Kutafuta Maongozi ya Kiungu

August 10, 2022 in Alfajiri, Mwongozo wa Maombi by TGVS

WAAMUZI 1B: MWONGOZO WA MAOMBI.

Waamuzi 1: Mwongozo wa Maombi/ 7-BSG-1B (Waamuzi 1:1-2)/ Dhima: Kutafuta Maongozi ya Kiungu/ Wimbo: Open my Eyes that I may see!


 

Andiko Kuu: “Sasa baada ya Yoshua kufa ikatokea kwamba wana wa Israeli walimuuliza BWANA, wakisema, ‘Nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu dhidi ya Wakanaani ili kupigana nao?’ Naye BWANA akasema, ‘Yuda atakwea. Hakika, nimeitia nchi hiyo mkononi mwake.’” (Waamuzi 1:1–2, NKJV)

Maelezo ya Ufunguzi: “Neno la Kiebrania linalotafsiriwa hapa “walimuuliza” mara nyingi pia hutafsiriwa “kutaaradhi,” au “kuomba ushauri” (angalia sura ya 18:5; 20:18). Neno hilo linatumika kwa ajili ya maulizo ya kuhani akitumia Urimu na Thumimu (Hes. 27:21), ambayo yawezekana ndiyo njia iliyotumika hapa. Ni muhimu kujua kwamba Waisraeli waliuliza ushauri kwa Bwana. Yoshua alipokuwa hai, walikuwa wamemtegemea yeye. Sasa, wakiwa wameachwa bila kiongozi na wakikabiliwa na hatari, hawakutegemea hekima yao wenyewe, bali kwa kufuata maagizo ya Musa, walimwomba Mungu awaelekeze (angalia Yakobo 1:5). Ombi lao lilikuwa rahisi na la moja kwa moja, lisilokuwa na “marudio batili” ya kupayukapayuka (Mat. 6:7). Ufasaha wa sala uko katika utambuzi wa hitaji lake na ubayana wake. Ni jambo la lazima katika karne ya 21 kama ilivyokuwa katika siku za waamuzi kwamba watu wa Mungu watafute maongozi ya kiungu kabla hawajafanya maamuzi muhimu. Utafutaji huu haupaswi kufanywa kwa harara, hovyo, au akili ikiwa imeazimu na uamuzi ukiwa umefikiwa mapema. Maombi kama hayo ya kutafuta maongozi ni dhihaka. Mungu huwaheshimu wale tu wanaomjia kwa unyofu na kwa akili elekevu—wale walio tayari kufuata njia anayoionesha.” – (SDA BC 2:307–308).

Maadili ya Kukuza: Imani, Maombi, Utii, na Utumishi (angalia kipengele “7-BSG-1Y” kwa maelezo zaidi)

Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Utumwa; Ukatili (ukorofi); Kushindwa au kukataa kuwafukuza Wakanaani “wote” – “zile dhambi mahususi “zinazotunasa kirahisi” (Ebr. 12:1) na kuweka ukuta wa utengano kati ya Mungu na sisi (cf. Isa 59:1-2).

Jambo la Kumshukuru Mungu: Baraka, uwepo wa Mungu, majaliwa ya Mungu, rehema/huruma za Mungu, Maombi yaliyojibiwa, Ufunuo wa Kiungu, Ushindi dhidi ya nguvu za uovu.

Masuala ya Kuombea: Kutafuta mapenzi ya Mungu kwa njia ya Maombi, Ujasiri wa kuwafukuza Wakanaani, Imani inayothibitishwa kwa utii wa kufanya mapenzi ya Mungu.

Ahadi ya Leo: “Ikiwa watu Wangu, walioitwa kwa jina Langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” (2 Nyakati 7:14)

 

WAAMUZI 1Z: OMBI LA KUHITIMISHA.

Ombi la Kuhitimisha/ Waamuzi 1, (7-BSG-1Z)/ Je kuna hitaji lolote ninaloweza kuomba/kuwasilisha katika sura hii? Ndiyo.


 

Sala: Baba, tunakushukuru tena kwa neno Lako katika Waamuzi sura ya kwanza. Tunakushukuru kwa zawadi ya uzima, kwa nafasi nyingine ya kuisikia Injili na kufanya mabadiliko muhimu katika maisha yetu.

Baba, tuliona orodha ya dhambi katika sura hii. Kama Israeli wa zamani, sisi ni wadhambi tunaomhitaji Mwokozi. Tusaidie kuwachunguza na kuwatambua ‘Wakanaani’ wanaokaa ndani ya mioyo yetu na kutubu mara moja.

Tunakushukuru kwa kusikiliza maombi yetu! Wana wa Israeli walipokuuliza mambo ya vita (kuwashinda adui), siyo tu kwamba ulijibu bali uliwapa ushindi (Waamuzi 1:1-2). Tunajua kwamba yeyote anayekuja Kwako kwa uaminifu kwa ajili ya maelekezo, kamwe hatakataliwa. Mara nyingi, kwa sababu ya kutokuwa na imani, tunashindwa vibaya katika juhudi zetu. Baba, tusaidie kutumia fursa hii ya kuwasiliana Nawe. Tusisahau kamwe kwamba nguvu zetu ziko kwa Bwana na katika uweza wa uweza Wake (Efe. 6:10).

Baba Mpendwa, tafadhali kuwa pamoja nami kila wakati katika majaribu, matatizo na dhiki zangu zote maishani. Uwe pamoja nami katika kukatishwa tamaa na kushindwa kwangu. Unitegemeze kwa mkono Wako uletao wokovu, nami nitakuwa “zaidi ya mshindi” (Warumi 8:37) katika Yesu Kristo. Nizingire kwa neno, upendo Wako, na ulinzi wa Malaika. Nijaze Roho Wako ili “nistahimili kuzipinga hila za mwovu’ (Efe. 6:10-13).

“Fumbua macho yangu ili niione nuru za ukweli ambazo umenihifadhia!” Na kadiri ninapoanza Kitabu cha Waamuzi, ruhusu Roho Wako anifundishe kuyatii mapenzi, amri na maagizo Yako. Tusamehe, Bwana mpendwa, na kutuandaa kwa ajili ya ufalme Wako. Tunakushukuru, Baba, na tunakuja tukiamini na kulitumainia jina la thamani la Yesu Kristo, Amina.

 

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email