Walawi 21: Maswali & Majibu

May 4, 2022 in Mwongozo wa Biblia by TGVS

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Walawi 21, (3-BSG-21J)/ Katika ibara fupi, jibu maswali au andika mawazo makuu uliyojifunza katika sura hii.

 


Utangulizi: “Ujumbe wa sura ya 21 ni makuhani na familia zao. Ni lazima wajiepushe na unajisi wa kila aina. Watu waliruhusiwa kufanya mambo fulani yaliyokatazwa kwa makuhani. Kwa upande mwingine, makuhani wa kawaida walipewa uhuru zaidi kuliko kuhani mkuu. Ilikuwepo mizani ya viwango vya maadili yaliyokuwa makali zaidi kulingana na cheo cha mtu.” (SDA BC 1:795). Makuhani walipewa sheria kali zaidi (kama tutakavyoona hapa kwa ufupi) kuliko raia wa kawaida kwa sababu ya silika ya kazi yao.

[1] Je, sura hii inahusu nini? – Sheria zinazowaongoza Watumishi wa Mungu (Makuhani): Maagizo ya Msingi na Sifa za Makuhani, 21:1–24.

[2] Je, wajibu wa mwanadamu kwa Mungu ni upi? – Lazima awe mtakatifu! — Kwa sababu Mungu ndiye BWANA; Kwa sababu Mungu ni mtakatifu; Kwa sababu BWANA ni Mungu “wako” (Law. 19:1-2); Lazima mwanadamu ajitakase nafsi yake “na kuwa mtakatifu,” kwa sababu BWANA ameamuru hivi: “Kwa maana Mimi ndimi Bwana, Mungu wako.” (20:7)

[3] Mtoa-sheria ni nani? BWANA Mungu. Je, nani aliye Hakimu anayetangaza adhabu katika sura hii? BWANA Mungu.

MAAGIZO YA MSINGI KWA KUHANI – (Sehemu ya 1).

[4] Lipi agizo la kwanza kuhusu mwenendo wa kuhani? – Asijitie unajisi (kujichafua) kwa kugusa maiti (21:1).

 • “Marufuku kuhusu maiti haikuwa tu kugusa maiti, bali hata kuwa katika chumba kimoja na maiti au kutembea juu ya kaburi au kuligusa kaburi.” (David Guzik).

[5] Wataje jamaa sita wa karibu ambao kuhani angeweza kujitia unajisi kwao.— “Isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume; na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.” (Walawi 21:2–3)

 • Isipokuwa kwa hawa jamaa wa karibu, Makuhani hawakuruhusiwa kugusa maiti, au kuwa mahali alipo maiti: kugusa maiti au kusaidia katika kuitayarisha kwa maziko.

[6] Kwa nini tofauti hii ilibainishwa? — Ili kuonesha upendo mkuu, faraja, na tumaini kwa kuiombolezea familia yake ya karibu inayomtegemea.

 • Zingatia: Makuhani hawakupaswa kujitia unajisi kwa kuomboleza kupita kiasi, au kwa kukatiza utumishi wao kupita kiasi kwa ajili ya jamaa wengine wanaokabiliwa na kifo.
 • “Katika nyakati za Biblia, kuonesha huzuni ilikuwa ni mbinu iliyofanywa na watu waliokuwa na fani ya kuomboleza (Mwa. 50:7–11; 2 Nyak. 35:25; Marko 5:38). Ingawa Mungu alitarajia makuhani waoneshe huzuni kwa kifo cha mpendwa wao, alitarajia pia watende kama watumishi wa Mungu. Yeyote aliyegusa maiti, au hata kuingia katika hema alimo mtu fulani aliyekufa, alitiwa unajisi kwa muda wa juma moja, na unajisi ungemzuia kuhani huyo kuwatumikia watu (Hes. 19:11–14). Kwa hiyo, makuhani wangeweza kujitia unajisi tu kwa ajili ya wazazi wao, watoto wao, na kaka zao na dada zao ambao hawajaolewa, lakini wengine wote waliokufa walikuwa wamewekewa mipaka kwao. Utii ulipaswa kuwa kipaumbele kuliko upendo.” – [Warren W. Wiersbe, Be Holy, “Be” Commentary Series, (Wheaton, IL: Victor Books, 1996), 91].

[7] Ni yapi Maagizo mengine kuhusu mwenendo wa Kuhani ambayo yamebainishwa hapa? – (21:10-15)

 1. Asifuate desturi za kipagani kama vile kuuharibu mwili wake (cf. Law. 19:27–28)
 2. Ni lazima aishi maisha matakatifu na safi kwa ajili ya Mungu.
 3. Asitilie unajisi jina la Mungu kamwe, kwa maana ametengwa kwa ajili ya vitu vitakatifu—(kwa ajili ya utumishi wa Mungu, ili kuhudhurisha matoleo kwa Bwana, kumpendeza Bwana)
 4. Lazima amwoe mwanamke safi: Si mwanamke aliyetiwa unajisi kimapenzi au talaka. Sababu: Utakatifu
 5. Lazima awe na ushuhuda thabiti wa utakatifu, wa kutengwa kabisa kwa ajili ya Mungu — Kwa sababu anamtumikia Mungu, kwa vile Mungu ni mtakatifu.
 6. Anapaswa kuwa na watoto wanaomcha Mungu – Kumbuka kwamba binti (au mwana) anayekuwa kahaba lazima ahukumiwe kwa sababu anamdhalilisha baba yake na Mungu

MAAGIZO YA MSINGI KWA KUHANI MKUU – (Sehemu ya 2).

[8] Lazima awe na upako wa pekee na mavazi ya ukuhani! – (Law. 21:10)

 • Kuhani mkuu aliwekwa wakfu kwa Mungu. Alivaa mavazi [matakatifu] ya ukuhani. Hakuruhusiwa kufunua kichwa chake wala kurarua nguo zake (kwa kuomboleza).

[9] Hapaswi kamwe kutiwa unajisi kwa mauti! – (Law. 21:11)

 • Kuhani mkuu hakuruhusiwa kumkaribia “mtu yeyote aliyekufa,” – hata baba yake au mama yake. Kwa kufanya hivyo, angejitia unajisi.
 • Hakupaswa kuhuzunika (kuomboleza) kifo, wala kuweka kando utumishi wake kwa Mungu ili kwenda kuwazika wafu (cf. Mat. 8:21–22).

[10] Asitoke katika mahali Patakatifu (wala asipanajisi); kwa kuwa usahimisho wa mafuta ya upako wa Mungu uko juu yake! – (Law. 21:12)

 • Kupanajisi Patakatifu ni kupafanya pawe pachafu kiibada.
 • Usahimisho wa mafuta ya upako (juu ya kichwa cha kuhani mkuu) ilikuwa ishara ya Yesu Kristo, Kuhani Mkuu mkuu zaidi ambaye angekuja, ambaye mtume Petro alizungumza habari Zake:
 • Jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; Naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja Naye.” (Matendo 10:37–38)

ZINGATIA: “Ijapokuwa sheria zilikuwa kali kwa kuhani, bado zilikuwa kali zaidi kwa kuhani mkuu. Yeye pekee kati ya makuhani wote ndiye alikuwa amepakwa mafuta kichwani, yeye pekee ndiye alisahimishwa ili kuvaa mavazi ya dhahabu. Hapaswi kufunua kichwa chake, kwa kuwa hilo lilimlazimu kuondoa bamba la dhahabu ambalo juu yake yalikuwepo maandishi “Utakatifu kwa Bwana.” Hapaswi kuyararua mavazi yake, kama ilivyokuwa desturi mtu anapokuwa na huzuni nyingi. Hapaswi kuikaribia maiti, hata ya baba yake au mama yake. Maneno ya Kristo kwa mtu ambaye angekuwa mwanafunzi Wake yanaonekana kuakisi utaratibu huu (Mat. 8:22). Iwapo kuhani mkuu angefanya hivyo, angekuwa najisi na hivyo kushindwa kutimiza wajibu wake takatifu.” — (The Seventh-day Adventist Bible Commentary, 1:796).

[10] Lazima amwoe mwanamke aliye safi (bikira): Si mjane, mtalikiwa, wala kahaba! – (Law. 21:13-14)

 • Sababu: Kuhani mkuu lazima amwoe bikira kutoka kwa watu wake mwenyewe ili “kuwahakikishia” watoto watakatifu, wacha-Mungu wasio na lawama, na warithi wa familia ya makuhani (ukuhani mkuu).
 • Watoto wa muunganiko wowote [pamoja na mjane, mtalikiwa, au kahaba] “hawatastahili kurithi nafasi ya baba yao, kwa vile yeye mwenyewe hangestahili kwa kukiuka sheria inayokataza muunganiko huo. Sheria hizi ziliwasilishwa ili kuhifadhi ukuhani kama utaratibu mtakatifu. Makuhani lazima wawe safi katika mambo yote, ili wastahili heshima ya watu.” – (SDA BC 1:796).

[11] Hapaswi kutia unajisi mzao wake — “Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe. Naye asiwatie unajisi kizazi chake katika watu wake; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nimtakasaye.” (Law. 21:14-15).

 • “Kiwango cha juu zaidi katika mahusiano ya ndoa kilitarajiwa kwa kuhani mkuu. Pamoja na maagizo kwa ajili ya ndoa ya makuhani wa kawaida katika mstari wa 7-9, Yehova aliongeza kwamba kuhani mkuu hakupaswa kumwoa mjane. Mke wa kuhani mkuu alipaswa kujisabilia sana kwa mumewe na kwa utumishi wake kwa Mungu kiasi kwamba alitakiwa kuwa mwanamke ambaye hakuwahi kamwe kuwa na uhusiano wowote na mwanamume mwingineyo. Pia, mke wa kuhani mkuu, kama mke wa kuhani wa kawaida, alipaswa kuwa “wa watu wake,” ikiwa na maana kwamba mke huyo alipaswa kuwa wa kabila la Lawi. Kauli hii huonesha kwamba tayari Yehova alikuwa amepanga kuwaweka Walawi mahali pa wazaliwa wa kwanza wa Israeli, ingawa utengano wao rasmi na kutakaswa haukufanyika hadi Hesabu 3. Mwanamke huyo alipaswa atoke katika familia ambayo Mungu angeitenga kama watumishi wa pekee walijisabilia utumishi Wake mtakatifu. Alipaswa kuitwa mahali pake pa huduma kama ilivyokuwa kwa mumewe.” — (Leon Hyatt, Leviticus 21:1-15 Commentary)

[12] Maana ya Kiibada: Kuhusu mwenendo wa Mchungaji, Familia (maisha ya ndoa), na utumishi kwa Mungu.

“Wachungaji Wakristo ni viongozi miongoni mwa watu wa siku hizi, waliotengwa ili kuliwakilisha jina na kusudi la Yesu. Kwa hiyo, wanapaswa kuwa kielelezo katika mwenendo wao. Hawaishi kwa viwango tofauti vya maadili, lakini wana wajibu wa pekee wa kuishi kikamilifu kulingana na maadili hayo. Lazima waweke kielelezo cha uaminifu kwa amri za Mungu kwa sababu ya nafasi yao yenye ushawishi mkubwa. Wanawajibika kuonesha imani yao nyakati za huzuni na kifo. Hawatakiwi kuepuka kuigusa maiti ya wapendwa wao kama ambavyo ilivyokuwa kwa makuhani wa Israeli kwa sababu vielelezo vya kidini vya usafi na unajisi haitakiwi tena kwa watu wa Mungu. Hata hivyo, wachungaji wa Yesu wanatazamiwa kuweka utiifu kwa Mungu uwe kipaumbele zaidi ya huzuni yao na kuonesha imani yao wanapokabili kifo.

Mavazi na unadhifu wa mchungaji pia ni muhimu. Viwango vya unadhifu hubadilika. Hakuna sheria za kudumu zinazoweza kuwekwa ili kufafanua kwa kina mavazi na unadhifu wa mchungaji, lakini lazima kujipamba kwake kuoneshe kwamba yeye si wa ulimwengu na ametengwa kwa ajili ya Mungu. Wajibu huu haumaanishi kwamba anapaswa kuvaa vazi dhahiri la “kichungaji” tu bali aepuke mavazi na unadhifu unaotambuliwa kuwa wa kilimwengu, usio wa adabu, au hata wa hovyo na kutojali.

Ndoa na nyumba ya mchungaji vina umuhimu maalum. Lazima amwoe mwanamke anayedumisha viwango vyake vya juu vya uadilifu na usabilifu usio na ubinafsi kwa utumishi wa Mungu. Watoto wa mchungaji wanapaswa pia kutambua fadhila na wajibu wa kipekee. Wanapaswa kuepuka hasa ukiukaji mkubwa wa ndoa na viwango vya maadili vya Mungu. Kadiri wanavyoishi kwa viwango vya juu zaidi, ndivyo huduma ya baba yao itaimarika zaidi.” — (Leon Hyatt – Leviticus 21:1-15 Commentary)


 

MWISHO WA SOMO: Bwana Akubariki unapoendelea kuwaombea wachungaji, wazee wa makanisa, mashemasi & watendakazi wengine wa Kanisa.

Comments
Print Friendly, PDF & Email