Kuiasi Amri ya Mungu
August 21, 2022 in Alfajiri, Mwongozo wa Maombi by TGVS
WAAMUZI 2B: MWONGOZO WA MAOMBI.
Waamuzi 2: Mwongozo wa Maombi/ 7-BSG-2B (Waamuzi 2:2, 11-13)/ Dhima: Kuiasi Amri ya Mungu/ Wimbo: Trust and Obey (SDAH 590).
Andiko Kuu: “Nanyi msifanye agano lolote na hawa wenyeji wa nchi hii; yapomoeni madhabahu yao. Lakini hamkuisikia sauti Yangu. Kwa nini mmefanya hivi?” (Waamuzi 2:2)
Maelezo ya Ufunguzi: Malaika wa Bwana aliishutumu Israeli kulivunja agano lao pamoja na Mungu. Licha ya uaminifu wa Yehova kwa niaba yao (Amu. 2:1; cf. Law. 26:42-44; Kumb 7:9), wao hawakuwa waaminifu (Amu. 2:2; cf. Kut. 34:12–16). Mungu aliwaamuru “wasifanye mapatano wala maagano yoyote” pamoja na Wakanaani. Walifanya nini badala yake? Walichagua kupuuza maagizo Yake na wakaiasi amri Yake. Kumbuka kwamba kama Israeli ingeendelea kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Bwana Mungu, Yeye, kufuatia hilo, angewapa ushindi kamili. Badala yake, kile kilichopaswa kuwa “sherehe ya ushindi” kiligeuka kuwa “wakati wa kilio kichungu” (Amu. 2:4). Uchaguzi wa Israeli [kutotii] ulimzuia Yehova asiwafukuze maadui wa Israeli watoke mbele yao (Amu. 2:3). Wapendwa, tunafanyaje chaguzi zetu leo (Yos 24:15)? Je, tumeazimu “kumtii” Bwana bila kujali matokeo? Au je, tumekuwa watu wasiofaa, wenye kiburi, wenye mioyo ya mawe wasiojali amri za Mungu? Kumbuka, Mungu, hawezi kutenda mema kwetu ikiwa hatutachagua jambo sahihi (utii).
Maadili ya Kukuza: Kumtii Mungu –(Neno Lake, mapenzi, maagizo Yake); Maombi & Toba halisi.
Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Kusahau yale ambayo Bwana amefanya (Amu. 2:6–10); Kuacha yale ambayo Bwana amesema (Amu. 2:11–13); Kupoteza kile ambacho Bwana ameahidi (Amu. 2:14–15); Kushindwa kujifunza kutokana na kile ambacho Bwana alifanya (Amu. 2:16–23). Dhambi Mahususi — kutozingatia maagizo ya Mungu ya kuharibu sanamu, miungu, madhabahu ya kipagani, na mambo mengine yoyote ya ibada haramu; Kushindwa au kukataa kuwafukuza Wakanaani wote.
Jambo la Kumshukuru Mungu: Katika 2 Timotheo 2:13, Biblia inasema, “Tusipokuwa waaminifu, Yeye hudumu kuwa mwaminifu, maana hawezi kujikana Mwenyewe.”
Watu wa Kuombewa: [1] Mwombee kila muumini awe na uhusiano uokoao na binafsi pamoja na Yesu Kristo; [2] Waombee viongozi wa kiroho waongoze kwa uadilifu na kuweka mfano bora kwa wengine; [3] Waombee Wakristo wote waelekeze macho yao kwa Yesu Kristo – (ikiwa viongozi wa kanisa mahalia ni wapotovu, washariki hawapaswi kudanganyika kufuata kanuni potovu); [4] Mwombee kila muumini ajihadhari hata zaidi dhidi ya uvivu, ulegevu, utepetevu unaoelekea kusababisha anguko lao. Lazima tujikite zaidi kuzingatia neema na huruma ya Mungu ili kuwafikishia wengine upendo Wake. Mara nyingi “tunazungumza juu ya Mungu” lakini mara chache “tunazungumza na Mungu” katika sala.
Masuala ya Kuombea: [1] Ombea ujazo wa Roho Mtakatifu, Utambuzi, na kujifunza Neno la Mungu; [2] Ombea uthabiti – (kudumisha macho yetu kwa Yesu Kristo wakati wote). Hivi ndivyo tutakavyoepuka kupotoshwa katika chochote kilicho nje ya mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu.
Ahadi ya Leo: Shabaha/ Mungu huwapa thawabu wale wanaomtii– “Basi, basi, ikiwa mtaitii sauti Yangu kweli kweli, na kulishika agano Langu, hapo ndipo mtakuwa tunu Kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote ni Yangu.” (Kutoka 19:5) “Laiti wangekuwa na moyo wa kunicha Mimi na kushika amri Zangu zote siku zote, waweze kufanikiwa wao na watoto wao milele!” (Kumbukumbu 5:29)
WAAMUZI 2Z: OMBI LA KUHITIMISHA.
Ombi la Kuhitimisha/ Waamuzi 2, (7-BSG-2Z)/ Je kuna hitaji lolote ninaloweza kuomba/kuwasilisha katika sura hii? Ndiyo.
Maswali ya Moyoni: Soma tena Waamuzi sura ya pili. Linganisha maisha yako ya dhambi na kisa hiki cha Israeli kukengeuka na kurudi nyuma kwa Israeli. Je, picha yoyote inaweza kuchorwa kwa namna ya kushangaza zaidi ya hapa? Ni jumbe ngapi za neema, kama “Malaika wa Bwana” (Amu. 2:1) kutoka Gilgali, ambazo lazima Mungu akutume ili uzikumbuke njia zako na kutubu?
Angalia kusudi la uvumilivu wa Mungu:
- “Au waudharau wingi wa wema Wake, ustahimilivu Wake, na uvumilivu Wake, usijue kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu?” (Warumi 2:4)
- “Je, huoni jinsi Mungu alivyo wa pekee ajabu, mvumilivu na mwenye subra nawe? Je, hii haimaanishi chochote kwako? Hivi huoni kwamba fadhili Zake zimekusudiwa kukugeuza kutoka katika dhambi yako?” (Warumi 2:4, NLT)
Sala: Baba, tunakushukuru tena kwa neno Lako katika Waamuzi sura ya pili. Tunakushukuru kwa zawadi ya uzima, kwa nafasi nyingine ya kuisikia Injili na kufanya mabadiliko ya lazima maishani mwetu.
Tunakushukuru kwa tabia Yako isiyobadilika — Huruma, na rehema! Wewe si mwepesi wa hasira! Uaminifu na upendo usio na kikomo! Uko tayari kusamehe uovu wetu, uasi na dhambi zetu!
Tunakushukuru kwa ajili ya kazi Zako za uumbaji, uumbaji upya, wokovu, na ukombozi. Tunakushukuru kwa baraka za kila siku unazotukirimia — kwa kuwa “ni mpya kila asubuhi: uaminifu Wako ni mkuu” (Maomb. 3:23).
Baba, hii ni sura ya kuhuzunisha. Mafanikio/masuluhisho ya Israeli katika nchi ya ahadi yanadokezwa hapa –(utiifu kwa agano), lakini walifikiri wangeweza kukuasi na kusalimika katika hilo. Kwa sababu hiyo, walishindwa vibaya sana (Amu. 2:2, 4, 14-15, 20-21), na Wakanaani wakawa kero machoni pao na “miiba ubavuni mwao” (Amu. 2:3; cf. Hes. 33:55; Yos. 23:13).
Bwana, tusaidie kujifunza masomo yetu vizuri –(kushikamana na maagizo Yako ya kubomoa miungu yote: sanamu, madhabahu ya kipagani, na mambo mengine yoyote ya ibada haramu). Hebu Roho Wako atusaidie kutambua vile vitu (dhambi) vinavyotutenganisha na Wewe (Isa. 59:1-2), kutubu mara moja na kuanza upya na Wewe.
Baba, tunakushukuru kwa uhuru wa uchaguzi (cf. Mwa. 2:15). Umetupa uwezo wa kuchagua, na mara nyingi, tuna mwelekeo wa kutenda kipumbavu, tukiipita njia rahisi ya dhambi. Ingawa njia hiyo ni hatari kwetu (Mithali 4:12), tuna mwelekeo wa kuifuata, kwa kuwa sisi ni waasi, wakaidi, na mara nyingi tunampinga Roho Wako. Katika siku hii, kila mmoja wetu, baada ya kuisoma sura hii, atubu mara moja na “kuchagua kwa hekima” kukutii Wewe na kufuata Amri Zako. Na hebu tuwezeshe kujitahidi kumgeukia Yesu, kutafuta mwongozo Wake, na kumfuata hatua kwa hatua huku tukiushikilia mkono Wake wenye nguvu.
Baba, tusaidie kuadhimisha yale uliyotufanyia na ambayo umeyafanya ndani yetu na kuwasilisha ushuhuda usadikishao kwa wale wanaotuzunguka. Wasaidie wengine waione Injili ya Yesu Kristo kupitia kwetu na kukulilia Wewe kwa imani, toba, na kujikabidhi Kwako tena. Tusamehe, Bwana mpendwa, na utusafishe tuondokane na udhalimu wote. Roho Wako na aendelee kutusihi, na atufundishe jinsi ya kutii neno Lako, mapenzi, amri na maagizo Yako – Siku Kristo atakapotokea (Tit. 2:13; Ebr. 10:37).
Ni katika jina Lake, tunaomba na kukupa Wewe heshima, sifa na utukufu wote. Amina.