,” na “Siyo,” yenu iwe “Siyo,” msije mkaangukia hukumu.” (Yakobo 5:12)