Kuingia kwa Ushindi

June 5, 2021 in Alfajiri by TGVS

Ibada ya Afajiri/ Dhima: Kuingia kwa Ushindi/ Andiko Makini: Marko 11:1-11.


 

Fungu Kuu: “Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; Umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana Juu Mbinguni.” (Marko 11:9–10)

Maswali ya Moyoni: Je, hii ilikuwa safari ya kwanza ya Yesu kwenda Yerusalemu? Ni sikukuu gani iliyokuwa ikiadhimishwa Yerusalemu wakati huu? Kwa nini watu waliweka mavazi na matawi barabarani? Watu waliimba wimbo gani? (mstari wa 9) Ni ufalme gani ambao watu walidhani Yesu alikuwa tayari kuuanzisha? Kwa nini Yesu alikaribisha onyesho hili la umma la kumuenzi kama Mfalme? Kwa nini sasa?

Kwa Kifupi: “Miaka mia tano kabla ya kuzaliwa kwa Kristo, nabii Zakaria hivyo alitabiri ujio wa Mfalme kwa Israeli. Unabii huu sasa unatimizwa. Yeye ambaye kwa muda mrefu amekataa heshima za kifalme sasa anakuja Yerusalemu kama mrithi aliyeahidiwa kwenye kiti cha enzi cha Daudi. – (The Desire of Ages, uk. 569). Safari ya Yesu kuingia Yerusalemu ilihusisha Punda, baadhi ya Mavazi na Matawi yaliyotupwa ardhini na sifa za baadhi ya mahujaji wa Pasaka. Maandiko yanasema: “Na wengi [wa watu] walieneza kanzu zao barabarani [kama tendo la heshima na matumaini mbele ya mfalme mpya], na wengine [walitawanya safu ya] matawi ya majani waliyoyakata kutoka mashambani [wakimheshimu kama Masihi],” (Mk. 11:8, AMP)

Huu ndio wakati pekee ambao Yesu angeruhusu maandamano ya umma kwa niaba Yake. Alifanya hivyo ili kuwalazimisha viongozi wa kidini wa Kiyahudi kufanya maamuzi, wakati wa Pasaka, wakati ilipotawazwa kiungu kwamba afe msalabani. Kumbuka walikusudia sana kifo Chake, kabla ya tukio hili, bila mafaniko (soma Mt. 26:3–5). Watu walilia, “Hosana!” Hosanna inamaanisha, “Okoa sasa, tunaomba!” Ikimaanisha, “Mungu muokoe mfalme!” Wapendwa, wakati Yesu aliingia kwa ushindi mjini humo, alijitangaza Mwenyewe Mfalme! Unajua, Mungu ana ufalme, na ufalme huo una Mfalme, jina lake ni Yesu Kristo. Katika tukio hili, Yesu hakutangaza tu Ufalme Wake, lakini pia alisaini hati yake ya kifo.

Ahadi ya Leo: “Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; Naye atamiliki mfalme, Atatenda kwa hekima, Naye atafanya hukumu na haki katika nchi.” (Yeremia 23:5) “Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka Yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na Ufalme Wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.”(Danieli 7:14). Amina.

Jambo la Kumshukuru Mungu: 1. Yesu Kristo alitimiza unabii wa Zakaria 9:9. (tazama Zab. 118:25-26)/ 2. Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu/ 3. Wakati tukisubiri hapa chini, Yesu hajatuacha yatima, anatupenda, anatujali, anatulinda/ 4. Yesu anakuja tena kama Mfalme wa Wafalme, na Bwana wa Bwana, kutupeleka nyumbani katika Paradiso Yake (Yohana 14:1-3).

Masuala ya Kuombea: 1. Mwongozo wa Kujifunza Biblia katika Injili ya Marko/ 2. Uongofu, Toba halisi / 3. Uamsho na Matengenezo kwa waumini wote hapa katika Sauti ya Injili.


 

Marafiki zangu wapendwa, ni Wasaa wa Ibada ya Maombi! Jisikie huru kutushirikisha Wimbo wowote, au Mzigo wowote unaoweza kuwa nao, na Pamoja, tutamtafuta Bwana katika Maombi. Bwana atubariki sote, tunapo “ANZA NA BWANA!” Amina.

 

Comments
Print Friendly, PDF & Email