Mambo Manne ya Ushindi

August 9, 2022 in Usiku by TGVS

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Waamuzi 1, (7-BSG-1Y)/ Dhima: Mambo Manne Muhimu kwa ajili ya Ushindi/ Wimbo: Faith is the Victory [Mwandishi: John H. Yates]


 

Andiko Kuu: “Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, ‘Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?’ Bwana akasema, ‘Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake.’” (Waamuzi 1:1–2)

Tafakari: Israeli ilianza vyema katika sura hii kwa kumwomba Mungu awaoneshe ni nani anayepaswa kuwa ‘wa kwanza kwenda kupigana na Wakanaani’ (1:1). BWANA akajibu: Yuda angeongoza mashambulizi hayo, na pia aliwahakikishia kwamba angewatia adui mikononi mwao! Kwa hiyo, wakaenda kufanya kazi—na kupigana kwenye vilima (1:9–15), kwenye nyanda za chini za kusini (1:16–17), na katika maeneo ya pwani (1:18). Mbinu yao ilifanikiwa kwa sababu “BWANA alikuwa pamoja nao” (1:19). Hizi hapa dondoo kadhaa za ibada

[1] Siri ya kwanza ya ushindi ni Maombi. Kabla tu Yoshua hajafa, aliwapa changamoto Israeli kuweka wakfu upya maisha yao kwa Mungu na kufanya upya agano lao (azma yao) kwa Mungu. Soma Yoshua 24:15–16; 19–24. Watu waliikubali changamoto hiyo na kuamua kumtii na kumfuata BWANA.

[2] Siri ya pili ya ushindi ni Neno la Mungu na Uhakikisho: “Yuda atakwea. Hakika nimeitia nchi mkononi mwake” (aya ya 2). Siyo tu kwamba Mungu alijibu maombi ya Israeli bali pia alizungumza nao na kuwapa Neno Lake na uhakikisho wa ushindi. Wapendwa, kila mara tunaanza vyema tunapotafuta mashauri ya Mungu mwenye uweza wote, mjuzi wa yote, Mungu Aliye Hai na Mtawala wa Ulimwengu. Kutafuta hekima na mapenzi ya Mungu daima ndiko mahali pazuri pa kuanzia mpango, mradi, au uamuzi wowote maishani mwetu.

[3] Huduma ni siri ya tatu ya ushindi—kuwasaidia ndugu walio dhaifu (Waamuzi 1:3a). Kabila la Yuda liliongoza mashambulizi dhidi ya maadui. Lakini kabla ya kabila hilo kuanza vita, muungano uliundwa na kabila dhaifu la Simeoni. Kuna hekima katika kuunganisha nguvu ili kushambulia adui wa pamoja.

[4] Siri ya nne ya ushindi ni Utiifu (Waamuzi 1:3b). Askari wa Simeoni walijiunga na Yuda. Makabila haya mawili yalienda pamoja ili kuwafukuza maadui waliotaka kuwatumikisha na kuwaangamiza. Picha hapa ni utii: walimtii Mungu!

 

Maana ya Kiibada: “Kushindwa wakati fulani maishani mwako ni jambo lisiloepukika, lakini kukata tamaa hakusameheki.” (Joe Biden, US President). Katika sehemu hii ya utangulizi ya sura, tunayo maelekezo kuhusu mafanikio na ushindi. Katika maisha haya, tutakabiliana na majaribu mengi, taabu (maradhi, ajali, hasara, mfadhaiko, upweke, utupu, kukosa tumaini), na hata kifo. Tunawezaje kuwa washindi? Tunawezaje kushinda mambo haya? Kwanza, kwa njia ya Maombi! Ni lazima tumtafute BWANA kwa bidii, na “kutafuta” huko lazima kudhihirishwe kwa utii wetu wenye tumaini na kumtegemea Yeye – (Mat 26:41; Yn. 15:7; Yakobo 5:13; 1 Yn. 3:22). BWANA, kupitia nabii Yeremia, anaandika muhtasari wa ‘kutafuta’ huku kwa njia hii: “Nanyi mtanitafuta na kunipata mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.” (Yeremia 29:13)

Pili, Utii kwa Mungu. Kristo alitufundisha, “Si kila mtu aniambiaye, ‘Bwana, Bwana,’ atakayeingia katika ufalme wa mbinguni, bali ni yule afanyaye mapenzi ya Baba Yangu aliye mbinguni.” (Mathayo 7:21). Wapendwa, Mungu havutiwi na huduma ya midomoni. Anadai utii kutoka moyoni – (kutoka ndani kwenda nje). Kukiri “Bwana, Bwana” bila kumtii Kristo kwanza kunavunja tu Amri ya Tatu (Kut. 20:7). Na kama tumesahau, Imani na Matendo huenda pamoja — matendo bila imani yamekufa, na imani bila matendo imekufa. Soma –(Yakobo 2:17-18, 26; Mat 5:16; Ebr. 11:6; Tito 1:16).

Tatu, Neno la Mungu lazima liwe GPS yetu – “mwongozo wa miguu yetu na mwanga wa njia yetu” (Zab. 119:105). “Ninyi mmeshakuwa safi,” Yesu aliwaambia wale wanafunzi kumi na mmoja waaminifu, “kwa sababu ya Neno nililowaambia.” (Yohana 15:3). Hilo “Neno la Kristo” (Kol. 3:16) ni muhimu sana katika utakaso wa awali wa kila mwamini katika wokovu (Rum. 1:16). Neno la Mungu daima husafisha, hupogoa, na kumtakasa muumini. Sura mbili baadaye, Kristo anaongeza, “Uwatakase kwa ile kweli Yako. Neno Lako ndiyo kweli.” (Yohana 17:17). Mtunzi wa Zaburi anathibitisha, “Neno Lako” Ee Mungu, “nimeliweka moyoni mwangu, nisije nikakutenda dhambi” (Zaburi 119:11). “Mafundisho ya [neno la Mungu] huleta nuru, kiasi kwamba hata wajinga wanaweza kuelewa.” (Zaburi 119:130, NLT) Hebu pia niongeze kwamba kwa kuwa tunapigana dhidi ya maadui halisi katika ulimwengu wa roho, tunahitaji sana vifaa maalum -(vya mashambulizi na kujihami)- ili kutusaidia kushinda vita dhidi ya Shetani na nguvu zote za uovu. Wapendwa, hebu tutumie fursa ya neno la Mungu, “silaha zote za Mungu” (Waefeso 6:11–12, 13-16, 17-18).

Kipengele cha Mwisho kwa ajili ya kuishi maisha yenye ushindi ni Utumishi—kuwasaidia waumini walio dhaifu. Yesu alimwagiza Petro, “Lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; na utakaporudi Kwangu uwaimarishe ndugu zako.” (Luka 22:32) Baada ya kupitia jaribu na dhiki kali zaidi maishani na kupata uzoefu wa tabia ya kudumu ya imani iokoayo, sisi, pia, lazima tuwe “nguvu kwa ndugu zetu walio dhaifu zaidi” katika Kristo. Ni lazima tuwaimarishe na kuwatia moyo katika kutembea kwao na Bwana.

Wito wa Mungu kwa kila muumini ni Utumishi: kuwatumikia na kuwahudumia watu wengine: “Wapendwa kaka na dada, iwapo muumini mwingine ameshindwa na dhambi fulani, ninyi mlio wacha-Mungu mnapaswa kumsaidia mtu huyo kwa upole na unyenyekevu arudi kwenye njia sahihi. Na iweni waangalifu msianguke kwenye jaribu lilelile ninyi wenyewe. Saidianeni mizigo yenu, na kwa njia hii tiini sheria ya Kristo.” (Wagalatia 6:1–2, NLT)

 


Uwe na Usiku Mwema: “Wala tusichoke wakati tukitenda mema, maana katika muda mwafaka tutavuna tusipozimia moyo. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi, hebu tuwatendee watu wote mema, na hususan wale walio wa nyumba ya imani.” (Wagalatia 6:9–10, NKJV)

Comments
Print Friendly, PDF & Email