Israeli Ilimwacha Bwana

August 21, 2022 in Usiku by TGVS

WAAMUZI 2Y: SAHAMU YA JIONI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Waamuzi 2, (7-BSG-2Y)/ Dhima: Israeli Ilimwacha Bwana/ Wimbo: Don’t forget, That the Lord is in you. [hymnal.net #  771]


 

Andiko Kuu: “Ndipo wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, wakawatumikia Mabaali; nao wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyekuwa amewatoa katika nchi ya Misri; nao wakafuata miungu mingine miongoni mwa miungu ya watu waliowazunguka pande zote, wakaisujudia; wakamkasirisha BWANA. Walimwacha BWANA na kutumikia Baali na Maashtorethi.” (Waamuzi 2:11–13)

 Swali: Iliwezekanaje Israeli, iliyokuwa imeona nguvu nyingi sana za Mungu kiasi hicho, kuyumba mbali Naye tena haraka sana hivyo? Haikutokea usiku mmoja. Haitokei hivyo kamwe.

[a] Israeli iliacha kile ambacho Yehova alikuwa amesema. “Kama wangemkumbuka Yoshua, wangejua “hotuba zake za kuwaaga” zilizowasilishwa kwa viongozi na watu wa Israeli (Yos. 23–24). Kama wangejua maneno hayo, wangeijua Sheria ya Musa; maana katika jumbe zake za mwisho, Yoshua alisisitiza agano ambalo Mungu alikuwa amefanya na Israeli na wajibu ambao Israeli ilipaswa kuudumisha. Unapolisahau Neno la Mungu, uko katika hatari ya kumwacha Mungu wa Neno, jambo linaloelezea kwa nini Israeli waliigeukia ibada ovu na ichukizayo ya Baali.” – [Warren W. Wiersbe, Be Available, “Be” Commentary Series, (Wheaton, IL: Victor Books, 1994), 18].

[b] Walipoteza ushirika na Mungu. Walikuwa wamejitosa kwenye upujufu, uasherati, na anasa. Walikuwa wamekabiliwa na kiburi na ukaidi (cf. Neh 9:16; Kumb 9:12-13; 2 Flm. 17:14-17; Yer. 7:22-26). Walikuwa wamejitosa kwenye kuabudu sanamu (Waamuzi 2:13; 8:33-34; cf, Kut. 32:1-8; Kumb 12:29-31; 1 Flm. 11:4-6). Wakati Israeli hawakuwafukuza watu kama Mungu alivyoamuru, walikuwa wakipanda mbegu za kushindwa kwao kiroho. Je, ni ‘Wakanaani’ (dhambi) gani unazoendekeza na kuziweka moyoni mwako leo? Kwa nini usiamue leo kumtumikia Mungu aliye hai kwa moyo wote? Kwa nini “usichague leo hii nani utakayemtumikia”? (Yos. 24:15).

[c] Hawakujikumbusha kwa dhati juu ya neema ya Mungu. Walimwacha Mungu “waliposahau yote” aliyokuwa amewatendea. Ndiyo maana katika agizo la Meza ya Bwana katika Agano Jipya, tunahimizwa kama watu “kuendelea kufanya hivi kwa ukumbusho Wangu.” (Luka 22:19). Na kila wakati tunapokuja kwenye meza ya Bwana, tunajikabili wenyewe upya kwa kutumia kweli kuu za yale aliyotufanyia, pale Kalvari.

[d] Walilikataa Neno la Mungu. Waisraeli walianza kuyatazama maisha kwamba jinsi ambavyo Wakanaani walifanya. Badala ya kutawaliwa na kweli za Maandiko, waliathiriwa na mitazamo na misukumo silika zao za dhambi. Mpendwa, kulipuuza Neno la Mungu ni hatari. Tunapoacha kuyasoma Maandiko na kutumia kanuni zake, siyo tu kwamba tunakwama; kwa kweli tunaanza “kukengeuka” kutoka kwa Mungu. Petro anatuambia tulitamani Neno ili tuweze kukua katika nyanja ya wokovu wetu: “Kama watoto wachanga waliozaliwa punde, lazima myatamani maziwa safi ya kiroho yasiyoghoshiwa, ili mkue katika uzoefu kamili wa wokovu. Lilieni lishe hii” (1 Petro 2:2, NLT). Mpendwa, kusoma, kujifunza, na kulitumia neno la Mungu maishani mwetu kunapaswa kuwa lengo letu kuu. Ikiwa unatamani kumtukuza Mungu na kushinda dhambi, wasiwasi, na hofu, basi Maandiko lazima yawe kipaumbele chako.

[e] Israeli walimsahau na kumwacha Mungu wa baba zao (Waamuzi 2:12). Walisahau kuhusu Ibrahimu, Isaka, Yakobo, Yusufu, Musa na Yoshua. Nao wakamwacha Bwana. Si ajabu waliangukia katika ukengeufu, mashaka (utashwisi), kutoamini, na hali ya kudumu ya kukosa uwezo.

Maana ya Kiibada: Nini matokeo ya kumsahau Bwana – [a] Uzinzi wa kiroho (Hos 1:2; Yer. 3:6-10; Hos 4:10-13; 5:4); [b] Jamii kuharibika (Hos 4:1-3); [c] Uangamivu wa taifa (Kumb 8:19-20; Kumb 6:14-15): [d] ] Kifo cha mdhambi (Zab. 9:17; Ayubu 8:11-13; Zab. 50:22; Isa 65:11-12).

Mpendwa, tunaposahau yaliyopita, hatufai kwa sasa au siku zijazo. Imani ya kweli, dini halisi ya Mungu, lazima itufungamanishe kwe mambo yaliyopita ili tuwe tayari kwa siku zijazo. Hakuna kizazi kinachoweza kusahau maisha yao ya zamani halafu kikafanikiwa kwa chochote katika siku zijazo. Na hicho ndicho hasa kinachotokea leo katika makundi ya Ukristo: tumesahau mizizi yetu (Kalvari), matendo makuu ya wokovu wa Mungu, na nguvu ya Msalaba Wake. Tunawezaje basi kutazama wakati ujao ikiwa tunasahau yaliyopita? Tunawezaje kuwa na uwezo (utawala) juu ya dhambi, Shetani, na nguvu za pepo waovu ikiwa tunamwacha Yule ambaye tunapata Kwake nguvu hizo?

Katika somo hili, tunahimizwa kuyakumbuka matendo makuu ya Mungu ya wakati uliopita: “Lakini, zingatia nafsini mwako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako. Na uwafundishe watoto wako na watoto wa watoto wako” (Kumbukumbu la Torati 4:9). Pili, kukumbuka na kudumisha agano la Mungu: “Na agano nililofanya nanyi, msilisahau, wala msiiogope miungu mingine.” (2 Wafalme 17:38). Mwisho, Kumtafuta Bwana: “Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni Yeye, maadamu yu karibu. Mtu mwovu na aiache njia yake, na mtu mdhalimu ayaache mawazo yake; Hebu amrudie BWANA, Naye atamrehemu; na amrudie Mungu wetu, maana atamsamehe kabisa.” (Isaya 55:6–7)


 

Uwe na Usiku Mwema: “Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, Nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.” (Ufunuo 2:4–5)

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email