Herode vs. Mamajusi

April 22, 2021 in Usiku by TGVS

Vidokezo vya Sahamu vinavyoshabihiana na “Mpango wa Usomaji Biblia” wa leo/ Dhima: Herode vs. Mamajusi.


 

Andiko Msingi: “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi Yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.” (Mathayo 2:1–3)

Wazo # 1: Yuko Wapi? Wapendwa, kila moja wetu anahitaji kuuliza maswali haya – Yuko wapi Yesu Kristo leo? Yuko wapi katika maisha yangu? Wapi nakoweza kumpata? Kwa kweli, yuko katika Patakatifu pa Mbinguni (Ebr. 8:1-2) akituombea sisi, akishughulikia mahitaji yete, nk. Lakini hajajitenga, kwa kweli, Yeye ni Rafiki aliye karibu daima, anayefahamu huzuni, masikitiko, dhiki, majaribu yetu, nk. (Isa 53:3; Mat 26:37-38; Yn. 11:35; Ebr. 2:17-18; 4:15; 5:7). Yuko tayari kabisa kusaidia wakati wowote tunapomwita (Ebr. 4:14-16); muhimu zaidi, anataka kustakimu/kudumu pamoja nasi (Zab. 91:1-2; Ufu. 3:20)

Tayari Kristo amekuja Ulimwengu (Mat 17:2) lakini wengi hawalijui hilo. Maandiko yanasema — “Alikuja ulimwenguni, na japo ulimwengu uliumbwa kupitia Yeye, wala ulimwengu haukumtambua [haukumjua Yeye].” (Yohana 1:10, AMP) Kwa nini? Kwa sababu wa kiburi, kutoamini, na kupenda dunia. Kwa sababu walijishughulisha na nafsi pamoja na mambo ya ulimwengu, na tamaa ya makuu na kumiliki mali. Nadhani inafaa tujikumbushe tena, kwamba — “dunia inapita na kutoweka, pamoja na matamanio (shauku za mihemko, hawaa) yake; bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu na kutekeleza makusudi Yake katika maisha haya adumu (huendelea kuishi) hata milele.” (1 Yohana 2:17, AMP) Naweza kuongeza, lakini Yeye ampataye Yesu, na kutii amri Zake adumu milele!

Wazo # 2: Je umewahi kuiona Nyota Yake? Wenye hekima wale waliiona! “Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” (2:2). “Nyota hiyo ilikuwa kundi la malaika wang’aao kwa mbali, lakini kuhusu hili wenye hekima hawa hawakujua. Hata hivyo walivutiwa kwamba nyota hiyo ilikuwa yenye umuhimu maalum kwao. Waliwaendea makuhani na wanafalsafa, na kuchunguza magombo ya rekodi za zamani. Unabii wa Balaamu ulikuwa umetamka, “Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli.” Hesabu 24:17. Ingewezekana nyota hii ya ajabu imetumwa kama ishara ya Yule Aliyeahidiwa? Mamajusi walikuwa wamekaribisha ukweli uliotumwa kutoka mbinguni; sasa iliangazwa juu yao katika miali angavu zaidi. Kupitia ndoto walielekezwa kwenda kumtafuta Mfalme aliyezaliwa.” — [Ellen Gould White, The Desire of Ages, Conflict of the Ages Series, (Pacific Press Publishing Association, 1898), 3:60].

“Wenye hekima hao waliongozwa kutafsiri shani hii ya ajabu kuwa utimizwaji wa unabii wa Balaamu kwamba “Nyota itatokea katika Yakobo” (Hes. 24:17)” – (SDA BC 5:289). Je umewahi kuiona Nyota Yake? Wapendwa, tunapoiona Nyota Yake tunajawa Furaha (Mat 2:10); Tunapoiona Nyota Yake tunamwabudu Yeye (Mat 2:11); Tunapoiona Nyota Yake tunampatia tunu zetu (Mat 2:11); Tunapoiona Nyota Yake tunarudi tulikotoka kupitia Njia Nyingine (Mat 2:12), yaani, “toba ya kweli.” Umefanya hivyo?

Wazo # 3: Kumwabudu Yesu Kristo! Herode hakutaka kumwabudu Yesu—alitaka kumuua. Kwa nini? Kwa sababu alihofu Kristo angeutwaa ufalme wake. Wapo wengi leo ambao bado wangali wanakataa kumtambua Kristo kama Mwana wa Mungu, Mfalme wa wafalme, na kumpatia huduma Yake, kumwabudu kwa jinsi alivyo. Je wewe ni miongoni mwao? Mpendwa, usiwe kama Herode! “Yesu Kristo” ni mada ambayo jamii yote ya wanadamu lazima waizingatie kwa uzito wote Kumkataa Kristo humaanisha upotevu wa milele: mauti ya pili (Ufu. 21:8; Rum. 6:23); kumkubali Kristo humaanisha uzima wa milele (Yn. 3:16; 10:28).

Unauliza— ni tunu za namna gani tunazopaswa kumpatia/kumleta Kristo leo? [a] Dhabihu hai kwa Mungu (Rum. 12:1–2); [b] Kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki Yake (Mat. 6:33); [c] Mali: muda wetu, talanta, zaka/sadaka; [d] Huduma: kumtendea kazi na kumtumikia Yeye (Marko 16:15; Yn. 15:16).


 

Iweni na Usiku Mwema: “Imenipasa kuzifanya kazi zake Yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana; usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi.” (Yohana 9:4) “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.” (Mathayo 9:36–37)

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email