Anza na Bwana, Agosti 5, 2022

August 5, 2022 in Alfajiri, Mwongozo wa Maombi by TGVS

NUSU-KABILA LINGINE LA MANASE (Yoshua 17)

Sura hii inahusika na nusu-kabila lingine la Manase, tofauti na ile nusu tuliyoiona katika somo la jana (Yoshua 16:4), ambayo alipokea sehemu yake ya urithi uliogawanyika Magharibi mwa Yordani. Nusu-kabila la kwanza la Manase lilitaka kubaki upande wa Mashariki wa Yordani. Hawakutaka “kuvuka” Yordani katika nchi ya ahadi. Walipenda na kutamani kile walichokiona. Hapa kuna onyo dhidi ya maridhiano na wadhambi (17:12), ubinafsi, na tamaa.

Hii ni kama wengi wetu leo: tumedhamiria kufanya mambo kwa njia yetu wenyewe. Hatuna heshima tena kwa Mungu wala Sheria yake takatifu. Tunapenda kile tunachokiona ulimwenguni, na hatujali kabisa kuhusu utakatifu au utakaso.

Roho Mtakatifu leo anatuhimiza – “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” (1 Yohana 2:15-17)

Nusu-kabila lingine la Manase lilikuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mungu. Hawa walikuwa jamii waliyokubali urithi wao upande wa Magharibi mwa Yordani – (ndani ya nchi ya ahadi). Hebu, mwombe Mungu akusaidie leo uwe mtoto Wake mwaminifu na mtiifu!


 

Ibada Ya Maombi (Alfajiri).
[1] “Mnapoomba leo nisaidieni kumbea afya yangu.. Mguu wangu una tatizo miezi 3 sasa… Bwana auponye” (RM); [2] “Lakini pia nina changamoto kazini kwangu, Bwana ashughulike nayo” (RM); [3] “Nina changamoto ya masikio yote mawili yanapiga kelele; imepelekea hadi Sasa sisikii vizuri” (MA); [4] “Nina changamoto ya kutoridhika na mke wangu wa ndoa… mniombee ili nitubu” (NL); [5] Ombea maandalizi ya Masomo haya ya Biblia, ili Roho Mtakatifu aendelee kuongea na kila msomaji, aokolewe na kupata Uzima wa Milele; [6] Ombea mtu mmoja anayetaabika kwa Ugonjwa Fulani na hana Fedha za matibabu; [7] Katika somo la leo (Yoshua 17), ombea Uaminifu na Utii kwa Mungu, kama “nusu-kabila” lingine la Manase.

SALA: Baba, asante tena kwa zawadi ya uhai leo. Sisi ni wakosaji mbele Zako, tusamehe Bwana. Tunaleta mizigo hii mbele Zako, Bwana. Ukatuangalie kwa jicho la huruma na ukapate kujibu maombi ya wana wako. Tusaidie ili tuwe waaminifu na watii mbele Zako daima, hata kama itatugharimu. Zaidi ya yote, hebu mafundisho yatakayotolewa hapa leo, yakapate kutusaidia kukua kiroho, na kutuandaa kwa ajili ya Umilele. Tumeomba haya katika jina la Yesu Kristo, Amina.


 

AHADI YA LEO.

Dhima: Mungu hukirimia wale wanaomtii.

  1. “Nawe ukienda katika njia Zangu, na kuyashika mausia Yangu, na amri Zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi Nitazifanya siku zako kuwa nyingi.” (1 Wafalame 3:14)
  2. “Sasa basi ikiwa mtaitii sauti Yangu kweli kweli, na kulishika agano Langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu Kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu” (Kutoka 19:5)
  3. “Mkizishika amri Zangu, mtakaa katika pendo Langu; kama vile Mimi nilivyozishika amri za Baba Yangu na kukaa katika pendo Lake.” (Yohana 15:10)

TUNAKARIBISHA:

  1. Nyimbo za Injili
  2. Ushuhuda
  3. Maombi (Sala)
  4. Kesha la Asubuhi
  5. Mahitaji (Changamoto za Kuombea).

Au, Jambo lolote la kiroho ambalo unaguswa kushirikisha watu wa Mungu. Bwana Awabariki.

 

 

 

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email