Neno Moja Tu

June 5, 2021 in Usiku by TGVS

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Marko 10, (41-BSG-10Y)/ Mawazo ya Kiibada katika Marko 10/ Somo: Umepungukiwa na Neno Moja.


 

Andiko Makini: “Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. ‘Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.’ Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” (Mk. 10:21–22)

Wazo # 1: Kijana Tajiri alipoteza kila kitu kwa sababu ya “Kitu Kimoja” tu (Mk 10:17-22). Ilimhuzunisha sana Yesu kumwona huyu Tajiri-mtawala mdogo akienda kwa huzuni, lakini Yesu hakuwa na njia mbadala bali kumwacha aende. Yesu hatulazimishi kuingia katika Ufalme wa Mungu, ni chaguo tunalopaswa kufanya sisi wenyewe kwa hiari yetu.

Wazo # 2: Sifa za Kijana Tajiri: Alikwenda kwenye Chanzo sahihi- Yesu Kristo, (Mt 11:28); Swali lake lilikuwa sahihi, “Nifanye nini?” (Matendo 16:30); Alihisi uharaka mkubwa— “kukimbia,” (Mk 10:17); Alionesha moyo mnyenyekevu — “kupiga magoti” (Mk 10:17); Alikuwa na maarifa ya Kibiblia “kutoka ujanani.” Alijua Amri zote za Mungu (Mk 10:20); Hakuwa mbali sana na ufalme –“Kitu kimoja” (Mk 12:34). Lakini, alikuwa na udhaifu (kiburi cha mali) na Yesu aligusa udhaifu huo, (Mk 10:21). Wapendwa, unaweza kuwa na sifa za nje za utaua lakini bado ukaukosa ufalme wa Mbinguni (2 Tim. 3:5) – Pale unaposhindwa kuwasilisha kiburi, ubinafsi, na tamaa ya mali/ utajiri. Je, unakumbuka Maonyo ya Kristo? – “Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” (Mathayo 16:26)

Wazo # 3: Kitu Kimoja” kinaweza kutuibia Baraka Kuu za Maisha – kwa mfano, Jaribu moja lilimgharimu Hawa paradiso (edeni) yake, (Mwa. 3:6); Chakula/ mlo mmoja ulimgharimu Esau haki yake ya uzaliwa wa kwanza, (Ebr. 12:16); Uamuzi mmoja usio sahihi ulisababisha uharibifu wa Lutu, (Mwa. 13:10–11); Mtazamo mmoja wa mwisho wa mke wa Lutu (alipogeuka na kutazama nyuma) kulipelekea kifo chake (Mwa. 19:26); Uongo mmoja tu ulimgharimu Anania maisha yake, (Matendo 5:4); Chuki moja tu kwa ndugu yako, isipotubiwa, huondoa uhusianao kati yako na Mungu wako — “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.” (1 Yohana 4:20).

Wazo # 4: Mwizi pale Msalabani alifanya Uamuzi Mmoja SahihiKisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja Nami peponi.” (Luka 23:42–43) Inashangaza jinsi gani uamuzi mmoja sahihi unavyoweza kubadilisha maisha yako milele zote (Rum. 6:23). Wapendwa, kushindwa kuitikia mwito wa Injili “siku moja” tu kunaweza kukupora Uzima wa Milele, kwa sababu haujui kama utakuwa hai kesho, aidha, hai katika saa moja tu inayofuata; Mungu pekee ndiye ajuaye yajayo. Hivyo basi, ninakusihi Rafiki yangu mpendwa, Roho Mtakatifu anapozungumza nawe kuhusu dhambi zako, na umuhimu wa Toba, je unamsikiliza au anampuuza?

Hitimisho: Jambo moja lilimtenganisha Mtawala Tajiri na wokovu/ Mwokozi wake. Rafiki yangu mpendwa, hata sasa Yesu bado anasihi: Leo, kama mtaisikia sauti Yake, Msifanye migumu mioyo yenu (Ebr. 3:15) Je, utamkubali? Je, wewe pia, utakataa upendo Wake kwa sababu tu ya mali na udanganyifu wa raha za ulimwengu huu? Hebu Bwana akusaidie kufanya uamuzi ulio sahihi leo. Ni ombi langu kwa ajili yako, Amina.


 

Uwe na Usiku Mwema: “Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti Yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa” (Ebr. 3:7-8) “Lakini mwenye haki Wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, Roho Yangu haina furaha naye.” (Ebr. 10:38)

Comments
Print Friendly, PDF & Email